Swahili Tales/Sultani Majinuni

From Wikisource
Jump to navigation Jump to search
Swahili Tales  (1870)  by Edward Steere
Sultani Majinuni
English translation: Sultan Majnun
[ 198 ]

SULTANI MAJINUNI.

Sultani Majinuni alioa mke, binti amu yake, akazaa naye mtoto wa kwanza mwanamume, akazaa naye na mtoto wa pili mwanamume, akazaa naye na mtoto wa tatu mwanamume, akazaa na mtoto wa nne mwanamume, akazaa naye na mtoto wa tano mwanamume, akazaa naye na mtoto wa sita mwanamume, akazaliwa mtoto wa saba kitinda mimba mwanamume. Sultani akafurahi sana kwa kupata simba wale.

Akakaa Sultani, akafanya bustani kuu, akapanda matunda yote ya ulimwengu ayajuaye yeye, naye asiyoyajua akauliza kwa watu akapata, akapanda. Akapanda na mtende moja, akapanda na jamii ya mbogamboga, killa siku aliyakwenda katika bustani marra tatu, aliyakwenda saa ya kwanza, akaenda na saa tissia, akaenda na saa edhashara u nussu.

Sultani akakaa na watoto wake, akawatia chuoni, wakasoma wakaihtimu wakafundishwa barua, wakajua.

Bassi katika watoto wale, yule wa saba, baba yake hampendi. Kazi yake yule mtoto hatoki jichoni kwa waanaake, hatoki katika chini ya vinu kwa waanaake. Akakasirika sana baba yake sababu yule kukaa kwa waanaake. [ 200 ]Amenena naye sana, hasikii, amempiga, hasikii, amemfunga, hasikii, bassi tena Sultani amechoka mambo yake, amemwachilia mbali.

Akakaa Sultani, hatta ule mtende wake, kikachanua kilele, hatta baada ya mwezi kupita, akapata dalili ya kuzaa mtende wa Sultani, akafurahi sana, akamwita waziri, akamwambia waziri, mtende wangu unazaa. Akamwambia amiri, mtende wangu unazaa. Akawaambia makathi, mtende wangu unazaa. Akawaambia na wote matajiri wangwana waliomo katika mji.

Akakaa baada za siku kupita, mtende zile tende zinafanya kuiva. Akawaita watoto wake wote sita. Akawaambia, yule mtoto mmoja hamo pamoja nanyi, amekaa kamma mwanamke, bassi nipeni shauri yenu waanangu. Wakamwuliza, kama ipi, baba? Akawaambia, nataka mtoto mmoja katika ninyi akaungojee ule mtende hatta tende ziwive, nipate kula tende zile. Siwezi kuwacha mtende ule pekeyake, naogopa watumwa watakula, ao huja ndege wakala. Bassi nataka wende ukaungojee mtende. Akamwambia, Ee walla! Akaenda zake.

Kumejengwa nyumba njema. Akikaa kitako kule hatta usiku. Akawakusanya watumwa wote wa shamba, wakapiga ngoma chini ya mtende. Aogopa yule kijana, akasema, nikilala ndani, huenda mtumwa akaja usiku akapanda juu ya mtende, akaiba tende, ao huenda akaja ndege mkubwa usiku akala tende, na tende zimewiva tena. Bassi na tucheze ngoma hapa chini ya mtende hatta ussubui.

Wakapiga ngoma, hatta ulipokoma nussu ya usiku [ 202 ]wakaona baridi sana bado hawakuweza kustahimili baridi ile. Wakacheza hatta yalipokoma saa ya kumi, wakalala wale wote chini ya mtende. Yule mtoto amekaa kitako, akaondoka mtumwa wake mmoja, akamwambia, bwana, lala ati. Akamwambia, nitalalaje mimi, na mimi nimeletwa, kungojea mtende? Akamwambia, sasa saa kumi hii, na majogoi yanawika, bassi kitu gani kitakachokuja sasa penyi mtende huu, hatathubutu, hawezi kuja mtu, wala ndege. Mtoto akamwambia, mimi siwezi kwenda kulala. Akamwambia, enende kalala kumekuwa kweupe tena. Akamwambia, wajua kweli nitakwenda lala. Akaenda zake, akalala.

