Swahili Tales/Sultani Darai

From Wikisource
Jump to navigation Jump to search
Swahili Tales  (1870)  by Edward Steere
Sultani Darai
English translation: Sultan Darai
[ 12 ]

SULTANI DARAI.


Aliondoka sermala, akaenda kuoa mke. Akakaa na mke wake miaka mingi, hatta akapata kijana manamke. Yule mkewe akapatikana na ugonjwa hatta akafariki dunia, akakaa na mtoto wake mdogo.

Akanena, mimi hapo ndipo manamume, ni mtu wa kwenda kazini, na kijana changu nalionaye ni mdogo, afathali nitafute mke, nioe, illi maksudi apate kulea huyu mtoto wangu; kama sikuwa na mke mtoto wangu atathii.

Nduguye akamwambia, astahili uoe, kwani wewe ni mwanamume, mtu mzima tena, na mtoto mdogo, bassi hutaweza, afathali uoe mke, akaaye na mtoto wako, na weye mwenyewe upate kwenda kazini. Akamwambia, vema, mashauri yako mema, bassi weye walionipa shauri hili, nifanyie shauri jema, ni mke upendaye, umwonaye mwema, nami nikubali. Akamwambia, yuko mwanamke mmoja jirani yangu, alikuwa mwanamke wa marehemu Salih, bassi roho yake nimemwona kuwa mwema, kwani alikaa sana na mumewe, sikusikia kugomba, bassi sijui wewe na nasibu yako, lakini mimi nimemwona mwanamke [ 14 ]mwema, naye ana mtoto mmoja mwanamke, alioachiwa na marehemu mumewe.

Akamwambia, bass, enenda kamtake, usikie majibu atakayokwambia, nawe kesho uje unijibu kwa wakati ntarudi kazini. Akaenda, akamwambia yule mwanamke, kuwa manamume amekuja kukutaka, nawe nijibu utakalonambia, nami nende hamjibu. Akamwambia, mimi kumkataa siwezi, kwani hapo nilipo ni mjani, nami na mtoto, bassi nipatapo mume naona raha zayidi. Akamwambia, vema, nitakwenda kumjibu.

Akaenda hatta kwa nduguye. Akamwambia, nimekuja kukujibu majibu yako, walionituma jana. Mwanamke nimemwambia, hakunijibu maovu, amenipa maneno mema ya sharia yenyi njia. Akamwambia, bassi mimi ntakupa nguo na mahari umpelekee, na ukienenda mwambie, haya mahari yako, na hizi nguo zako, kama una neno lingine nambie nikamjibu. Mwanamke akamwambia, mimi sina neno, maadamu yamewasili mahari na nguo, sina jambo nafsini mwangu lingine la zayidi. Nami nakwambia mume wangu na aje siku ya Juma tano.

Akaenenda kumjibu, nimempelekea mwanamke nguo na mahari, nimempa, hamwuliza, una neno zayidi? Akaniambia, sina neno nafsini mwangu zayidi, neno lake ni moja alioniambia, mwache mume wangu aje siku ya juma tano, bass! Akamwambia, Juma tano si mbali, tukijaliwa na Muungu, ni leo juma 'nne hatta kesho imekuwa juma tano. Akamwambia, fanya shughuli zako tayari. Akamwambia, mimi sina shughuli tena, shughuli zangu zimekwisha, ni tayari mimi na mwanangu, lakini weye ndugu yangu enenda kamwambia mke, nao kwao [ 16 ]tayari. Akikwambia, tu tayari, njoo niite twenende wakati umekuwapo naliokwambiwa kuenenda.

Akaenda hatta kwa mke akamwambia, mumewo akusalimu, nanyi huku m tayari? Bwana harrusi ataka kuja. Akamwambia, siye tu tayari twamngoja yeye kuja, na wakati unapita, enenda mwambia upesi aje.

Akaenenda mbiombio akamkuta nduguye akisimama mlangoni, yu tayari kutaka kutoka. Akamwambia, mkewo salaam. Akamwambia, Je! habari gani? Akamwambia, hakuna habari illa wewe upesi unakwitwa, nao huku wa tayari wakungoja wewe kuenenda, haya, upesi, wakati unapita. Wakaondoka, wakitoka nyumbani, wakaenda zao hatta wakifika nyumba ya mkewe, akasimama nje. Akaingia yule nduguye, akamwambia, haya waanawake, bwana harrusi amekuja ataka kuingia nyumbani. Akamwambia, ruhusa na apite. Akaenda.

Wakakaa nyumbani kwake, yee na mkewe na mwanawe na yule mtoto wa mkewe, hatta muda wa siku saba kwisha. Akamwambia, mke wangu. Akamwambia, lebeka bwana. Akamwambia, kesho siku alhamisi nitakwenda kazini, kaa sana na mwanao naye mtoto mdogo. Hatta ussubui walipokucha, akaenda zake kazini.

Mwanamuke huku nyuma akapika chakula akawapa sehemu zao watoto, killa mtu mbali mbali, yule mwanawe akampa wali mwema, na yule mwana wa mumewe akampa ukoko walioungua.

Hatta athuuri akija babaye, Pakua, bibi, chakula. Mwanamke akaenda jikoni akapakua chakula, akaenda kumwandikia mumewe, akampa maji kunawa. Akamwambia, Waite watoto, tule chakula. Mwanamke akamwambia, [ 18 ]Ah! Bwana, watoto wale marra mbili, nami nimekwisha wapa sehemu zao, sikuwafundisha mathehebu mabaya, watoto wadogo wakiisha pewa chakula chao, wakiisha kula marra moja, bass na tungojee chakula cha jioni. Akamwambia, bass mke wangu, nathania hawajala, ndio hakwambia waite, kama wamekula, bass.

Akatoka kwenda zake kazini, mwanamke akapika chakula cha jioni, chalipokwisha chakula, kabla hajaja mumewe, akawapa kulia watoto, akampa mwanawe wali mwema, na yule akampa ukoko, tena walioungua. Kijana akala, akanywa maji, akatoka akaenda kucheza nje.

Hatta jioni mumewe akarudi, akija zake nyumbani, akamwita, Mke wangu. Akamwambia, lebeka, bwana. Akamwambia, chakula kimekwisha? Akamwambia, kimekwisha, bwana. Pakua. Ee walla, bwana. Akaenda akapakua, akaja akaandika, akampa mumewe maji ya kunawa. Akamwambia, mke wangu! Akamwambia, lebeka, bwana. Waite watoto, waje kula chakula. Ah! Bwana, maneno naliyokwambia ussubui hayakukutosha? Akamwambia, maneno gani, bibi? Sikukwambia, vijana hawali marra mbili chakula, utawafundisha mathehebu mabaya. Akamwambia, sina khabari, mke wangu, kama vijana vimekwisha kula, bassi ntakula pekeyangu, mke wangu? Nawe nawa, tule wote. Akamwambia, nnakuja. Akatwaa chicha mwanamuke, akasugua mikono yake. Mumewe akamwambia, mbona unakawia, mke wangu, nami nakungoja tule. Mikono yangu ina masizi, nasugua sana kwa chicha, ipate kuwa meupe, nawe kula ntakuja; upande wangu sitie mchuzi, ntakula kwa kitoweo. Akaja [ 20 ]mwanamke, wakakaa kitako kula, wakiisha wakanawa mikono, wakaondoka.

Akamwambia, mke wangu, niletee tambuu. Mbona tumbako hamna, funua chini ya mchago, akamwambia, nalifahamu kuweka jana tumbako, bassi tezama uniletee. Akaenda mwanamke, akafunua mchagoni, tumbako asione. Akamwambia, bwana. Akamwambia, lebeka, bibi. Mbona nimefunua mchagoni, tumbako sikuiona? Akamwambia, tezama sana, ela tartibu, ukitezama kwa harraka, hutaona kitu. Ee, bwana, natezama kwa taratibu, na tumbako siioni. Akamwambia, tezama illa miguuni. Akafunua kitanda yule mwanamke asione tumbako. Akamwambia, Ee, bibi wee, labuda umekwenda kwa harraka hapo kitandani, tumbako nathani umeyangusha chini. Akamwambia, bwana chini haikuanguka. Akamwambia, kama husadiki nitatwaa taa nimulike hapa chini ya mvungu, kama iko tumbako yako ntaiona. Bassi mulika upesi, nami nimekwisha unga tambuu, nangojea, hiyo tumbako tu, unaitafuta kutwa kamma sindano, ndio huioni, nawe ungeiona sembuse hiyo tumbako, nalo jino zima si kipande kidogo. Ah! Bwana siwezi, njoo tafuta mwenyewe nami huku. Siji nimechoka, tafuta uniletee bass, ufunue mikeka yote ukatezame; hiyo tumbako, bass, imekwenda wapi? Eee! mke wangu, nimesahau iko ndani ya mfumbati kitanda kidogo. Ah! bassi wee, waliotaka kuniathibu, nawe wajua tumbako walipoweka. Walitaka kuniathibu mimi, mwana wa mwenzio. Akitwaa chini ya mfumbati tumbako, akampelekea. Shika tumbako yako, una wazimo wako, hatta mtu wali hujaisha kumshuka matumboni, unaingia ukiniathibu. Ah! mke wangu, nimechoka, nami [ 22 ]nalisahau, bassi kumekuwa wakati wa usiku, waita watoto walale, ondoka kafunga mlango. Watoto wakaingia kwao chumbani kulala, na baba zao akaenda zake kulala.

Hatta ussubui walipokucha, akamwaita, Mke wangu. Akamwambia, lebeka, bwana. Naenda zangu kazini, mtazama mtoto asitoke nje na acheze hapa ndani uwanjani na nduguye. Akamwambia, Ee walla, bwana. Akaenda zake kazini.

Mwanamke akapika chakula akawaita, Watoto! Lebeka, Mama! wakaja wote wawili mbio. Yule mtoto wa mumewe akamwambia, miye, mama. Ah! nalikwitwa mimi mama yako, nalikuzaa lini? Mamako yule amekufa kule, mimi namwita mwanangu, naliomzaa mwenyewe. Yule kijana akazunguka nyuma, akakumbuka, akalia sana, hatta yule mwenziwe akamwambia, dada, unalia nini?

Akamwambia, mimi si dada yako, mama yako ameniambia, mamako yule amekufa, mimi si dada yako, mimi kuwa dada yako ningepewa ukoko wa wali tena ulioungua? Wewe ukapata wali mwema, na kitoweo kukupa, mimi hala ukoko mkavu ila kuwa na mchuzi sababu mimi sina mama, bass; mimi si dada yako. Yule kijana akaondoka akamwita, Mama! Mwanangu! Mbona yule dada amezunguka nyuma analia, mama, umemtendani? Ah! mimi, yule si mwanangu, nalikuzaa pekeyako. Ah! si mtoto wa baba? Akiwa mtoto wa babayo, bassi nimtendeni? Nimtie katika mboni ya macho, utakapojua kweli kamma huyu ni nduguyo. Uss, nyamae si nene, kamwita mle chakula. Akamwambia, dada unakwitwa. Nani ananiita? Unakwitwa na mama. Unanikufuru wewe, sina mama mimi, [ 24 ]mamangu yule amekufa, mwenyi mama wewe tu. Hupewa wali mwema ukila, bassi, uende kwa mamayo. Ee dada, si fanya hasira, twende zetu tukale. Mimi huko siendi, nileteeni wangu papa hapa.

Akaondoka, akaenenda, akamwita mama. Akamwitikia, mwanangu yu wapi nduguyo? Akamwambia, mimemwita, hataki kuja, akaniambia nipelekee wali kuko huko. Akamwambia, yuko wapi? Yuko nyuma uani. Chukua, mpelekea. Akachukua yule kijana, akaenda akampelekea. Dada, dada, wali huu nimepewa kukupa. Akamwambia, wache hapa nitakula. Akiweka wali chini, akashika njia kwenda zake.

Je! umempa wali nduguyo. Nimempa hajala na akaniambia, weka chini, nami nikaweka. Bassi kaa kitako, ule wali wako. Hatta akala, akaisha.

Kamtezame nduguyo amekwisha kula wake. Naye akaenda akamkuta amenamia chini, na machozi humtoka, akumbuka yale yaliotendwa na yule mke wa babaye. Akamwita, dada yangu, usilie sana, kitwa hicho kitakuuma, afathali ule wali. Akamwambia, roho yangu ina hasira, nami nakumbuka ulimwengu rohoni mwangu, wali haupiti, nami njaa ninayo. Kwa nini, ndugu yangu? Akaambia, hivyo tu. Akatwaa ule wali akampa mbuzi.

Marra babaye akaja, akapiga hodi! Mke akaitika hodi! Karibu bwana! Akamwambia, habari ya pwani? Kwema, jua kali, nipe maji kidogo ninywe. Akapewa maji, akanywa. Akamwita, Bibi! Lebeka, bwana! [ 26 ]Chakula kimekwisha. Oh! kimekwisha zamani, bwana, tena wali umepoa. Pakua upesi, nataka kulala.

Mwanamke akaenda jikoni, akapakua wali upesi, akaja akamwandikia mumewe. Akaleta maji ya kunawa. Mumewe akanawa mkono. Akamwambia, waite watoto tupate kula chakula.

Ah! mume wangu huna mashikio? Maneno yayo kwa yayo sikuzote, ela vijana wakae kitako na chakula kimekwisha wakungojea wewe hatta urudipo kazini, saa ya saba? Watoto hawa wangekufa na njaa, lakini miye hupika upesi makusudi, hawa vijana wale na mapema, wasione njaa. Bassi wewe, killa siku unaporudi kazini, huwaite watoto ule nao, wataka kuwalisha marra mbili ao tatu hawa, bassi hayo mambo gani?

Ee bibi sina habari, kama watoto wamekwisha kula, bassi bibi, ningekuwa na habari ningewaita marra ya pili? Lakini nnanena, hawajala, ndio maana hawaita, sasa wamekula, bass! Kanawe, tule.

Na mwanamke akaenda kunawa, wakarudi, wakala. Akamwambia, desturi, mume wangu, ujapo uje shuti waite watoto, huwaambia watoto njooni mle, na desturi za nyumba kwanza huulizwa mke, kwani ndiyo alionao nyumbani, kwani ndiye ajuaye vitu pia vipikwavyo na vibichi, na ashibaye na mwenyi njaa, kwani mke ndiye ajuaye, kwani yee ndiye mpishi, ndiye apakuaye, bassi ukija, mume wangu, sasa desturi ukiniuliza mimi, kwani ndiyo ulioniachia nyumba yako kwani nasikia, ndio mkeo mimi.