Muda wa kitambo kupita, akashuka ndege akila zile tende, asisaze hatta moja. Akaruka akaenda zake. Hatta kulipopambazuka, akiwa mtu msimamizi wao akiutazama mtende, hamna tende. Akiondoka mbio, hatta kwa bwana wake mdogo, akamkuta amelala. Akimamsha, Kibwana! Kibwana! Akazindukana, akamwambia, wataka nini? Akamwambia, baba yako alikuleta kuungojea mtende na ule mtende hukuungojea, na tende zimeliwa na ndege zote. Akamwambia, sema kweli. Akamwambia, maneno haya kweli, nawe ondoka ukatazame. Akiondoka mtoto, hatta akifika penyi mtende akaona tende hamna, akasangaa. Nikienda nimwambie baba yangu, nimwambie, tende zimeliwa na watu, niseme, tende zimeliwa na ndege, ao niseme imekunya mvua mkubwa jana usiku, na tofani imevuma kubwa, nimwambie, tende zimepukutika zote chini. Ataniambia, enende kazoe, uniletee, nitazame hizo zalizopukutika na tofani na mvua, na pale chini hapana, manenoye [ 204 ]yamekuwa ya uwongo. Ah! nifanye shauri gani? Mimi nitakwenda zangu kwa baba nimwambie, walikuja Mabedui wakanifukuza, huku nyuma naliporudi tende nikitazama ndani ya mtende hamna. Ataniambia, watumwa wako wote wale msiwapige? Manenoye yamekuwa ya uwongo. Hatakubali mzee maneno haya. Mimi kesho nitakwenda kwa baba, nitamwambia, mtende mimi naliungojea hatta walipokuwa alfajiri, nako tena kunapambazuka haondoka enda kujinyosha kidogo, hatta nikipita mda kidogo kumekucha, nikimwona mtwana, akinijia akiniamsha, akaniambia, bwana, mtende hamna tende hatta moja. Nikiondoka, nikaenda hatta nikafika penyi mtende hautazama mtende, kweli, hamna tende. Bassi nami nimekuja kwako baba. Wewe kisu, mimi nyama, utakavyo vyote nitende. Haya ndiyo maneno mema, afathali kunena kweli, kama kunena uwongo.

Akaondoka hatta kwa babaye. Akamkuta babaye amekaa kitako barazini na watoto wake wale watano. Akija pale akimwamkia baba yake. Akamwambia, nipe khabari za katika bustani. Akamwambia, khabari njema mbaya. Gissi gani kuwa mbaya, gissi gani kuwa njema? Akamwambia, mbaya, ule mtende, tende zimeliwa na ndege zote, haikusaa hatta moja. Akamwambia, walikuwa wapi hatta mtende wangu ukaliwa na ndege? Akamwambia, mimi naliungojea mtende hatta alfajiri, na majogoi wanawika, tena kumepambazuka, haondoka pale kwenda kujinyosha kidogo, marra akinitokea nokoa, akaniamsha. Nikaamka hamwuliza, wataka nini? Akaniambia, wewe umekuja kuungojea mtende? Nikamwambia, nimekuja kuungojea mtende. Akaniambia bassi katika mtende [ 206 ]hamna tende hatta moja. Nikiondoka nikienda hatta mtendeni hatazama haona kweli, hamna tende hatta moja. Bassi, khabari ni hizo za katika bustani, nami sina la zayidi.

Akamwambia, nimekuuliza khabari za katika bustani, umeniambia khabari mbili, umeniambia khabari njema na mbaya, mbaya nimekwisha kuziona kama tende zangu zimeliwa na ndege, bassi nambie na hizo njema. Akamwambia na hizi njema si miye mwana nimerudi salama? Akamwambia, si mwanangu sikutaki. Akamwambia, kana mwana wewe wa kula na kulala tu, utakapokuwa mtu atakapokwambia, wee baba twaa huu mchanga unitie wa macho, hutakubali wee. Bassi mwana gani wee? Sikutaki, enda zako, baba.