Bassi, mke wangu, uwe rathi kwa hili nalionena, na hili nalilokosa, haya walioniambia ndio maneno ya sheria ya [ 28 ]mume atoka amwulize mkewe. Je! bibi, umepika? Je! bibi, watoto wamekula? Je! bibi, chakula ulichowapa watoto kimewatosha?

Bassi nami mke ndio nikujibupo. Ah! Bwana, watoto chakula kimetosha. Ndipo watu wanapokaa na wake wao katika majumba, ndipo watu wakaoa makusudi wakitoka nje wasimwulize mtumwa, wala wasimwulize mtoto, ni kuulizwa mke aliomo nyumbani, ndiyo mwenyi madaraka ya nyumba, ndio maana watu wakaoa wake kutaka haya, akija akute killa kitu nyumbani tayari. Na kitapopungua killa kitu katika nyumba asiulizwe mtumwa, wala asiulizwe mtoto, uniulize mimi mkeo, nilio katika nyumba, ukitaka kunipiga, ukitaka kunifunga, ukitaka kunitukana, ni lile ulipendalo, mume wangu, nikikosa ndilo.

Bassi, mke wangu, nisamehe kwa haya naliyofanya, wala sitafanya tena, bassi nawe, twende zetu tukalale.

Hatta usiku ulipokucha, mumewe kuondoka, akamwambia, bibi, leo mimi siendi kazini, naona maungo yote yananiuma, lakini nitaondoka marra moja, nitakwenda kwa jirani, ntakwenda kucheza bao. Bassi chakula kikiisha, mtume mtoto aje niite. Akamwambia, marahaba, mume wangu.

Mwanamke akaenda jikoni akavunja nazi. Alipokwisha pika wali jua limekuwa mafungulia ng'ombe. Mumewe hajadiriki kwenda kwitwa, amekuja mwenyewe nyumbani. Ee mke wangu umekawia mbona kupika. Nami bwana, nimekwisha kupika, lakini bwana ninakosha sahani, nalitaka kumtuma mtoto kuja kukwita, bassi, bwana, [ 30 ]nipakue? Kama u tayari, pakua. Akaenda akaingia jikoni mwanamke, akipakua sahani tatu, sahani moja ya mumewe, sahani moja ya mtoto wa mumewe, na sahani moja ya mwanawe. Na sahani mbili zile za wali mwema, sahani ya mumewe na sahani ya mwanawe, na sahani ya yule mtoto wa mumewe ametia ukoko wa wali, na ukoko umeungua, na kitwa cha samaki, ndicho alichompa. Mumewe akapelekewa wali, na mwanawe akachukua wake wali, na mtoto wa mumewe akachukua ukoko ule ulioungua. Na yule mume roho yake inasikitika kwa sababu hapati kula na mwanawe sahani moja, na kunena kwa yule mwanamke hathubutu.

Akamwambia, bibi, watoto wamekula? Akamwambia, nimekwisha wapa sahemu zao, wamekula yee na nduguye. Akamwambia, bass, nipe maji ninawe, na akinawa mkono, mume akatoka.

Na yule mtoto wake kule nyuma aliko hakula ule wali, analia, anasikitika kuona mwenziwe ana mwema, naye kula ukoko. Akiacha ule ukoko, akaenda hatta kaburini kwa mama, akaenda akisikitika sana, na kulia sana.

Akizunguka katika nyuma ya kaburi, akaona mtango. Akatazama chini, akaona matango, akichuma mawili, moja akila, moja akachukua kufanya mtoto. Hatta alipofika kule nyumbani. Tango hili umepata api? Akamwambia, tango hili nimechuma kule shambani kwa watu. Akamwambia, nilete tango. Akamnyang'anya, akimpa mwanawe. Yule akakaa kitako akilia.

Hatta babaye alipotoka, amkuta kijana analia. Je! mama, unalilia nini? Akamwambia, sina hatta kitu. Unalia burre? Una jawabu ndani ya roho yako, nambie [ 32 ]jawabu hii, hili linalokuliza nami nipate kulijua. Akamwambia, sina hatta kitu, baba. Akamwambia, itayamkini kulia burre wee? Akamwambia, ninalia tu.

Mkewe akaja. Weye wafanya nini kwa mtoto? Namtezama huyu kijana, namwona akilia, namwuliza linaomliza, hanambii. Akamwambia, wataka nini na kijana, kijana huyu mpumbavu, ana wazimo, huyu amekwenda huko kwenda kwiba tango la watu, amekuja hapa, nimeliona nimemnyang'anya lile tango, nimewapa wenyewe. Bassi kijana huyu anataka kutuvumbulia vita, anataka kutujongea kutukana na watu, atatujongea kupigwa na watu, tezama huyu mtoto wangu, haendi kutwaa kitu cha watu, akiisha kula, hukaa kitako akasuka ukili wake, akichoka kusuka hulala. Huyu mtoto wako hakubali, akiisha kula kwenda ndani ya mashamba ya watu, akitwaa vitu vya watu, hutaka kutujongea sisi maskini ya Muungu. Wakija watu wenyi vitu vyao mimi simo, najitoa, nitawaambia enendeni kwa babaye, kama kulipa ulipe wewe, kama kufungwa ufungwe wewe, kama kupigwa upigwe wewe, na haya yote yatakupata kwa sababu ya mwanao, kwani mwanao hasikii, harudiki, haambiliki. Bassi mtoto huyu mtu mtendani? Bassi mimi nimejitoa, mume wangu, mimi simo kwa sababu ya vitendo vya kijana huyu.

Babaye akamshika mkono yule mtoto, akaingia naye ndani akamfunga mikono na miguu, akamchimbia na mti kati, akamwambia sikufungulii, shuti utakufa papo hapa.

Akamwambia, baba unifungie nini, wanifunga kunionea [ 34 ]kwa kuwa mwanao, ao nimetukana mtu, bass umenifunga kunirudi ili situkane tena mtu, ao nimekwiba mali ya watu, umekuja kustakiwa, bassi umenifunga kunirudi, ili sitwae tena mali za watu?

Akamwambia, wewe umekwenda katika shamba la watu, mamayo ameniambia, ukaenda ukayachuma matango ya watu, wenyewe wakaja wakushtaki nyumbani, mamako amekunyang'anya tango, amewapa mwenyewe.

Baba yangu, sina la kunena, kinwa kimejaa maji, na nikinena nakuogopa, baba yangu, kuona hasira nyingi, ukagomba na mkeo, kwa hayo anitendayo.

Ee mwanangu, unieleze, wala sina hasira, wala simwambii mke wangu, nataka niyajue mimi na roho yangu. Akamwambia, waniona baba ninapokonda. Akamwambia, nakuona, mwanangu. Akamwambia, mimi sipewi wali, ila ukoko, tena ukoko ulioungua, na kunena sithubutu, na mwanawe humpa kulia wali mwema, akampa na mwingine, akamfichia, ussubui ukitoka ukaenda kazini kumwita mwanawe chumbani, akampa ule wali uliomwekewa wa jana, akala pekeyake, na mimi najua sipewi, na kuambia babangu naogopa, kwani ninyi wazee mmenena, hawa waanawake uchungu watoto wao u katika nyonga, na ninyi waanaume mmenena, mtoto mwanamke kwa mamaye mwanamke, nawe, babangu, umeoa huyu mwanamke, anitunze, na mimi mwanao ntaweza mimi kijana kizima mwanamke nikija nikikwambia, baba nna njaa? Nije nikwambie, baba nataka mtama? Mimi mwana mwanamke shuti niende kwa yule mama yangu, nenda hataki nikija [ 36 ]kwako, baba yangu, yule mama kusikia hatanipenda. Atanambia, yule mwana si kitu, ananiacha kuniomba mimi mamaye, shuti akamwombe baba yake, bassi mimi mke wa nini nyumbani?

Akamwambia, kweli mwanangu. Bassi nipe habari ya tango hili, mwanangu.

Akamwambia, tango lile naliokuja nalo juzi, siku ile ulipokuwa hawezi, walipokwenda kwenda kwa jirani kwenda kucheza bao, ukarudi upesi, kabla mtu hajaja kukwita, ukamwuliza mama, mbona kimekawia, jua limekuwa mafungulia ng'ombe, hakukwambia chakula kimekwisha, nali nikiosha sahani, nipate kumtuma mtu, aje akwite? Ukamwambia, kama chakula kimekwisha, pakue. Akamwambia, kimekwisha, akaenda akapakua mwanamke sahani tatu, moja yako baba, moja ya mwanawe, moja yangu. Sahani yako ya wali, naye mwanawe ya wali, yangu mimi imetiwa ukoko tena ulioungua, na kitwa cha samaki. Wangu nikazunguka nao nyuma, hautazama ule wali siwezi kula, nikasikitika sana, nikalia sana, nikanena na mimi mama yangu angekuwa hayi, ningekula wali mwema na mimi, kama anavyokula mwenzangu, anavyopewa na mamaye. Bassi walipokwisha kula wewe baba, waliponawa mkono wakatoka, na mimi nikatoka kwa uchungu wa roho yangu, nikaenda hatta kaburini kwa mama yangu, nikasikitika sana, nikalia sana, tena nikaondoka nikazunguka nyuma ya kaburi, hatazama chini, haona mtango, hachuma matango mawili, moja hatafuna, na moja hachukua mwenyewe kufanya mtoto. Nalipokuja hapa nyumbani, huyu mama akaniuliza, watoka wapi na tango? Mimi simwambii, natoka nalo kaburini kwa mama yangu, [ 38 ]nikamwambia, natoka nalo huko shambani kwa watu, akinyang'anya lile tango, akimpa mwanawe. Bassi mimi tena nikafanya roho yangu hasira, nikafanya roho yangu kuonewa, nikajiinamia hakumbuka mama yangu, hanena tango hili, kama ningekuwa na mama yangu, hangeweza kuninyang'anya huyu, akampa mwanawe. Nami naliogopa kumwambia, matango haya ninakwenda nikichuma kule katika kaburi ya mama yangu, angekwenda marra moja, akaenda akayachuma yote, akampa mwanawe, nami ningeyakosa. Bassi mwenyewe mimi nimeyaacha maksudi kule kaburini, nikiumwa na njaa nikapate moja nitafune, nidanganye roho yangu, na moja nifanye mtoto. Bassi mimi matango yale sikuyaiba baba, kama husadiki baba, mwenyewe enenda hatta chini ya kaburi, kuna matango saba makubwa, na madogo yaliomo na maua, hayana idadi. Bassi umenifunga, baba, kwa kunionea, sina naliolikosa kwako, wala kwa huyu mkewo.

Akamfungua mwanawe, akamwambia, mama niwie rathi kwa haya naliyokutenda, nami sikuyajua, wala sikuyasikia, wala sikuyatambua. Ah! baba yangu, mimi ni rathi kwa lo lote unitendalo. Bassi kesho, mwanangu, ntakununulia mtumwa mwanamke, na nyumba nikuhamishe, nikuweke nyumba ya marehemu mamayo, wewe na mtumwa wako, na chakula ntakupa.

Hatta usiku walipokucha, akaenda zake sokoni, jua limekuwa saa ya tatu, akazabuni mjakazi mzuri ampendaye, akampeleka nyumbani. Akamwambia, mwanangu, huyu mtumwa wako, huyu ndiye ni yaya yako, huyu ndiye mama yako, bassi nawe kaa naye. Wee Mjakazi! Lebeka, Bwana. Mimi nimekununua sababu ya mwanangu, umpikie [ 40 ]chakula chema, umvike nguo njema, umtandikie kitanda chema, umzumgumze mazumgumzo mema, huyu ndiye mamayo, huyu ndiye babayo, huyu ndiye mumewo, huyu ndiye shogayo, huyu ndiye mwanao. Bassi, tafáthali mtunze sana mtoto.

Mwanamume akaondoka hatta akafika kwake mwanamke wake. Mkewe amepata habari, kama mumeo amenunua suria, ame'mweka nyumba marehemu mkewe, bassi akanena mwanamke, nyumba hilo akija haingii, atamrudia suria hiyo, aliko'mweka, ao tutakwenda zetu kwa Shekhi sasa hivi, akaniache, simtaki mume huyu tena. Ah! mume akinunua suria, miye anitakia nini tena?

Marra mwanamume amekuja, mwanamke akatwaa mguu moja huku, na moja huku, akatanua katika mwango, kungoja mumewe akija, asipate njia ya kuingia ndani, akatanua na yote mikono miwili mwangoni.

Alipotokea mumewe, amwambia, Rudi, rudi, koma sije nyumbani kwangu, usije, huko ulikonunua suria na nyumba ulio'mweka, rudi, kakae kuko huko, nyumba hii yone paa usije mwangoni kwangu.

Oh! Mwanamke, una wazimo uningoje kwanza ukaniuliza. Pa! ukanirukia. Niite faraghani nyumbani uniulize, umekaa mwangoni hapo mguu huku, mguu huku, mkono huku mkono huku, umewamba mwango, watu pia wakipita wakuone umesimama hivyo katika mwango, hutahayari nafsi yako?

Sitaki maneno yako leo, rudi kuko huko, rudi kuko huko, usiingie nyumbani mwangu.

Ee, bibi yangu, tafáthali uniache haneno nayo maneno matatu.

[ 42 ]Ee mwongo, mimi sitaki maneno yako leo, mimi nataka uniache tu, ukae na suria yako.

Marra pale akaja mtu, akamwita, Fundi! Ameitika, lebeka. Akamwambia, nna maneno matano nataka kukwambia. Akamwambia, Ee walla. Akamwambia, bassi njoo, tukanong'one. Akamwambia, Ee walla. Akamwambia, kuna mtu ataka mwanao kumoa. Akamwambia, vema mimi napenda sana. Akamwambia, wamwona ugomvi kwa nyumba hapa, mimi na mke wangu, kwa sababu ya kijana huyu nimemnunulia mtumwa, bassi mke wangu amenena ni suria yangu mimi, bassi afathali aolewe mwanangu, na mimi nipumzike. Akamwambia, na mimi nimekubali. Bassi akaenda kwenda kumjibu yule mwanamume anaoposa maneno aliojibiwa na babaye mchumba wake.

Hatta alipokwenda akamwita yule mwanamume anaoposa, akamkuta nyumbani amelala, akamwambia yule mtoto alioko nyumbani, mwamushe marra moja, amenituma maneno, nataka kumjibu majibu naliopewa huko ntokako. Akamwambia, Ee walla. Akaingia mtoto hatta ndani, akamwamusha, baba! Akaitika na'am, mbona uniamsha? Waniamushia nini, usingizi wangu haujaniisha? Akamwambia, ni tume wako, waliokomtuma amekuja kukujibu. Akanena, bashire kheiri. Akaondoka hatta nje. Akamkaribisha, Karibu, Je! habari za huko utokako. Akamwambia, huko njema, sijui wewe nafsi yako. Akamwambia, nafsi yangu nimetangulia kupenda, haikutangulia kuiza.

Akamwambia, nimetumwa na mkweo, Salaam nyingi, baada ya salaam, hapana zema walizomtenda kamazo. [ 44 ]Bassi yeye yu tayari, fanye nawe yako shauri. Akamwambia, mimi sina shauri, shauri yangu imekwisha, ni kukupa nguo, na mahari, na mkaja, na kilemba, na ubeleko.

Bassi nipe upesi, nipeleke kabla jua halijachwa. Akamwambia, zote tayari, nimekwisha kuziweka, nalikungoja wewe kutwaa, na wewe wazitaka, tayari. Ingie ndani kanipe upesi, nami nna shughuli, ntakwenda zangu.

Mwanamume akaingia ndani, akaenda akatwaa mahari, akaenda akatwaa kilemba, akaenda akatwaa mkaja, akaenda akatwaa ubeleko. Akaisha akamwambia, na kiosha miguu, chukua, na kifungua mwango, chukua. Akamwambia kipa mkono ntachukua mwenyewe. Bassi nawe enenda uwapelekee na salaam, mimi huku ni tayari, nangoja wao waje waniite.

Akatoka akachukua zote alizopewa, akaenda hatta kwa babaye yule mke, hako, akamwambia mkewe, kendapi huyu mumeo? Ametwambia anazunguka nyuma kwa jirani, kwenda kucheza tiabu, alitwagiza, uje hapo tume, mtoto akamwite.

Akanena, bassi upesi, kaniitieni, nami hapa namngoja. Akaondoka mtoto, akaenda mbio hatta pale nyuma kwa jirani, akamwona babaye anacheza tiabu, akampungia mkono kumwita. Babaye akatambua, akawaambia, Mimi naondoka jamaa, akaja mtoto kuniita, labuda nyumbani kuna shughuli. Wakamwambia, Haya, enenda.

Akaenda hatta kwake, akamwona tume wake anamngoja barazani, Je! umekuja. Amwambia, nimekuja, bwana. Habari za utokako? Akamwambia, Habari za nitokako njema sana, tena za kufurahisha, tena za kupendeza, amana yako imekuja, ya kwanza hii mahari, za pili hizi [ 46 ]nguo, cha tatu hichi kilemba, la nne huu mkaja, la tano huu ubeleko, cha sita hichi kiosha miguu, cha saba hichi kifungua mwango, na hizi ndizo nalizopewa kukabithi, na kipa mkono amesema atakuja nacho mwenyewe, naye akasema yeye huko yu tayari akungoja wewe kwenda kumwita. Amwambia, nami sina shughuli, muhulla wangu leo, hatta kesho atapata mkewe.

Akachukua nguo zake, akaenda nazo ndani kwa mkewe. Akamwambia, mke wangu mwite mtoto kumwonya nguo zake, kumwonya na mahari yake, afanye atakalofanya.

Akamwita mtoto, Mama njoo, hizi nguo zako zimetoka kwa mchumba wako, na haya mahari yako, na hizo zalizobaki ni ada zetu, ni mimi na babayo.

Akamwambia, bassi mama, laliokwisha kwenu, mimi naweza kulirudi? Ni lile mpendalo nami nimependa, siwezi kumpaka baba angu uso mavi, apitapo asipate kufunua macho, napenda nimfurahishe baba yangu apitapo afunue macho, acheke kama ada, kama walimwengu wachekavyo, anene kama ada, walimwengu wanenavyo, atembee kama ada ya walimwengu, watembeavyo, nami sipendi kuipata kasarani ya baba yangu, napenda kama watu wakaavyo na baba zao, nami ni vivyohivyo.

Akamwambia, vema mwanangu, umenena maneno yapendezao, mimi nalithani mwanangu, utaniinamisha uso mbele za watu nawe umeniinua uso mbele za watu. Muungu akupe kukua mwanangu, uwe na moyo mzuri kama haya walionijibu, kwani ni maneno yenyi njia, nami baba yako nimefurahiwa.

Bassi, wakakaa kitako nyumbani wakati kutengeneza [ 48 ]shughuli zao, hatta ussubui. Siku ya pili ile wakampelekea habari mume, Umekuwa wakati, njoo, uoe, upate kuingia nyumbani. Yule mjumbe akaenda hatta akafika kule nyumbani akamkuta yule bwana amekaa barazani, awangoja watakaomwita. Akamwambia, bwana unakwitwa, wakati umewadia. Akamwambia, mimi tayari, Ee wala.

Akaondoka yeye na jamaa zake, wakaenda, hatta wakifika katika ile nyumba ya mkwewe, akapiga hodi! Akamwambia, hód! karibu Shekh, karibu na wangwana. Akamwambia, tumekaa. Wakapita barazani, wakaenda, wakaita mwalimu. Akaja akawaoza. Kwa kuondoka wale watu wakapewa wali, wakala, wakafanywa na uzuri sana, wakaambiwa, wangwana karibuni. Wakamwambia, na wewe, bwana harrusi, kua heri. Wakatoka, wakaenda zao.

Akaingia ndani katika nyumba yake, wakakaa katika nyumba ile ya mkwewe muda wa siku saba, zalipotimu.

Akamwita mkwe, akamwitikia, labeka. Akamwambia, nna maneno matatu nataka kukwambia. Akamwambia, Bwana, Shekhi langu, licha ya matatu, hatta kumi na matatu, sijione hasara kunambia. Akamwambia, sina zayidi ya matatu haya. Akamwambia, Ee walla, nambie. Akamwambia, la kwanza, nataka unipe rukhusa, mimi na mke wangu kwenenda kwangu, la pili, sikasirike kwa haya nnaokwambia, la tatu, nataka unipe ruksa leo kabla ya kesho, kwani nimeona leo siku njema ya kutoka, mimi na mke wangu. Na wewe si nene, tumekimbia, utatuona ussubui na jioni, hatta labuda wewe mwenyewe ushibe, wewe, mwenyi kujiwa.

[ 50 ]Akamwambia, mimi sina kasarani kwenu, napenda killa siku mje kwa killa wakati, mje nimtazame nami mwanangu huyu mmoja, sipendi kumkosa sana. Akamwambia, Inshallah, bwana.

Hatta jua lalipokuchwa wakihama yeye na mkewe, wakaenda zao kwake. Wakakaa sana na yule mwanamke, wakapendana sana. Na yule mwanamke akampenda sana mumewe, mapendo asiokuwa na kifani. Ampenda sana mkwewe yule mwanamume, asiokuwa na kifani.

Wakakaa miaka mingi, wasigombe yeye na mkewe, wala wasigombe yeye na mkwewe. Wakakaa watu hawa, mashauri yao mamoja, hatta yule mkwewe akapatikana na farathi akafa. Wakasimama, yeye na mkewe, wakamzika.

Wakakaa muda ya miaka mingi kupita, akapatikana na farathi mkewe, akafa, akasimama akamzika.

Bassi akakaa kitako yeye pekeyake, akakaa muda ya siku nyingi kupita, akafanya mambo ya asherati, killa alichonacho kikampotea, kwa uasherati mwingi.

Akakaa mtu wa kuomba, killa nyumba huenda akiomba, akipata. Akapita siku zile, nyumba alizo akaenda akiomba, asipewe kitu tena. Akaregea katika jaa, akapekua kama kuku, akipata punje za mtama, akitwaa akila, muda ya siku nyingi.

Hatta siku hiyo, akienda jaani akaenda akipekua, akapata themuni ya mzinga, akainama marra ya pili, akapekua jaani, asipate hatta punje moja ya mtama. Ahh! mimi nimepata themuni hii ya mzinga, bassi ntakwenda zangu, nikalale. Akaenda hatta nyumbani, akatwaa maji, akanywa, akatwaa na tumbako, akatafuna. Ndicho kitu [ 52 ]alichokipata siku ile, ile themuni ya mzinga, na maji ya kunywa, na tumbako kutafuna. Akapanda kitandani kulala.

Hatta ussubui walipokucha, akaenda zake jaani. Akitupa macho njia kuu, amwona muhadimu na tundu la mibaazi. Akamwita, Ee! Muhadimu, umechukua nini ndani ya tundu hilo? Akamwambia, Paa! Paa! Akamwambia, Lete! Lete!

Pana watu wamesimama watatu, wakamwambia, wewe muhadimu, una kazi. Kwa nini, bwana zangu? Yule masikini hana cho chote, hohe hahe. Akawaambia, labuda bwana anayo. Hanayo, wamwona nawe jaani haondoki, hupekua kama kuku, killa siku hupata punje mbili za mtama, akatafuna; kama ana kitu, hangalinunua mtama akale, angetaka kununua paa? Hawezi kujilisha nafsi yake, ataweza kumlisha paa?

Akawaambia muhadimu, Yee, bwana, simjui mimi, nimechukua biashara, aniitaye yote namwitika, na akiniambia njoo, nikaenda, nitamjua huyu mnunuzi ao huyu si mnunuzi? Ntagomba na watu? nimechukua biashara nikiitwa nisiende? Ada ya mchukua biashara, aitwaye na yo yote hwenenda, akiwa mdogo akiwa mkubwa, akiwa mke, akiwa maskini, akiwa fukara, mimi hayo siyajui, mimi mchukua biashara, aniitaye yote huenenda.

Oo, bassi wewe husikii maneno yetu hayo tuliokwambia, tumeona kwake, nasi twamjua kama huyu si mnunuzi. Akaondoka yule wa pili akamwambia, Hoo! maneno gani hayo, labuda Muungu amempa, ao Muungu atakapompa, atakwambia leo fullani nimempa, njoo mtezame?

[ 54 ]Akaondoka yule wa tatu, akanena, Hoo! dalili ya mvua si mawingu? Bassi sisi hatta dalili zake hatukuzipata za kupata huyu.

Akaondoka yule muhadimu, akanena, mimi, waungwana, nitakwenda, kumsikiliza anaoniita, kwani mimi nimetoka tokea kwangu shamba, hatta kufika hapa ndipo, nimekwitwa na watu wengi, hawapungua khamsini ao kama si zayidi, naye hapana mtu mmoja alionunua. Na hawa wote wana mali, si kwamba nga maskini, nao hakununua, bassi nami pia hao nalionyesha wakatazama, wakaisha wakaenda wakaniambia, Chukua. Killa endapo ikawa kazi ni hiyo. Lete paa, hupeleka wakatezama, Ahh! bassi, ghali, chukua. Nami hichukua. Huondoka nikienda mbele, Ewe muhadimu, ewe lete paa, lete. Nami hupeleka, nikatua wakatazama. Ah! paa wazuri, lakini ghali, chukua paa. Nami hichukua, nami nisikasirike, ni ada ya mchukua biashara ya kwitwa hapa na hapa, na kutua na kujitwika, nami nisikasirike, kwani ni ada ya biashara, humjui atakayonunua, wewe hunena, labuda huyu atanunua, huyu atanunua, hatta upate mnunuzi hatta kununua.

Bassi wewe maneno yetu huyashiki, umetolewa wingi wa maneno na wingi wa masaala, enenda zako maskini.

Bassi wale wakanena wale watu watatu, 'M! Bassi nasi tutamfuata, kamtazame yule maskini, atanunua kweli.

Ee, bwana, apate wapi yule? Maneno gani hayo? 'M! dalili za kupata mtu hazionekani. 'M! tokea kufa mkewe, yule akatoa mali yake akafanya uasherati, haipungui mwaka wa tatu, hajui chakula cha moto tumboni mwake. Bassi mtu asioweza kupata chakula cha moto tumboni [ 56 ]mwake, itakapokuwa siku kumi kwa siku moja, atapata kitu kununua paa? Lakini twende tukamtazame, Muhadimu, twende tukamtazame yule asharati anaosumbua nafsi yake kupiga kelele, na kukusumbua wewe mwenyi mzigo kitwani, ila twende tukamtazame atanunua kweli, kama hatanunua killa mtu atampiga bakora moja moja, apate kutubu, siku ya pili akimwona mtu na mzigo wake, asimwite.

Wakaenda hatta wakafika. Ah! hawa paa, nunua bassi, nataka paa, nataka paa, hawa, ewe maneno si kitendo. 'M! Utatamani kwa macho, hutashika kwa mkono.

Akamwambia muhadimu, Paa wako kiassi gani? Wakaruka wale watu watatu. Ee mwongo, Ewe unajua killa siku paa wanauzanya wawili kwa robo. Bassi, akamwambia, nataka mmoja kwa themuni. Ee mwongo wee, una themuni wee, umepata api? Akamtia mdukuo.

Wamenitilia nini, bwana, mdukuo burre? Nimekutendani? Nimekutukana, nimekufyonya? Nimekutwalia chako? Mimi namwita huyu mwenyi paa kununua hawa paa wake, mmetokea ninyi pingamizi, mwataka kuniharibia hii biashara, nisipate? Akashika utamvua wa nguo, akifungua ile themuni, akamwambia, twaa, muhadimu, nipe paa wangu mmoja nitazame. Akatwaa muhadimu yule paa. Huyu, bwana, chukua. Muhadimu akacheka yeye, mbona ninyi wenyi kanzu na vilemba, na panga na majambia, na viatu miguuni, nanyi ni wangwana wenyi mali, hamkosi, nanyi mmenambia, huyu ni fukara hohe hahe, hana mbele hana nyuma, naye ameweza kununua paa wa themuni, nanyi kuwa wangwana bora na mali kwenu tele hamkuweza kununua hatta nussu ya themuni, [ 58 ]na yule mwaliomnena maskini naye fukara, hohe hahe, hana mbele hana nyuma, naye ameweza yeye kunipunguza mzigo wangu, nanyi wangwana bora hamkuweza akali ya nussu themuni.

Yule maskini akapokea paa wake, akaenda zake pale katika jaa, yeye na paa wake mkononi, akainama kupekua pale jaani, akapata punje za mtama za kutia kinwani mwake, akapata na kidogo punje za mtama akampa paa yake. Akashika njia akaenda zake, akaenda kule nyumbani pale panapo kile kitanda anacholala, akatandika mkeka wake, akalala, yeye na paa wake, pahali pamoja. Hatta usiku ukacha, akaondoka akamchukua na paa wake, akaenda zake hatta palepale jaani, akipekua akapata punje za mtama zinazopata ukufi, akatia kinwani mwake, zaliobaki akampa paa wake. Akaondoka akaenda zake hatta nyumbani kwake, ikapata muda wa siku tano.