Akawaambia, safari hii ukizaa mtende wangu nitampeleka mtoto mwingine, hwenda akaungojea, hwenda nikapata tende nikalimbuka.

Akakaa muda wa miezi mingi, mtende ukazaa sana usichokuwa na kifani, ukakaa hatta karibu na kuiva, nathani, imesalia siku moja kuiva. Akatwaa mtoto akampeleka. Akamwambia, mwanangu nakupeleka katika bustani, natamani tende hizi mwaka huu kuzilimbuka. Akamwambia, baba yangu, nnakwenda zangu mimi sasa, hatta ussubui likikoma jua saa ya kwanza, mlete mtu aje akutwalie tende. Akamwambia, vema, mwanangu, napenda nilimbuke tende kesho.

Akaondoka mtoto akaenda zake. Hatta akafika bustani akalala sana hatta imekuwa tena, nathani, saa saba ya usiku, akiondoka akaenda hatta mtendeni, akaziona tende nzuri, matawi yananying'inia. Akauona mtende umesitawi sana, akanena. Ah! tende hizi babangu kesho [ 208 ]atakula hizi, nitakaa mimi, kama yule mpumbafu akaja kulala usingizi burre, sasa baba amekwisha mchukia yule. Bassi mimi leo nitakaa hapa, nimtazame huyo ndege anaokuja kula tende hizi, nimwone mimi leo. Akakaa kitako akasoma sana. Akasikia majogoi yanawika, akautazame mtende akaziona tende zipo, akanena, Oh! baba yangu kesho atakula tende, athani mimi kama yule mpumbafu. Ukafanya kupambauka kidogo, ukampata usingizi. Akasema, Ah! nitegemee kidogo hapa penyi shina la mtende, usingizi ukamtwaa, ukimtwaa usingizi ndege akashukia mtende akala hatta asisaze hatta moja, naye yupo chini ya mtende, akalala, na msahafu wake kwapani.

Hatta kulipopambazuka akija yule nokoa wake, akiutazama mtende, hapana tende. Alipotupa macho chini akamwona bwana wake amelala chini ya mtende. Akamwambia, Bwana! Bwana! Akamwitikia, naam! Akamwambia umelala na tende zote zimeliwa na ndege. Kweli? Akamwambia, tupe macho juu, utazame. Akitupa macho, akaona tende hamna. Akasangaa, akili zake zimepotea, mashikio yake yameziba, miguu yake ikatetemeka, ulimi ukiwa mzito, akatekewa.

Akaondoka mtumwa wake akamwambia, Je! Bwana, una nini? Akamwambia, mimi mgonjwa sana leo. Akamwambia, kufa ku karibu kuliko kupona.

Akamwambia, ugonjwa wako gani, bwana? Akamwambia, mimi siumwi na kitwa, wala siumwi na tumbo, wala siumwi na ubavu, wala siumwi na mgongo, wala siumwi na kiuno, wala siumwi na miguu, wala siumwi na mikono, [ 210 ]viwiliwili vyangu vyote vizima, na viwiliwili vyangu vyote vigonjwa.

Gissi gani, bwana, ugonjwa huu?

Akamwambia, sababu ya ugonjwa huu ni sababu ya kuogopa leo baba yangu. Saa ya kwanza ikapiga, ataleta mtu illi kutwaa tende, nami nalimwambia baba yangu, kama kesho saa ya kwanza utalimbuka tende. Bassi mimi tena simekuwa mwongo, mimi simekuwa mpumbavu, nami baba atanifukuza kama amemfukuza ndugu yangu, kwa sababu ya kukosa kula tende.

Akamwambia, bass, bwana, utafanyaje, na jambo limekwisha kuwa?

Ah! bassi nitafanyaje tena? Nitakwenda mimi kabla hajamleta mtu hapa.