Yule paa usiku akinena, akamwita, Bwana! Yule bwana wake akaitika, Labeka, akamwambia, mbona mimi nimeona ajabu?

Paa akauliza, ya nini hii ajabu walioiona hatta ukasituka, hatta ukaghumiwa, hatta ukadaghadagha nafsi yako?

Akamwambia, haya nalioona si haba, ya wewe, paa, kunena.

Akamwambia, wewe umekuupuka na rehema ya Muungu?

Akamwambia, mimi toka asili za baba zetu na bibi zetu na jamii ya watu waliomo katika ulimwengu, sikupata kusikia mtu mmoja kunihadithia kama paa walifahamu kunena.

Bassi, wewe usitaajabu, Mwenyi ezi Muungu anaweza [ 60 ]yote, kuyafanya ya kunena mimi na mgine kuliko mimi. Wewe sasa huna haja, sikiliza haya ninaokwitia.

Akamwambia, vema, sasa nitasikia, nami nieleze kiada, hatta mambo nisikie.

Akamwambia, la kwanza, mimi nimekukubali kuwa wewe bwana wangu, tena umenigharimia kwa kitu ulichonacho, nami nimeona hali yako thaifu, siwezi kukukimbia wallakini mimi nitakupa wahadi nitakaokwambia, nawe shika.

Akamwambia, Inshallah, wahadi wako utakaonipa utapokuwa mwovu, kwangu mwema, na uwapo mwema, na kwangu zayidi kuliko mwema.

Akamwambia, la kwanza, bwana, nitakwambia wewe bwana maskini, na makuli yako nami bwana nayajua, wewe mwenyewe wayaweza, na kuyaweza kwako ni ukwasefu, bassi kama mimi mtumwa wako wa zakula zile ulazo mimi kwangu ni kuthii wala sina tabassám.

Akamwambia, Bassi wewe wapendaje?

Akamwambia, Bwana wangu, ni mimi nipendalo, nataka uniwie rathi sana, kwani nitanena maneno yatakaokuwa hayakupendezi, ni maneno ya kukasiri.

Amwambia, wewe hukuwa paa tena, umekuwa mwanangu, na uchungu wa mwana ni katika nyongani mwa nina. Akamwambia, bassi wewe unene lo lote ndilo.

Akamwambia, nataka unipe ruksa, mimi tena unisamehe, nataka unipe ruksa nikienda nikilisha hatta jioni, nikirudi nikija nikilala, kama roho yako haistaamani kwa haya nnayokwambia. Kwani yale makuli yako ni machache nami ni kidogo, naye ndio maana nisiweze kukufuata tukila wote, bassi nataka unisamehe tena, na roho yako nayo [ 62 ]amini kama mimi nitaregea, nami Bwana, kua heri, nakuaga, natoka naenda zangu.

Akamwambia, haya enenda. Paa akitoka mbio, na yule maskini akatoka mbio ndani, akasimama uwanjani. Na paa amezidi kwenda mbio. Yule maskini akapigwa na msangao na machozi yakamtoka. Akapiga ukelele moja, yule maskini. Mama yangu, ee, na mikono katika kitwani. Akapiga ukelele wa pili, Baba yangu, ee! Akapiga ukelele wa tatu. Ee, paa wangu amekimbia.

Wale jirani waliopo wakaja wakamzomea, wakamwambia, wewe mpumbafu, wewe barthuli, wewe asharati, umekaa jaani siku kathawakatha, umepekua kama kuku, hatta Muungu amekupa themuni ile, usiweze kununua muhogo, ukale, ukanunua paa, tena umemwachia, walia na nini sasa, kilio cha mwenda nguu.

Akanyamaa, shukuru. Akaondoka, akaenda zake maskini, akaenda pale jaani pake, akapata punje za mtama, akarudi nyumbani, akafanya ukiwa.

Hatta yalipokoma maghrebi akija paa wake. Akacheka sana maskini, Muungu akusimika, ah! umekuja baba.

Akamwambia, si ule wahadi naliokupa? Akamwambia, nakuona themuni walionunua mimi kwako, ndio lakki yako ya mali, nami naona hasara utwae lakki yako ya mali enda kuwapa watu wangine sasa nikikukimbia. Nimekwenda zangu mwituni, amekwenda mtu ameninasa ao methali amekuja mtu amenipiga bunduki; amenipata mtu mgine. Bassi uthia wote unipatao wa nini nikutie hasarani, siwezi. Nikikwenda nikichuma, jioni nije nilale.

[ 64 ]Ah! vema baba yangu, Muungu akupe huruma. Wakaingia kitandani wakalala yee na bwana wake. Paa siku ile tumbo limeshiba sana majani.

Hatta ussubui walipokucha, akamwambia bwana, naenda zangu, kulisha. Akamwambia, enenda kwa afya na nguvu. Bassi paa akaenda zake, na bwana wake akitoka kwenda zake jaani, wale jirani zake wakimnena. Ah! maskini mwenyi wazimu, labuda huyu mchawi, paa jana siye tukanena hatarudi tena? Kumbe jana jioni akarudi, akalala humuhumu ndani mwake? Sasa hivi ussubui huu, paa ametoka huyu mbio akaenda zake njiani, bassi yale makelele aliyopiga jana, ana wazimo ya kumlilia paa wake, mbona leo amwachia tena? Huyo si burre, nathani ana wazimo, tena wa siri haujawa wa thahiri. Bassi wakaondoka wale jirani, maskini akarudi kwake.

Na yule paa jua lalipokuchwa akarudi nyumbani kwao, amekuta bwana wake amelala anatafuna tumbako, alipokuja yule paa akitwaa mguu wake akawinua aka'mweka nao ndevuni. Akamwita.

Ah! huko utokako kwema? Akamwambia, ah! kwema sana, leo bwana nimekwenda pahali pana majani mazuri, tena pana na mvili, tena pana na baridi, bassi nalipokula majani yale hatta nikashiba, tena pana na faragha, tena pana na mto, bassi hula nikilala nikapunga na upepo, nikatelemka mtoni hinywa maji, hurudi nikaja nikalala, nikapunga na upepo, kazi yalikuwa hii hatta wakati wa kurudi, yalikuwa kazi ya kula, na kulala, na kupunga upepo, kushuka mtoni kunywa maji, hirudi hipunga upepo, bassi roho yangu yanena vema leo, sababu nimestarehe [ 66 ]sana kwa majani hayo, na mvili huo, na upepo wa hapo, gissi ulio mwema, tena na mto karibu, tena pana na faragha, hapana njia, hapana nyumba karibu, hatta mto wenyewe u katika magugu, na kesho nikiamka nitakwenda kuko huko.

Amwambia, ukiamka ukaende, bwana. Wakalala.

Hatta ussubui kulipopambauka akatoka paa mbio, akaenda zake, akakutana na watu yule paa—huyo, huyo, paa wa maskini mkamateni, huyo, huyo, kamateni paa wa maskini, kamateni, kamateni, wasimpate. Paa akakaza mbio, akaenda zake. Wale waliomfukuza wakarudi.

Hatta muda wa siku tano yule paa alipokwenda kulisha, akaenda palipo mti mkubwa, u katika miiba, u katika msitu, yule paa amechoka jua, akanena, pale penyi mti mkubwa nikajifiche hapo pale pana mvili nipumzike hili jua. Akaenda, akalala, pale penyi mti ule mkubwa. Muda mkubwa waliopita kulala kwake yule paa pale penyi mti mkubwa ule.

Akiamka akizungukazunguka chini ya mti ule, akaona pahali pamefanya majani kichungu, akainua mguu wake, akapekua, akaona almasi kubwa mno, inang'ara sana. Ooo yule paa akasangaa, haya ndio mali, hii ndio ufalme, lakini nikimpelekea bwana wangu hii, atauawa, kwani maskini ataambiwa, umepata api, akinena nimeokota hasadikiwi, hatta atakaponena nimepewa hasadikiwi, bassi ya nini miye kwenda kumtia bwana wangu katika matata? Ntatafuta watu wenyi nguvu, nao ndio wawezao kuila.

Akaondoka paa mbio, akaingia katika mwitu, naye almás [ 68 ]akaiuma kinwani, akaenda mbio sana katika mwitu asipate mji siku ile, akalala mwituni, hatta ussubui wa pili, akaondoka kabla ussubui haujapambauka, akaenda mbio hatta jua lalipokoma mafungulia ng'ombe makuu, akapumuzika, hatta lalipokoma jua vitwani akaenda zake mbio sána na almás yake kinwani, hatta jua lalipokuchwa akalala ndiani. Hatta ussubui walipopambauka, akaenda zake mbio akajitahili kwenda mbio sana hatta lalipokoma mafungulia ng'ombe madogo akapumzika akaona dalili za mji karibu akaenda zake mbio akaenda mbio sana, hatta lalipopinduka jua vitwani, akiona dalili ya majumba na mji asiweze kusimama tena, akakaza mbio sana akaenda hatta akiwasili katika njia kuu ya katika ule mji, na ile njia imekabili nyumba ya Sultani. Akaenda zake hatta akiona nyumba ya Sultani imefafanukia. Akazidi kukaza mwendo, na mle katika njia anapopita, watu wamesangaa, wamemwona paa mbio na kitu ndani ya majani amekiuma kinwani, amelekea nyumba ya Sultani.

Wale watu waliomo katika mji walisangaa hatta paa akiwasili pale mwangoni pa Sultani, na Sultani amekaa mbele ya mwango. Paa akapiga, hodi! hodi! Ameitupa chini almas, naye amekaa kitako pale njiani kinatweta, akapiga marra ya pili, hodi! hodi! Sultani akanena, sikilizeni hodi inaopigwa hiyo. Wakamwambia, bwana, hodi inapigwa na paa. Akawaambia mkaribisheni, mkaribisheni! Wakaenda watu watatu mbio, wamwambia, haya, ondoka, unakwitwa, karibu. Akaondoka paa, akainua ile almasi yake, hatta pale pa Sultani, akiiweka chini ya miguu ya Sultani.

Akamwambia, Bwana, Masalkheri. Sultani akamwitika, Allah masik bilkheri, karibu. Nimekaa, Bwana. Sultani akaamuru, asikari, leteni busati, leta na zulia, lete na [ 70 ]takia. Marra pale yamekuja yakatandikwa pale. Akamwambia paa, kaa kitako pale. Ah! bwana, hapa patosha nalipokaa, mimi mtumwa wako, mimi kulala chini ni kuona vema, sembuse hapa pametandikwa jamvi. Akamwambia, huna buddi ukaondoke ukakae palepale. Akaondoka akaenda akakaa. Akaamru Sultani kuletewa paa maziwa, akaamru kuleta wali, yakaja maziwa na wali, akala, akaisha wali akanywa na yale maziwa; akaachwa pumzika muda kidogo.

Akamwuliza, nipe khabari yako waliojia. Akamwambia, bwana, nikupe habari naliojia mimi, nimetumwa kuja kukutukana, nimetumwa kuja kukutaka shari, mimi nimekuja kutaka kwako ugomvi, mimi nimetumwa kuja kutaka kwako udugu na ahali.

Sultani akamwambia, Auu! paa, wewe wajua kunena, akamwambia, mimi namtafuta mtu wa kunitukana, mimi namtafuta mtu wa kunisengenya, mimi namtafuta mtu wa kutakana udugu na ahali, nami nimempata kheri, akamwambia, bassi ukanambia maneno yako.

Akamwambia, u rathi Sultani? Akamwambia, elfu marra. Akamwambia, bassi kama u rathi, funua hiyo amana yako. Sultani akainama akaitwaa, akaiweka panapo paja lake, akifungua mwenyewe bi nafsi yake, alipoona almas ile, akataajabu sana Sultani, kwa ginsi yalivyo njema, kwa ginsi inavyotoa nuru. Akaona roho yake Sultani, ametenda zema sana, zisizokuwa na kifani zema zile. Akamwambia, nimeona amana yangu.

Akamwambia, bassi nimekuja na amana hiyo, nimepewa na bwana wangu, Sultani Darai, bassi amesikia, una mtoto [ 72 ]mwanamke; bassi amekuletea hii, nawe mwie rathi, mstahimilie, amekuletea kitu kisichokuwa sawa nawe, kwa nini kitu kidogo.

Sultani akamwambia, Allahu, mimi ni rathi sana, mimi ni rathi sana, hatta kaburi yangu nikifa i rathi kwa haya alionitendea Sultani Darai. Akamwambia, marahaba, ahsánte, ni rathi sana, mke mkewe, ndugu nduguye, mtumwa mtumwa wake, atakapo wakati wo wote, Sultani Darai nimwoze mwanangu, sitaki pishi kwake, sitaki kisaga kwake, sitaki kibaba kwake; sitaki nussu ya kibaba kwake, sitaki robo kibaba kwake, walakini aje yee mtupu, baada ya hizi asizidi kitu tena, haya alioniletea si haba, yaliobaki na yache kuko huko, bassi ndiyo maneno yangu, ukamweleza Sultani Darai.

Bassi paa akaondoka, akamwambia, Bwana, kua heri! nami niwie rathi sana mtumwa wako. Akamwambia, mimi nimetangulia kupokea rathi zako, nami nataka uniwie rathi sana, wewe paa, kwa haya naliokujibu. Akamwambia, rathi, bwana, hatta kwa mangine, nami, bwana, ni rathi, nami, bwana, ninakwenda zangu hatta mjini kwetu, hatutakaa siku nyingi, labuda siku nane, ao siku edashara, tutakuwa tutawasili wageni wenu. Akamwambia, Ah! kua heri.

Na yule bwana wake paa katika ule mji watu wanamzomea, na watu wanamcheka, na baathi ya watu wanamguna, na baathi ya watu wangine wanamsema, amba huyu maskini ana wazimu zayidi sasa, alikuwa na themuni yake, akaenda akanunua paa, na yule paa akamwachia, sasa anazunguka na mji, na kilio, maskini paa wangu ee, maskini paa wangu. Na watu nukumcheka, naye akili zake zimepotea kwa sababu ya paa yule.

[ 74 ]Hatta siku ile akaondoka, akaenda kwake, kadiri ya kukaa kitako, paa akatokea. Akiondoka kitandani mbio yule maskini, akaenda akamkumbatia na kulia. Paa akamwambia, nyamaa bwana, silie, nikupe habari nilizo nazo. Ah! paa wangu siku nyingi umepotea, mimi huku nyuma nikalia, nikasikitika, nathania umekufa. Akamwambia, Ah! bwana, mzima mimi, bassi kaa kitako, bwana, nikueleze nalio nayo.

Bwana wake akakaa kitako, akamwambia, haya nieleze. Akamwambia, Bwana ntakueleza mambo, nawe sharti uyaweze. Akamwambia, jambo lo lote utakaloniambia, kwa sababu roho yangu inavyokupenda, ntayaweza utakaponiambia, bwana lale chani, nikupindulie jabali, nami nitalala. Akamwambia, bwana nimeona vyakula vingi, vyakula vya kushiba, vingine vya kuviacha baki, lakini vyakula hivyo vyakula vitamu sana, bwana.

Akamwambia, katika ulimwengu kuna mema matupu? Shuti mema na maovu, ndio ulimwengu, na vyakula ni tamu na uchungu, ndio vyakula vema, viwapo vyakula vitamu tupu, hivyo haviwi vyakula vya sumu?

Akamwambia, bassi sasa tukalale, hatta ussubui nitakapokwenda unifuate. Wakalala, hatta ussubui walipopambauka wakitoka yeye na paa wake, wakaingia katika mwitu. Wakaenda siku ya kwanza, wakaenda siku ya pili, katika mwitu, hatta yalipokuwa siku ya tano katika mwitu, paa akamwambia bwana wake, kaa kitako, napo karibu na mto. Akamtwaa bwana wake, akampiga sana, hatta bwana wake akapiga kelele, Nimetubu, bwana wangu.

Akimwacha pale, akamwambia, usiondoke hapa, mimi [ 76 ]ninakwenda zangu, nije nikukute papa hapa. Paa akatoka mbio hatta jua lalipopata mafungulia ya ng'ombe makuu, ametokea ile nyumba ya Sultani. Marra asikari waliowekwa katika njia kumngojea Sultani Darai atakapokuja, alikwenda asikari mbio, akamwambia Sultani, Sultani Darai anakuja, nimemwona paa anakuja mbio.

Sultani akatoka na watu wake kwenda kumlaki kule katika njia. Alipokwenda hatta alipokoma nussu ya njia, wakakutana na paa. Paa akamwambia, Sabalkheiri, bwana. Akamwambia, marahaba paa, hujambo. Akamwambia, bwana, sasa si niulize neno, siwezi kuvuta hatua hapa na hapa.

Sultani akanena, gissi gani paa? Akamwambia, Nimekuja na Sultani Darai, na katika njiani, nimetoka mimi naye peke yetu, hakufuatana na mtu yo yote, zayidi yangu mimi. Tukaja hatta katika mwitu, tukakutana na haramia, wakamkamata bwana wangu, wakamfunga, akapigwa na haramia sana, wakamnyang'anya na vyombo vyake alivyokuwa navyo vyote, hatta kitambi cha kuvaa chini wamemvua. Bassi hapo alipo bwana kama siku aliozaliwa na mamaye.

Sultani akatoka mbio na waaskari, wakaenda mbio tena hatta nyumbani kwake. Akamwita mtunga frasi, akamwambia, Tandika frasi katika banda, alio mwema katika frasi wangu, na matandiko yale yalio mema ninaopandia mwenyewe. Akamwita mjakazi wake—Henzerani! Akamwitika, Labeka, bwana. Akamwambia, fungua kasha kubwa la njumu, toa bahasha moja ya nguo. Akaenda akifungua, akaleta bahasha ya nguo. Sultani akifungua, akatoa joho moja nyeusi ilio njema sana, akatoa [ 78 ]na kanzu moja ya daria ilio njema sana, akatoa na kikoi kimoja cha albunseyidi kilicho chema sana, akatoa na kitambi kimoja kariyati kilicho chema sana, akatoa na shatoruma ilio njema sana. Akaenda kuleta kitara kimoja kilicho chema sana cha thahabu. Akaenda akaleta jambia moja la temsi la thahabu lilio jema sana. Akaleta na jozi moja ya viatu, akapewa na bakora moja la mtobwi lilio jema sana.

Akamwambia paa, Chukua vitu hivi na waaskari hawa hatta kwa Sultani, mpe, apate kuja zake. Akamwambia, Ah! bwana, itayamkini kuchukua askari hawa, mimi kwenda kufazehi bwana wangu, na hapo alipo ni kama alivyozaliwa na mamaye? Mimi pekeyangu natosha, bwana.

Akamwambia, Utatoshaje wee pekeyako, na huyu ni frasi, na nguo hizi? Amwambia, Bwana huyu frasi nifungeni hapa shingoni pangu, na hizi nguo zifungeni juu ya mgongo wa frasi, mzifunge sana, kwani mimi nitakwenda mbio na frasi. Sultani akamwambia, Kama waweza nitakufanyia. Akamwambia, Bwana, kama siwezi singekwambia, hatta hakwambia naliweza.

Akafungia frasi shingoni pake, zikafungwa na nguo juu ya mgongo wa frasi. Akamwambia, Ah! bwana, kua heri, naenda zangu. Sultani akamwambia, Je! paa, tukungoje lini? Akamwambia, mshuko wa alasiri kasiri. Akamwambia, Inshallah.

Paa akatoka mbio na frasi wake, paa mbele, frasi nyuma. Wale watu waliomo mji ule, na Sultani, na maamiri, na mawaziri, na maakida, na makathi, na jamii wangwana walio nao matajiri katika mji, wakataajabu paa [ 80 ]yule kujua kunena na kuweza kusarifu maneno kwa uzuri. Hatta akachukua frasi yule. Akaamini roho yake yule paa. Frasi ni mkuu kuliko paa, frasi na yule paa, akiinama yule frasi akimtazama paa, huona kama sisi tunavyoona chungu chini, naye frasi ndivyo amwonavyo paa chini yake. Lakini hatutambui busara ya paa yule.

Sultani akanena, Hee! paa yule ametoka katika mkono wa mngwana, katika miango ya Sultani, ametoka katika macho ya watu wenyi nguvu, ndio maana ya paa yule. Akawa mtu bora yeye kwa Sultani huyu.

Bassi akaenda yule paa hatta akafika kwa bwana wake pale alipo, alipomwambia, hapa usiondoke, naye akamkuta palepale, hakuondoka.

Yule bwana aliposikia shindo alipotupa macho nyuma, aona paa na frasi, akacheka sana, hatta paa akifika, akamwambia bwana wake, Hodi! hódi! Akamwambia, Hodi! bwana wangu. Akamwambia, karibu mfathili wangu, karibu msemaji wangu, karibu takarima wangu. Akamwambia, Nimekaa bwana wangu, nimekaa seyedi yangu. Akamwambia, nimekuletea vyakula hivi vitamu. Akamwambia, nivipendavyo vyakula hivi, kwani vyakula vikiwa vitamu vitupu vyakula huwa sumu.

Akamwambia, uondoke bwana, uoge. Akaingia katika mto bwana wake. Akamwambia hapa mtoni maji haba, ingia pale ziwani. Akamwambia, pale ziwani mbona unaogopa, pana maji ungi ungi tele, na pahali panapokuwa na maji ungi tele, panapo ziwa, hapakosi nyama walio adui.

Akamwambia, nyama gani, bwana? Akamwambia, kwanza, katika maziwa hamkosi chatu, na wa pili, [ 82 ]hakosi kenge, na wa tatu hamkosi nyoka, na la nne akali ya kitu ni vyura, nao huuma watu, nami hivi vyote naviogopa. Bassi bwana, koga papa hapa mtoni.

Bwana wake akiingia katika mto, akaoga. Akamwambia, jisugue sana na udongo. Akamwambia, utwae mchanga, uyasugue meno yako sana kwa mchanga, kwani meno yako yana ukoga. Akajisugua kwa udongo sana, akasugua meno kwa mchanga sana. Akamwambia, haya bassi, toka, jua limekuchwa, twende zetu.

Akileta pale zile nguo, akamwambia, Fungua, bwana. Akafungua zile nguo, akavaa. Akavaa kikoi seyediya, akavaa na kanzu doria, akajifunga na jambia la temsi la thahabu, akavaa na joho yake nyeusi, ilio njema sana, akajipiga kilemba kariyati, kitambi kilicho chema sana. Akavaa na viatu, akitia kitara kwapani, akashika bakora mkononi ya mtobwe.

Akamwambia, Bwana! Akamwambia, Lebeka mwanangu, lebeka mfathili wangu, lebeka mzishi wangu, lebeka msemaji wangu, lebeka nuru yangu. Akamwambia, huko tunakokwenda usitoke na neno, liwa lo lote katika kinwa chako, zayidi ya kuamkiana na kutakana habari, usizidi neno tena, maneno yote niache mimi, huna lako neno kutia. Akamwambia, Vema. Akamwambia, Huko mimi mimekuposea mke, na mahari, na nguo, na mikaja, na vilemba, na ubeleko, na jamii za ada za mke na za mamaye, na za babaye pia nimewapa. Akamwambia, mimi sitanena kitu. Akamwambia, bass, panda fras, twende zetu.

Paa akaenda mbio, akasimama mbali, akamwambia, bwana, bwana! Akamwambia, labeka. Akamwambia, [ 84 ]mke, nguo, mgomba na kulimiwa, ndiwo wapo mnono. Akamwambia, bwana wangu, wewe kuko uliko mbali, walipopanda frasi huyo ulivyovaa na kisua hicho, mtu hakujui kama walikuwa jana ukipekua, licha ya huku ugenini twendako tutakaporegea katika inchi yetu tulipotoka, hutaambiwa ndiye maskini aliopekua jaani, watu hatasadiki gissi ulivyokuwa mzuri, gissi ulivyotakata uso. Akamwambia, akali ya neno, na akali ya jawabu, hatta meno yako leo yalivyokuwa meupe, mtu haneni ila mwezi arobatashara ndio mwezi mwenyi wanga. Akamwambia, hiiyote ni takarimu yako walio nikerimu.

Bassi wakaenda zao. Wakaenda—a—a, hatta alipotupa macho yule paa, akaiona ile nyumba ya Sultani. Akamwambia, Bwana wayona nyumba ile? Akamwambia, nimeyona. Akamwambia, bassi ndio nyumba tunaoikwenda, bassi wewe tena huku si maskini, nawe jina lako walijua? Akamwambia, nalijua. Jina lako nani? Akamwambia, nimekwitwa Hamdani. Akamwambia, sili jina lako hilo. Je! baba, jina langu nani? Akamwambia, jina lako Sultani Darai. Akamwambia, vema.

Marra wakawaona asikari wanakuja mbio, na waasikari wangine wakaenda mbio, kwenda kumwambia Sultani. Wakawasili pale waaskari arobatashara, hatta wakienda kidogo, wamwona Sultani, na mawaziri, na maamiri, na makathi, na matajiri yalionao katika mji wanakuja.

Paa akamwambia, Shuka juu ya frasi, bwana, mkwewe anakuja kukulaki, na mkwewe ni yule alio katinakati, yule mwenyi kuvaa joho ya samawi. Akamwambia, vema. Akashuka juu ya frasi, wakaitwa waaskari, wakapokea frasi.

[ 86 ]Wakaenda hatta wakakutana, Sultani Darai na mkwewe, wapana mikono, killa mtu akambusu mwenziwe sana, wakafuatana hatta nyumbani.

Walipokwenda hatta nyumbani, akawaambia yule kijana, mtengeni mbali chumba, asichomwona mtu. Kwani mchumbawe amekuja. Sultani pale akaamru chakula, wakaja wakala, wakazumgumza sana, hatta walipokoma wakati wa usiku, akatiwa ndani Sultani Darai, yeye na paa wake, na waaskari watatu kumngojea mwangoni hatta siku ukacha.

Walipokucha usiku paa akaenda, akamwambia Sultani, akamwambia, bwana kazi hii mtu ajiayo ndio atendayo, bassi bwana, twataka utuoze mke wetu, kwani Sultani Darai roho yake na inamkumutika. Akamwambia, tayari mke, kamwiteni mwalimu waje. Akaenda akaita mwalimu akaja. Haya twataka umwoze bwana huyu. Ee wala, tayari. Akitwaa akimwoza. Sultani akaamru kupiga mizinga, ikapigwa mizinga sana. Sultani akaamru kupiga ngoma, killa taifa ipige ngoma yake. Bassi Sultani Darai akaingia nyumbani.

Hatta muda siku ya pili, paa akamwambia bwana wake, mimi ninatoka nasafiri, muda wa siku saba nitarudi, na nisiporudi muda wa siku saba usitoke ndani illa nije. Akamwambia, vema, inshallah. Akamwambia, kua heri sana bwana.

Akaenda akamwaga yule Sultani mwenyi inchi, akamwambia, Bwana. Akamwambia, lebeka, paa. Akamwambia, Sultani Darai amenituma kwenda mjini kwake, kwenda kutengeneza nyumba. Ameniambia, muda wa [ 88 ]siku saba nirudi, kama sikurudi muda wa siku saba, hatatoka ndani illa nije. Akamwambia, vema, kua heri.

Sultani akamwambia, hutaki watu wakufuate. Akamwambia, mimi nalitumwa kwetu na wingi wa mali, nikaingia katika nyika na katika nyika hamna jambo jema, killa jambo baya asili yake yatoka na nyikani, nami nalikuja hapa pekeyangu nisiogope, sembuse leo nisipochukua kitu nitaogopa mimi? Kua heri bwana, naenda zangu.

Akaenda—a—a katika msitu na nyika hatta akawasili katika mji. Mji ule mkubwa, una majumba mazuri. Akaona ule mji umejiinama, akasangaa, asiweze kwenda, wala asiweze kurudi, akanama, akafikiri, akawaza, akatazama, hakutanabahi jawabu, illa kuingia katika mji. Akaingia. Akafuata njia mkubwa, hatta mwisho wa njia kubwa, kuna nyumba kuu, nyumba mzuri mno isiyokuwa na kifani katika ule mji. Akaiona nyumba umejengwa kwa yakuti, kwa fieruzi, kwa mawe mazuri ya mármár.

Paa akasangaa, akawaza, akafikiri, alipotanabahi, akanena, hii ndio nyumba kwa bwana wangu. Nami nitapiga moyo konde, nende niwatazame watu walio katika nyumba hii, ina mtu ao haina mtu. Kwani nimeanza kuingia katika mji, tokea mwanzo wa mji hatta nimefika hapa kati ya mji, sikupata kumwona mtu awe yote katika mji huu, sikumwona mume, wala mke, wala mzee, wala kijana, hatta nimewasili hapa. Bassi na nyumba hii ntapiga moyo konde niingie. Akanena, kama kufa nitakufa, kama kupona nitapona, kwani mimi hapa sasa nilipo sina hila kwani nitokako mbali, bassi kama kitakachojaliwa kuniua na kiniue.

[ 90 ]Akapiga mwango konde, akapiga hodi! Akapiga tena, hodi! asipate mtu ndani wa kumjibu. Ah! nyumba hii haina mtu. Mbona mwango haukufungwa kwa 'nje? Labuda wenyewe wamelala, ao labuda wenyewe wako mbali, hawanisikii. Lakini sasa nitapiga hodi sana, wakiwa mbali wanisikie, na kama wamelala waamke.

Akapiga ho-o-o-di! ho-o-o-o-di! Akaitika huko ndani mzee, hodi! Akamwuliza, nani wewe unayopiga hodi? Akamwambia, mimi, bibi mkubwa, mjukuu wako. Akamwambia, kama ni mjukuu wangu, baba, rudi kuko ulikotoka, usije ukafa hapa, ukanijongea na mimi kufa.

Akamwambia, bibi, fungua, nna maneno yangu matatu nataka kukwambia. Akamwambia, mjukuu wangu, sikatai kufungua, nachelea kuponza roho yako, yaponza na yangu. Akamwambia, bibi roho yangu haitakwenda, wala yako haitakwenda, wallakini, bibi mkubwa, tafáthali fungua, nikwambie maneno yangu matatu.

Akafungua mwango yule kizee. Akamwambia, nashika moo, bibi. Akamwambia, marahaba, mjukuu wangu, akamwambia, Je! habari utokako, mjukuu wangu. Akamwambia, bibi mkubwa, nitokako kwema na hapa nijapo pema. Akamwambia, Ah! mwanangu, hapa ndio si pema kabisa, kama wewe watafuta njia ya kufa, wala kama hujaona kufa, bassi leo ndio siku ya kuona kufa, ndio siku ya kujua kufa.

Akamwambia, bibi mkubwa, nzi kufia tuini, si hasara. Akamwambia, yatakapokuwa hayo, mwanangu, mimi nakuonea hasara, kwani wamekufa watu wengi, wana na [ 92 ]panga na ngao. Akamwambia, mama, hayo yamepita, tazama na yangu. Akamwambia, baba, kuwa hawakuwa wenyi miguu miwili, utakuja kuwa wewe, mwenyi miguu minne. Akamwambia, mama, masifiwa sikuona sifa, nda kujionea.

Akamwambia, napenda mtoto, urudi ulikotoka. Akamwambia, si jambo la kupatikana, mama, pale, nalikokwambia niregee nyuma tena. Walinambia nini kwanza? Akamwambia, sikuambia, nzi kufia tuini si hasara? Akamwambia, kweli umeniambia, nami, mwanangu, simekujibu? Akamwambia, walinijibu nini mama? Akamwambia, sikukwambia, nakuonea hasara? Akamwambia, hasara yako mbona sipendelei sana. Akamwambia, mimi sina buddi kukuuliza pindi usiniambie, lakini ntakuuliza, mwenyi nyumba hii nani?

Akamwambia, Oh!—baba wee, nyumba hii ina wingi wa mali, ina wingi wa watu waliomo, ina na wingi wa zakula ziliomo, ina na wingi wa frasi waliomo, bassi na mwenyewe mji huu wote ni nyoka mkuu mno wa ajabu.

Ehée! mzee, nipe busara nipate nyoka huyu, hatta nimpate nimwue. Akamwambia, Oh! mwanangu, maneno haya usinene, utanichongea, tena kuko aliko yeye mwenyewe alisikia tena, nimewekwa mimi pekeyangu hapa, mimi mzee, kazi yangu ya kupika zakula; wayaona masufuria yale, bassi anapokuja yule joka hapa, kuvuma baridi na vumbi kuruka kama methili ya tufani inapokuja. Bassi akija, hufikia pale uwanjani, akala hatta akashiba, akaingia hapa ndani kunywa maji. Akiisha kunywa maji, [ 94 ]huenda zake, haji illa kwa siku ya pili, wakati uleule jua vitwani. Bassi uta'mweza api, baba, nyoka huyu? Naye ana vitwa saba, hawaku'mweza kindakindaki wafalme wa nyuki, uta'mweza wewe baba?

Akamwambia, mama, ona ulicho nacho usione usichokuwa nacho. Huyu nyoka hana upanga? Akamwambia, ana upanga, tena mzuri, tena mwema, tena upanga huu ni wa radi. Akamwambia nipe, mama. Akaenda hatta changoni, akiwangua, akija akimpa. Akamwambia, ndiwo huu mama? Akamwambia, ndio huu, mwanangu. Akamwambia, tena upesi, anakuja tena wakati huu, wewe umekuja kujiua wewe, uje uniue na mimi. Akamwambia, kwa nini, mama? Akamwambia, si nnakwambia, huta'mweza. Akamwambia, Kama kufa, tumekwisha kufa, tumesalia kuoza, nawe mama piga moyo konde, nami nijaribu leo, kama hawa wakiwa kindakindaki wafaume wa nyuki, hawaku'mweza nyoka huyu, bassi mimi leo nita'mweza. Akamwambia, Ah! mwanangu.

Marra asikia tufani inavuma. Yule mzee akamwambia, wamsikia mwanamume anakuja? Akamwambia, nami nilio ndani mwanamume, mafahali mawili hayakai zizi moja, atakaa yeye nyumba hii, ao nitakaa mimi. Yule kizee akacheka sana kwa maneno anaotoa yule paa. Yule mzee akaona nafsi yake amekufa, kwani yule kizee, aliwaona watu wanao nguvu marra elfu kuliko huyu paa, nao hawaku'mweza nyoka huyu, aliwashinda. Akamwambia, mama, ache haya, matunda si mazu, mazu ni mwekundu. Bassi saburi, mama.

Marra mbeja wa kani akiwasili nyumbani alikowasili, [ 96 ]akaingia katika sufuria zake kula, hatta alipokwisha kula, akaja hatta akafika pale mlangoni. Akasikia harufu ya kitu chingine kiwamo ndani. Akamwita, wee kizee, mbona leo nasikia harufu nyingine, humo ndani? Akamwambia, bwana, mimi hapa pekeyangu, nimekaa siku nyingi, sikupata kujisinga, leo nimejisinga, bassi ndio unaposikia harufu hii, unanena ndio kuna kitu kingine ndani. Kitatoka wapi kitu hapa, Bwana?

Na yule paa ameutoa upanga amekaa tayari. Yule nyoka akitia kitwa ndani, paa upanga umemtoka, akamkata kitwa, yule nyoka asijue kama amekatwa kitwa. Akipenyeza cha pili, yule paa umemtoka upanga, akamkata kitwa cha pili. Yule nyoka akainua kitwa akamwambia, umekuja nani katika nyumba yangu kunikunakuna? Akikitia kitwa cha tatu kutaka kuingia ndani, paa umemtoka upanga, akimkata kitwa cha tatu.

Hatta alipotimiza vitwa sita, ghathabu za nyoka, akajiacha mapindi, yeye paa na yule kizee wasionane kwa vumbi. Hatta alipotia kitwa cha saba, alipokitia mwangoni, paa akamwambia, Leo ndio mauti yako, akamwambia, miti pia umepanda huu ndio mparamuzi. Akainua kitwa kuingia nyoka ndani, paa upanga umemtoka, akamkata kitwa cha saba. Paa akianguka akizimia.

Bibi yule kizee, akapiga kigelegele, akapiga na hoihoi, akajiona mwili wake na macho yake, na roho yake, na nguvu zake ni kama mtoto wa miaka tissa, naye ni mtu wa miaka khamsi u sabwini. Akaondoka mbio yule kizee, akamchukua yule paa, na yule paa amezimia, akamtia maji, na kumpepea, na ku'mweka pahali palipokabili baridi, hatta paa akatweta, hatta paa akaenda [ 98 ]chafya, chééé. Mzee yule akafurahi sana, akamwona yule paa akienda chafya. Akampepea sana, akamtia maji sana, na kumgeuzageuza, hatta paa akaondoka.

Yule bibi akasema, ah! mjukuu wangu wee, pole mwanangu, wala sikukuthania kama uta'mweza huyu. Akamwambia, mama, nalitangulia kukwambia, masifiwa sikuona shani, nda kujionea. Akamwambia, kweli, mwanangu, akamwambia, kwani nimeona.

Akamwambia, njema unipe habari. Akamwambia, kama ipi, mwanangu? Akamwambia, hapana pingamizi tena mbele yetu? Akamwambia, mbele kweu na nyuma kweu, sijui ya Muungu. Bassi nataka unionya nyumba hii, mwanzo hatta mwisho, chini hatta juu, ndani hatta nje. Akamwambia, Ee walla, baba. Akamwambia, kwanza na tupite uani. Akamwambia, nitakupitisha, baba, kwenda kukuonya cha siri na cha thahiri zalizowekwa. Akamwambia, vema, mama yangu, zema haziozi. Akamwambia, kweli, mwanangu.

Bassi tena akamwonya ghala za mali, akamwonya na vyumba, vilivyotiwa vyakula vya mali. Akamwonya na vyumba vilivyotiwa watu wazuri, waliofungwa tokea zamani. Akampandisha hatta orofani, akamwonya kama kilichomo kinenacho na kisichonena. Hizi, bwana, mali zako. Akamwambia, Mali haya yaweke wewe, hatta mimi hamwite bwana wangu, ndiye mwenyi mali haya.

Yule paa akafurahi sana. Ile nyumba imempendeza sana, na atakapokuja yeye na mkwewe, na mkewe, na jamii ya watu watakaofuatana nao, killa atakaokuja, akiona nyumba hii, atanena hii ndio nyumba, bassi, kwani kule mji wao hakuna nyumba yapatao nusu ya ile. Ah! bassi, paa [ 100 ]akanena, bwana wangu atafurahiwa kwa hayo naliyomtendea, kwani bwana wangu akiwa na nyumba hii, naye mtu aliyekuwa mbali, atakuwa kama aliozaliwa marra ya pili, ginsi atakavyojiona mzuri.

Akakaa nyumbani akizumgumza na kizee yule, hatta baada ya siku ya tatu, akaenda zake.

Akaenda hatta akawasili katika ule mji, alioko bwana wake. Sultani aliposikia yule paa amekuja, alifurahi sana, akaona kama mtu alioshushiwa jaha. Hatta alipopata habari bwana wake ndani aliko, akaona nafsi yake kama mtu alioyona leilat al kadri. Bassi akaondoka aka'mbusu sana. Baba yangu, umekawia, umeniacha sikitiko, nimekaa kukumbuka, siwezi kula, siwezi kunywa, siwezi kucheka, moyo wangu haukuona tabassamu kwa jawabu liwe lote, na sababu kukumbuka wewe.

Akamwambia, mimi mzima, na nitokako kwema, nami napenda baada ya siku nne, kutukua mkewo, twende zetu kwetu. Akamwambia, Ni ihtiari yako, ni lile unambialo ndilo nitafuata. Bassi, akamwambia, mimi nnakwenda kwa mkwewo, hamkhubiri habari hizi. Akamwambia, Enenda.

Akaenda hatta barazani, akamwambia, Bwana nimekuja kwako. Akamwambia, Bashiri kheiri, nambie uliyojia. Akamwambia, Nimekuja, nimetumwa na bwana kuja kukwambia, baada ya siku nne, atakwenda zake, yeye na mkewe, nawe nimekupasha habari. Akamwambia, mimi sipendi kuondoka upesi, kwani hatujakaa sana, mimi na Sultani Darai, wala hatujazumgumza sana, mimi naye, tokea alipokuja hatta leo siku arobatashara, hatujapata kukaa mimi naye tukazumgumza, wala hatujapata kupanda [ 102 ]frasi mimi naye tukatembea, wala hatujapata kutanganya mimi naye tukala, na kuondoka naona hasara. Akamwambia, Bwana huna buddi kwani yeye anataka upesi kwenda kwao, baada yeye ameniambia, kama yeye amekaa siku nyingi. Akamwambia, Vema. Akaenda zake, akamjibu bwana wake. Akamwambia, nimemwambia mkwewo mashauri yako, amerithika. Akamwambia, Bassi amruni waambie jamii ya watu, kama muda ya siku nne Sultani mwanawe anakwenda kwa mumewe, nanyi 'mwe na habari.

Sultani akawaambia watu walio katika mji, wake kwa waume, siku ya kwenda mwanangu, na waanawake wa kiungwana wamfuate. Akatoa na watu, akawaambia, ninyi kaeni mkimtazama mwanangu katika njia.

Hatta muda ilipokoma siku ya nne wakatoka wangwana wote waanawake walio bora, na watumwa wao, na frasi zao, wakaingia katika kundi kumpeleka mwana wa Sultani kwa mumewe, Sultani Darai. Wakatokea, wakaingia katika njia, wakaenda hatta lilipokoma jua vitwani, wakapumzika. Paa akaamru kufanyiza vyakula vema, wakala tokea wangwana hatta watumwa, wakashiba sana na roho zao zikafurahi kwa zakula kuwa zema.

Wakaenda hatta ilipokoma saa kumi na moja. Akawaambia, wangwana hapa na tukae, mahali pa kulala. Vikafanyizwa vyakula vema na wali mzuri, wakala wangwana hatta watumwa. Wakafurahi wangwana hatta watumwa wakalala pahali pale. Bassi usiku alianza tokea pembe hatta pembe, tokea mwanzo hatta mwisho, kwa wangwana na watumwa, hatta kwa nyama zalizopandwa, pasiwe mtu mmoja alioikosa heshima yake, tokea watumwa hatta wangwana, hatta nyama zao walizopanda, na wote walifurahi kwani yeye apenda sana kumfurahisha bwana wake. Akamwita, Baba! akamwambia, naona umechoka [ 104 ]sana, tokea lalikwanza kutoka jua, hatta kuchwa kwake hukupata kupumzika hatta marra moja, hatta huu usiku. Akamwambia, tafathali nawe lala. Nawe usikasirike, baba, mkuu ni jaa, mtukuzi ni atukuaye, asiotukua si mtukuzi. Akamwambia, kweli. Wakalala.

Hatta ussubui kabla hakujapambauka vema, akaamsha wangwana. Wangwana, Wangwana, amkeni. Wajoli, Wajoli, Wajoli, amkeni. Wangwana naweni uso, na wajoli wangu naweni uso.

Akawaambia, njooni wangwana mfungue kinywa, na wajoli, wajoli, njooni mfungue kinywa, tupate kimbia jua. Wakaondoka wale wangwana wakala vyakula vema, wakafurahi, roho zao hatta watumwa. Na wote waliopo, watumwa kwa wangwana wakampenda yule paa kuliko Sultani Darai.

Wakiisha, wakaondoka. Je! Wangwana mmeshiba? Wakamwambia, tumeshiba. Wakamwambia, sisi ni wangwana, hatta kama hatukula chakula hichi, kwa heshima zako na kwa mambo yako sisi pekeyetu hushiba. Akamwambia, ahsánt. Akauliza, Je! jamaa zangu mmeshiba? Wakamwambia, Hapo tulipo sisi hatta ukope twaonea mzito kutia tumboni mwetu, kwa ginsi tulivyoshiba.

Akamwambia, Haya tusafiri sasa. Wakaenda hatta lalipokoma jua vitwani, wakatua. Na tupumzike hapa tunywe maji, tule chakula. Bassi kikaja chakula, wakala, wangwana kwa watumwa, wakashiba, wangwana kwa watumwa, wakafurahi, wangwana kwa watumwa.

[ 106 ]Wangwana wale wakampenda yule paa mapenzi yalio bora yasiokuwa na kifani. Na wale watumwa wao walimwona yule paa kamma mboni zao za macho, gissi wanavyompenda kwa ginsi walivyomwona tamu.

Akawauliza, wangwana mmeshiba? Wakamwambia, hapa tulipo hatta pumuzi twajiona kuwa ndogo nasi. Akawauliza, ewe wajoli wangu, wake kwa waume, anao njaa asinifiche. Wakamwambia, sisi hatuna njaa. Akawaambia, Haya wangwana, twendezetuni. Wakaondoka, wakaenda hatta yalipokoma saa edashara, akawaambia, wangwana hakuna mwendo wa usiku. Akawaambia, na tukae. Wakakaa kitako. Kikaletwa chakula, wakala, wangwana na watumwa, wakashiba, wangwana na watumwa, wakafurahi, wangwana kwa watumwa, kwa zile heshima walizozipata kwa paa, wakamwona yeye bora angawa paa, wakamwona zayidi kuliko bwana wake Sultani Darai. Akaanza toka mwanzo hatta mwisho, mngwana kwa mahali pake, na mtumwa kwa pahali pake, na mkubwa kwa pahali pake, na mdogo kwa pahali pake. Bassi akarudi, akaja akalala hatta jogoo la kwanza lalipowika. Akaondoka, akamwambia bwana wake. Akamwambia, Bwana! Akamwambia, Labeka baba, akaitika, labeka, azizi wangu, labeka mvika nguo yangu, nambie ulilo nalo, baba. Akamwambia, Hapo tulipo na nyumba tunaokwenda nnavyoaza, napenda nafsi yangu tuondoke na mapema hapa. Akamwambia, Vema. Bassi mimi nitaamshe wangwana wafungue kinywa na mapema, tupate kwenda zetu. Akamwambia, halitupata athuuri tutauona mji. Akamwambia, Vema.

Akawaamsha, Wangwana! Wangwana! Wakamwitika, labeka. Akawaambia, Ondokeni na nawe uso. [ 108 ]Wakaondoka. Akawaambia, Wajoli! Wajoli! Wakamwitika, Labeka baba. Ondokeni, nawe uso. Wakamwambia, tumeondoka, baba. Waandikiwa chakula, wangwana kwa watumwa, wakubwa kwa wadogo. Haya, wangwana, fungueni kinywa. Akaenda akawaambia, haya wajoli, fungueni kinywa. Watu wakala hatta wakashiba. Walipokwisha kula hakujapambauka bado. Haya, wangwana, twendezetuni.

Wakaondoka wakaenda zao. Wakaenda hatta alipokoma jua vitwani paa akaona, na wale wangwana waliofuatana nao wakaona dalili ya jumba mbele yao. Wakamwita, Paa! Akaitika, Labeka, bibi zangu. Wakamwambia, mbele yetu twaona kama dalili ya nyumba. Akawaambia, Oh! bibi, bassi huu, si huu mji wetu? Ndio nyumba ya Sultani Darai.

Waanaake wakafurahi sana, na wale watumwa wakafurahi sana. Wakaenda hatta yalipokoma muda wa saa mbili, wakawasili katika mwango wa mji.

Akawaambia paa, Wangwana kaeni hapa, wangwana kwa watumwa, wake kwa waume, niacheni mimi na Sultani Darai twende nyumbani. Wakamwambia, Vema. Akaondoka paa na bwana wake, hatta wakiwasili katika nyumba.

Yule kizee aliyo katika nyumba alipomwona paa, anakuja, aliruka na kigelegele na hoihoi, na kuranda, na kwenda mbio hatta akawasili katika miguu ya paa. Akimchukua, aki'mbusu. Paa akamwambia mzee, Nache, wa kuchukuliwa ni huyu bwana wetu, wa kubusiwa ni huyu bwana wetu, kwani mimi nikiisha fuatana na bwana njia moja, heshima za kwanza apewe bwana, bassi ndio nikapewe mimi. Akamwambia niwie rathi, baba, sana, [ 110 ]sikumjua kama ndiye bwana wetu. Akamwambia, nawe, bwana, niwie rathi sana, mtumwa wako, sina habari kama wewe ndio bwana wetu. Akamwambia, ni rathi.

Akaondoka pale, ukifunguliwa mwango, tokea chini hatta juu, na vyumba vyote, na ghala zote, ya mini wa shemali. Akaingia yule kijana, akawaambia, wafungueni hawa watu waliofungwa. Wangine na wafagie, wangine watandike vitanda, na wangine wapike, na wangine wateke maji, na wangine watoke nje wapate kwenda kumtwaa bibi.

Yule Sultani Darai akaona nyumba ile mzuri sana, akaona, vitanda vizuri mno, akaliona pambo la nyumba, hakupata kuliona, wala hakupata kulisikia pambo kama lile. Roho yake ikafurahi sana, moyo wake ukaona, kama mtu alioletwa habari na Muungu, kama wewe umekwenda ingia peponi, kwa roho yake yalivyofurahi.

Wakaenda watu kule, wakaenda wakamchukua bibi na wale wangwana waliokuja, na wale watumwa wao waliokuja nao, na mwenyewe pambele, wakaja nao hatta wakafika nyumbani. Akawaambia, Karibuni wangwana, piteni wangwana. Akawaambia, karibuni jamaa, piteni ndani jamaa zangu. Waanawake mwende darini. Walipokwenda wangwana wakapita, akawaambia, na hawa frasi, waliokuja na wangwana, na wapelekwe uani, wakakaa.

Bassi wakaenda wakafanya vyakula vingi sana, wakafanyiziwa wali mzuri sana, wakala, wangwana kwa watumwa, kwa killa mtu, akashibia nafsi yake. Wale waanaake waliokuja, wakamwambia, Ah! paa wee, eh! baba wee, sisi tumeona majumba, sisi tumeona watu, sisi tumesikia mambo. Wallakini nyumba hii, na wewe ginsi ulivyo, hatukupata kuona wala hatukupata kusikia, na mwenyi kutaka kuona, na one nyumba kama hii, asizidi [ 112 ]nyumba kama hii. Na atakayokwambia iko nyumba zayidi kuliko hii, mtu huyo ni mwongo, na mtu atakayokwambia, yuko mtu mwenyi akili na busara, na kujua makazi ya wangwana na watumwa, na kujua, huyu mkubwa na huyu mdogo, akupitaye wewe, mtu huyo mjua kuwa mwongo. Akiwa akitokea wa kwanza huwa huyu, wa pili ni wewe. Na mtu atakaokwambia zayidi, mwambie kuwa mwongo.

Wakikaa siku nyingi katika ile nyumba, hatta wakaomba rukusa, wale waanaake, Twataka kwenda kwetu. Akawaambia, Ee, wangwana wangu, ehee, bibi zangu, ee seyidi zangu, mmekuja jana ussubui, leo jioni mtaondoka? Wakamwambia, Tumekuja siku nyingi, baba, tumemleta harrusi kwa mumewe, nasi tumefika salama, nasi twataka kurudi, tukatazame shauri ya kwetu. Akawaambia, Ee walla, bibi, Ee walla bibi zangu, Ee walla, na jamaa zangu.

Akawafanya zawadi nyingi, akawapa wale wangwana, akawapa zawadi nyingi, akawapa watumwa wa wale wangwana. Wangwana wale wakafurahi sana, na wale watumwa wakafurahi sana kwa zawadi walizopewa. Wakamwona yule paa ni bora marra elfu kuliko yeye, bwana wake, Sultani Darai. Wakatoka, wakaenda zao kwao. Akawapa na watu wakawasindikiza.

Wakakaa kitako, paa na bwana wake, katika nyumba, muhulla wa siku nyingi.

Paa akanena na bibi yule kizee, Mimi nimekuja na bwana wangu katika nyumba hii, katika mji huu, nami nimemfanyia mambo mengi bwana wangu, tena mambo mema, tena mambo ya kumwinua uso wake mbele za watu, hatta tumefika hapa, hatta leo hajaniuliza, Je! baba, je! [ 114 ]paa wangu, je! mtumwa wangu, je! kiatu changu! nyumba hii umepataje? Mji huu mwenyewe nani? Nyumba hii mwenyewe nani? Ao nyumba hii unapanga, ao nyumba hii umenunua, ao mji huu umepewa, ao mji huu hamna watu kumi hatta moja. Bassi, mama, mambo haya, mambo gani? Zema zote nnazomtenda bwana, naye hatta siku moja hajanitenda jambo jema, alijua mtu aliokuja naye hapa, nyumba hii si yake, wala inchi hii si yake, tokea alipozaliwa hatta leo hakupata kuiona nyumba kama hii, wala hakupata kuuona mji kama huu. Bassi yeye anga haniiti kwa thikaka, akaniuliza. Lakini watu wamenena, hakuna wema watu mtenda zema cha nina, na wazee walinena ukitaka kumtenda mtu vema, simtende mema matupu, mtende na mabaya, ndipo mtakapopatana wewe naye. Akamwambia, bassi mama, nimekwisha, nataka kutazama fathili nalivyomtenda bwana wangu, nami atanifathili. Akamwambia, Vema baba, wakalala.

Hatta ussubui walipokucha, paa akaugua tumbo na homa na miguu yote kumwuma. Akamwambia, mama! Akamwitika, Labeka, baba. Akamwambia, Enenda kamwambia bwana darini, paa hawezi sana. Akamwambia, vema, baba, na akiniuliza, hawezi nini, nimwambieje? Mwambia, Maungo yote yaniuma sana sina pahali pamoja pasiponiuma.

Akaenda yule mzee hatta darini. Akamkuta bibi na bwana wamekaa katika kitanda cha mawe ya marmari, na godoro ya mdarahani, na takia huku na huku, wakati hutafuna tambuu, mke na mume.

Wakamwuza, Je! kizee, umekuja taka nini? Akamwambia, kwambia bwana, yule paa hawezi. Yule [ 116 ]mwanamke akasituka, akauliza, hawezi nini? Akamwambia, mwili wote, bwana, wamwuma, hana pahali pamoja pasipomwuma.

Ah! bassi, miye nifanyeje, tazama mtama, ule wa felefele, mfanyizia uji, mpe. Yule mkewe akasangaa, amwambia, Bwana, unakwenda kumwambia kufanyiziwa paa uji mtama wa felefele, hatta frasi anaopewa hali aukataa? Eh! Bwana, si mwema wee.

Akamwambia, Oh! ondoka huko, una wazimu wali watu hutupa tu, huko kupata mtama yeye ni haba?

Akamwambia, Kama yule, bwana, si paa, ni mboni yakwe ya jicho, likiingia mchanga, utaingia na shughuli.

Ah! maneno yako mengi, mwanamke saa!

Akaenda yule mzee hatta chini. Yule mzee alipomwona paa, akasangaa, akitoka na machozi sana, akalia sana. Ah! paa!

Akamwuliza, gissi gani, mama? Nimekutuma na kurudi na kulia tu, hunijibu naliokutuma? Likiwa jema, nijibu, na likiwa baya, nijibu, kwani hii ndio hali ya ulimwengu wakimtenda vema mtu atakutenda mabaya. Bassi sikutendwa mimi tu, wametangulia na watu zamani wakatendwa kama haya. Akamwambia, bassi nambie.

Akamwambia, kinwa kimejaa mate, na ulimi wangu umejaa kinwani, siwezi kukwambia kama hayo nalioambiwa, wala siwezi kukutendea kama haya nalioagizwa.

Akamwambia, Mama wewe waliloagizwa na waliloambiwa kunitendea, nitendee, na uliloagizwa kunambia, nambie. Wala usiogope kwambia, wala si tahayari kuniambia, kwani haya hukuniambia wewe, alionambia mwenyewe namjua, nieleze mama.

[ 118 ]Akamwambia, nimekwenda hatta darini nnamkuta bibi na bwana, wamekaa kitako katika kitanda cha mawe ya marmari, na godoro kitambaa cha mdarahani, na takia huku na huku, wanatafuna tambuu, mke na mume. Akaondoka bwana, akaniambia, umekuja taka nini, kizee? Nikamwambia, nimetumwa na mtumwa wako paa, kuja kukwambia kama hawezi. Yule mkewe akaruka, akaisha akasangaa, akaniuliza, hawezi nini paa? Hamwambia, maongo yote yameuma, hana pahali pamoja pasipomwuma. Akaniambia bwana, Katwae ule mtama wa felefele, mfanye uji mpe. Bibi akanena, Eh! bwana, paa ndio mboni yako wa macho, wewe huna mtoto, humfanya paa kama mwanao, wewe huna karani, humfanya paa ndio kama karani wako, wewe huwezi kusimamia, humfanya paa kama msimamizi wako, bassi bwana kumi kwako hatta moja halipatikani lilio jema kwako, paa huyu, bwana, si wa kutendwa mabaya, huyu ni paa umbo, si paa kwa moyo, moyo wake na mambo yake ampita mngwana, alio yee yote, bora.

Akamwambia, Wewe mpuzi, maneno yako mengi, thamani yake mimi namjua yule, nimemnunua kwa thamani ya themuni, bassi mimi nina hasara gani?

Akamwambia, Bwana sitazame hayo yaliopita, tazama haya yalio usoni pako. Huyu si paa wa thamani ya themuni, wala lakki, huyu neno lake na tasfida yake anapotuliza ulimi wake kunena na akili yake, yapita lakki mbili.

Eh! maneno yako mengi, mwanamke saa, hupunguzi?

Yule mzee akamjibu paa, Nikaambiwa na bwana, utwaliwe mtama wa felefele, ufanywe uji unywe.

[ 120 ]Paa akanena, Ha! mimi ndio kufanyiwa uji huyo, akakwambia yeye bwana?

Bassi naweza kukwambia uwongo, baba? Akaniambia mwenyewe bwana na mkewe yuko, hatta mkewe akigombana naye bwana kwani kumfanyia hivyo paa, na bibi akatukanwa kwa sababu wewe kukugombea.

Paa akanena, Wazee walinena, mtenda mema cha nina, nami nimemtenda zema, nami nimepata haya walionena wazee.

Akamwambia, Mama, enenda tena juu kwa bwana, usichoke kwa haya ninayokuagiza, ukamwambie bwana,—paa hawezi sana, na ule ulionambia mtama kumfanyizia uji, hakunywa.

Akaenda yule mzee, akamkuta bwana na bibi, wamekaa katika dirisha, wanakunywa kahawa. Alipotupa macho yule bwana nyuma yake, amwona yule kizee. Akamwambia, Una nini wee kizee? Akamwambia, Nimetumwa bwana na paa, ule mtama walioniagiza kumfanyizia uji; hakunywa, naye hawezi sana paa.

Akamwambia, Eee chúb! zuia ulimi wako, uzuie na miguu yako, ufumbe na macho yako, uzibe na masikio yako kwa nta, akikwambia paa, panda juu, mwambia miguu yangu haiwezi kupanda darajani, imekunjika. Akikwambia sikia, mwambia masikio yangu hayasikii maneno yako, yamezibwa na nta, akikwambia, nitazame, mwambia, macho yangu yametiwa vijamanda kama anavyofungwa ngamia, akikwambia njoo tunene, mwambia, ulimi wangu nimetiwa kulabu, hauwezi kunena nawe.

Yule mzee akasangaa, kwa sababu ya maneno yale kwambiwa, na sababu alipomwona paa kuja katika mji ule akaja kuuza roho kununua mali, lakini roho akapata, na mali akapata, na leo anavyomwona heshima yake hana [ 122 ]kwa bwana wake, anamwonea huruma, taabu yaliompata huyu paa, ndio mambo ya ulimwengu.

Yule mkewe Sultani, aliposikia maneno yale mumewe kumwambia mzee, akapotewa na nuru za uso, akaingiwa na imani roho yake, akatoka na machozi katika macho yake, hatta mumewe, alipomwona anatoka na machozi, na nuru za uso zimempotea, akamwuliza, una nini, binti Sultani? Akamwambia, katika ulimwengu asio mengi ana machache, na mtu wazimu wake ndio akili yake.

Kwa nini, bibi, ukanena maneno haya?

Akamwambia, nakusikitikia wewe, mume wangu, kwa haya unayomtenda paa, killa ninapokwambia neno jema kwa paa, mume wangu, hutaki wewe na akili yako tu. Nakuona huruma mume wangu, akili yako kukupoteza.

Akamwambia, Kwani ukanambia neno hilo?

Akamwambia, Shauri mbaraka tu, watu wawili katika nyumba, mke na mume, mke akipata neno, amwambie mume, na mume akipata neno, amwambie mke, kwani shauri mbaraka.

Akamwambia, mwanamke wewe una wazimu, tena wazimu wako u thahiri, tena wataka kutiwa pingu.

Akamwambia, Bwana, mimi sina wazimu, kana mimi nna wazimu, huu wazimu wangu ndio akili yangu.

Akamwambia, Ee kizee, usisikilize maneno ya huyu bibi, ukamwambie, potelea mbali. Kamwambia paa, asinifanye uthia, tena asikae huko chini akajifanye yeye ndio Sultani, mimi huku sipati usingizi wa usiku, wala wa mchana, sipati kula, wala sipati maji ya kunywa, kwa uthi wa yule paa anaokuja akiniuthi. Marra [ 124 ]amekuja mtu, paa hawezi, marra amekuja mtu, paa hataki kula, na potelea mbali, akitaka kula na ule, hakutaka, na apotelee mbali. Mama yangu amekufa, na baba yangu amekufa, nami ninakula na kunywa, sembuse yule paa mmoja, naliomnunua kwa themuni, atakuwa akinipanza na kunishusha? Nenda kamwambia paa ataadabu.

Akishuka yule mzee, huku anatoka damu, huku anatoka uzaha. Akaenda hatta akimwona paa, yule mzee akamkumbatia paa, akampakata, akamwambia, Mwanangu, mema yako walioyatenda yamepotea, yaliosalia stahamili.

Akamwambia, Mama, matumbo yangu yamejaa, na ulimi wangu mzito, na macho yamefanya kiwi, kwa haya ninayoyasikia. Wakalia sana wote wawili, paa na mzee.

Akamwambia, Mama, mimi ntakufa, kwani roho yangu umejaa ghathabu sana, imejaa na uchungu sana, na uso wangu nimetahayari kumtenda bwana wangu vema, kunilipa maovu.

Akamwambia, Ahh! mwanangu, sina la kunena.

Akamwambia, Mama, mali yaliomo katika nyumba hii mimi paa mmoja nnakula gani? Killa siku angenipikia nussu kibaba, naye hangepungukiwa na kitu bwana wangu. Nimesumbuka mimi kuchuma, mimi kuugua, kwambiwa nikatwaliwe felefele, asiokula frasi, nifanyiziwe uji mimi? Wazee walinena, mtenda mema cha nina.

Akamwambia, Enenda baada juu kamwambia bwana, paa hawezi sana, mwambia, kumwona kwetu, twamwona kufa ku karibu kuliko hayi.

Akaenda hatta darini, akamwona bwana, atafuna 'mua. [ 126 ]Akaambiwa bwana, na huku mzee analia. Akamwambia, Bwana, paa hawezi sana, twamwona kufa ku karibu kuliko kuwa mzima.

Akamwambia, nimekwambia usiniuthi.

Mkewe akamwambia, Ee bwana, hushuki ukaenda kumtazama paa wako, hushuki kumtazama kiatu chako, hushuki kumtazama mboni yako wa jicho, hushuki kwenda kumtazama karani wako, hushuki kumtazama msimamizi wako? Na kama hutaki kushuka wewe, nache mimi nikamtazame. Bassi kwako kumi hatta moja halipatikani jema.

Akamwambia, Enenda kamwambia paa, kama watu hufa marra moja, yeye na afe marra kumi na moja.

Mke akamwambia, Ah! bwana, amekutenda nini paa, amekukosa nini paa? Maneno haya hamwambii mtu illa adui yake, asiopenda kuona. Ehe, weye na paa, bwana, mna wadui gani? Bwana, mambo yako unaomtenda si mema, wala wewe kuyafanya haya, wala kumfanyizia paa. Watu wakisikia watakucheka, kwani huyu paa si mdogo, paa amependwa tokea wangwana hatta na watumwa, paa amependwa na wadogo hatta nao wakubwa, paa amependwa na wake hatta na waume. Bassi wewe bwana, kwani ukamchukia paa huyu, wala siyo maungwana. Mngwana akitendwa jema kulipa jema. Mngwana hatendwi jema akalipa maovu, sicho kiungwana. Bassi kwako mambo kumi hatta moja, halipatikani jema kwako. Kama paa huyu wewe humpendi kwa uzuri, mpende kwa kunena, kama humpendi kwa kunena, mpende kwa sababu kuwa mtu wako, unamtuma hapa na hapa, kama humpendi kwa hilo, mpende kwa sababu anavyojua heshima za watu, kama humpendi kwa hayo, mpende kwa [ 128 ]kuwa msimamizi wako katika nyumba. Tena paa yule, bwana wangu, mume wangu, Sheki langu, Eh! Sialtani Darai, mimi nalinena una akili nyingi, kumbe huna akili hatta kidogo, bwana, kumi hatta moja kwako halipatikani jema. Bwana, ukuu si pembe kama mtu ataota, ukuu shuti astahamili, na huyu mkuu ni jaa, killa mwenyi taka yake humwaga, kwani hili jaa halina mtu mmoja, halina tajiri, wala halina Sultani, wala halina Kathi, wala halina maskini, wala halina mkubwa, wala halina mdogo, wala halina mke, wala mume.

Akamwambia, wewe una wazimu mke wangu. Akamwambia, Maneno yako yote hayo, ni nguo yangu ya pili ya kujitanda.

Bassi bwana, mzee analia, haliki hatafuniki.

Akashuka mzee hatta akifika kwa paa, akamkuta paa, anatapika, akiondoka, akimdaka, akimpakata, paa na yule mzee wakalia sana.

Akaondoka yule bibi darini, akaiba maziwa, akaiba na mchele kidogo, akatwaa na mjakazi, akamwambia, twaa ukampikie paa chini mpe, akamwambia, twaa na nguo hii, ukampe ya kujifunika, na mto huu kampe, aulalie, na killa anachotaka, na anachotamani, na amtume mtu aje kwangu, asimwambie bwana wake, kwani bwana wake hatampa. Atapotaka hapa, nimpe watu wampeleke kwa baba yangu, akafanywe dawa, atatazamwa sana huko, nitampeleka.

Akashuka yule mjakazi hatta chini, akamwambia paa, Salaam sana bibi, haya si yake, ni ya bwana wako, [ 130 ]yeye apenda kutia katika macho akuweke, lakini hathubutu, hana amri mwanamke, nami nimepewa kukuletea maziwa haya, na mchele huu, na nguo ya kujifunika, na mto huu, na killa unachotaka, nambie wala usinifiche, anakwambia bibi, na kama wataka kwenda kwa babaye, atakupa watu wakupeleke, wakuchukue polepole, na huko utakwenda fanywa dawa sana utatazamwa sana, una heshima nyingi huko sana. Bassi nijibu, nikamwambie bibi.

Marra paa akafa.

Alipokwisha kufa, nyumba nzima watu wakalia, watumwa kwa wangwana, mkubwa kwa mdogo, mke kwa mume.

Akaondoka yule Sultani Darai, akawaambia, Mnalia nini, mnalia nini? Akawaambia, mnalilia paa kama naliokufa mimi. Yule aliokufa ni paa tu, thamani yake themuni.

Yule mkewe akamwambia, Bwana twalimwona paa hatta kukuona wewe. Paa ndio aliokuja kunitaka kwa baba yangu, paa ndio alionichukua kwa baba yangu, paa ndio aliopewa mimi kwa baba yangu.

Wakamwambia, Sisi hapa hatukukuona wewe, twalimwona paa ndio aliokuja, akakuta taabu hapa, ndio aliokuja, akakuta nafasi hapa. Bassi na mtu yule kuondoka katika huu ulimwengu sisi twalilia yetu, hatumlilii paa.

Wakamwambia, Paa amekufanya vema vingi, na vikiwa vema na viwe kama hivi, wala visizidi, na anenayo viko vema vizidio hivi mtu huyu mkanye tena mwongo. Ee bassi, sisi tusiokutenda vema, utafanyaje? Yule paa aliotenda vema vyote, wala hukumjua kwa kheri, wala [ 132 ]kwa shari, hatta paa amekufa kwa ghathabu na uchungu katika nafsi yake, tena umeamru watu wakamtupa ndani ya kisima! Ah! twache tulie.

Akachukuliwa paa akatupwa ndani ya kisima kilichotekwa maji.

Yule bibi aliposikia darini, akaandika barua mbiombio, upesi upesi, harraka harraka, akamwambia, Baba yangu nimekuletea barua hiyo ukiisha kuisoma, ingia njiani uje. Akaiba punda watatu, akawapa watumwa watatu, akawaambia, pandeni, mwenende mbiombio na punda, hatta mkipa baba yangu barua, akiisha isoma, mwambieni upesiupesi twenende. Na wewe nimekuacha huru, na wewe wa pili nimekuacha huru, na wewe wa tatu nimekuacha huru, kwa sababu ya barua hii mwipeleke upesi.

Watu wale wakaenda mbiombio na punda, usiku na mchana, hatta wakafika, wakampa barua Sultani. Alipoisoma barua hili Sultani akanama, akalia sana, kama mtu aliofiwa na mamaye, akaona huzuni sana Sultani. Akaamuru Sultani kutandikwa frasi. Akaenda akaitwa liwali, akaenda wakaitwa makathi, wakaitwa na jamii matajiri, waliomo katika mji. Akawaambia, haya, nifuateni upesi, tumefiwa, twendeni tukazike.

Akatoka Sultani, akaenda usiku na mchana, hatta akawasili pale kisimani, alipotupwa yule paa.

Akaingia mwenyewe, binafsi yake Sultani, ndani ya kisimani, akaingia na waziri binafsi yake, wakaingia makathi binafsi yake, kisimani, wakaingia na matajiri makuu ndani ya kisima, wakamfuata Sultani. Sultani alipomwona paa ndani ya kisiwa, alilia sana, na wale [ 134 ]waliomo wakalia sana, kwa sababu ya uchungu wa yule paa. Akimtoa Sultani paa nje. Wakimchukua.

Na wale watu watatu wakarudi wakaenda kumjibu bibi. Wakamwambia, Babako amekuja na wangwana bora walio katika mji, nao walikuja, nao wamechukua paa, wamekwenda zao. Wamwambia bibi, Si kilio kilichokuwako ndani ya kisima? Watu wote walilia kama siku aliokufa mamaye Sultani.

Akawaambia, na mimi tokea siku aliokufa paa yule, sijala chakula, wala sijanywa maji, sijanena, wala sijacheka.

Yule babaye akaenda akazika paa. Akamfanyizia matanga makuu sana, akamfanyizia na msiba mkuu sana katika mji.

Hatta baada ya kwisha msiba, yule mwanamke amelala na mumewe usiku, katika usingizi yule mwanamke akiota, yuko kwa babaye, na yule wakati anaota ule umekuwa ussubui, akafunua macho yule mwanamke, anajiona katika mji wa babaye, na nyumba ileile aliokuwa nayo kule.

Yule mwanamume akiota kama yuko pale jaani, akapekua. Na yule wakati anaota, limekuwa jua wakati wa saa ya pili, nao ndio wakati anaokwenda kupekua, killa siku. Hatta alipofunua macho, Sultani Darai akaona mkono wake u katika jaa, unapekua. Akasangaa, Ah! nimekuja na nani huku? Akatazama ya mini wa shemali haoni kitu. Akatazama mbele, aona giza, na akitazama nyuma aona vumbi. Marra pale watoto wakipita, [ 136 ]amerudi hali yake kama kwanza, watoto wakamzomea, Huu! huu! Amekwenda wapi huyu? Atoka wapi huyu? Siye twalinena amekufa, kumbe mzima bado?

Na yule mwanamke akajikalia na mali yake kule, yeye na babaye, na nduguye, na jamaa yake, raha mustarehe.

Na yule babangu mimi, maskini, akawa kazi yake ileile, kama kwanza, ya kupekua chini, na hupata punje za mtama akitafuna.

Ikiwa njema, njema yetu wote, na ikiwa mbaya, ya mwenyewe mosi, aliofanya hadithi hii.