Akitoka akaenda zake. Hatta akifika katika njia amkuta mtu akichukua kombe kubwa, na kitambaa cheupe cha kufunikia tende, na kisu kikali cha kukatia tawi la mtende. Akamwambia, Je! unakwenda api? Akamwambia, nimetumwa na babako kuja kwako. Baba yako amenituma kukata tawi moja la mtende lilioiva, unitilie katika kombe hili nipeleke. Akamwambia, Yeye baba ataka zilizoiva, tende hizo mbichi zipo, rudi, twende zetu. Akamwambia, Ee walla.

Hatta alipofika mwangoni pao, akamwona baba yake amekaa kitako, yee na nduguze watu wanne. Akamwambia, Bwana, Sabalkheiri! Akamwambia, karibu. Akamwambia, umemwona mtu naliomleta? Akamwambia, nimemwona, Bwana. Nimemwambia, umkatie tawi la tende laliowiva. Akamwambia, licha laliloiva, hatta bichi liko?

Ah! wamekwenda fanya nini wee? Watu walinena, [ 212 ]kuzaa kupona, kumbe kuzaa kwangu mimi ni kufa? Vijana viwili mwaliokwenda katika bustani, pasiwe mtoto alionilimbusha tende. Bassi kuzaa huku kwa nini na watu wanena, mwenyi kuzaa kupona, na kupona huko? Msinene, ninyi watoto, mtanitia mimi roho, kupona kwangu ni kutaka kitu nikakipata, roho yangu ikafurahi, ndio kupona kwangu ni kumwona mtu ataka kunipiga, ukapigana naye ukanigombea mimi baba yako, ndio kupona kwangu, nikikutuma pahali, ukaenda, ukajua kunena na watu, ukajua mazumgumzo na watu, ukamjua mkubwa na mdogo, ukamjua tajiri na maskini, bassi ndiko kupona kwangu. Bassi, nyie waanangu, mwaka wa pili huu sipati kula tende, tende zangu mimi, huzisikia kwa mashikio, kwa macho nisizione. Bassi niondokee enenda zako. Akaondoka akaenda zake.

Akawaambia, ninyi, waanangu waliosalia watu wanne. Ukizaa sasa mtende, atakaokwenda akaungojea hatta nikapata tende nikazilimbuka, nitamfanyia harrusi ya miezi mitatu.

Killa mtu pale wale vijana wananena, baba, nitakwenda mimi; na mwingine, baba, nitakwenda mimi; na mwingine akamwambia, baba, nitakwenda mimi; na mwingine akamwambia, baba, nitakwenda mimi. Akawaambia, vema, killa atakaye na aende, lakini mimi nataka waenende mmoja mmoja. Wakamwambia, Vema, bwana.

Akakaa muda wa miezi mingi ukazaa mtende, ukazaa sana, ukaacha kuzaa, ukawayawaya. Akawaambia watoto, mtende umezaa, na mwaka huu kuzaa kwake ni sana kuliko miaka yote. Akamwambia, nitakwenda mimi baba, yule mkubwa kuliko hawa. Akamwambia, ngoja kwanza zipevuke. Bassi akakaa kitako hatta akaletewa khabari, [ 214 ]Sultani, tende linaanza kuiva. Akamwambia, haya, mwanangu, enenda katika bustani, kesho mwanangu utanilisha tende. Akamwambia, baba kesho saa ya kwanza ikipiga tende utaona katika kinwa chako unakula. Akamwambia, naomba miye mwanangu kesho nile tende hizi. Akamwambia, bassi, utakula baba, nami, kua heri, naenda zangu.

Akaondoka, akaenda zake. Hatta akawasili katika bustani, akawaambia wale watu walioko, killa mtu na alale nyumbani mwake asitoke. Tutakuachaje, Bwana, peke yako? Akawaambia, haithuru, niacheni, nimetaka mwenyewe. Wale watumwa wakaenda, wakalala. Na yeye akala, akaisha akalala, akalala sana, akiamka imekuwa saa sita, akakaa kitako chini ya mtende akicheza karata, yeye pekeyake, hatta alipokoma karibu alfajiri, ukampiga upepo mwema, akafanya kulala, usingizi ukimtwaa. Marra ndege akija akila tende zote, asisaze hatta moja, na yule mwenyewe amelala chini ya mtende na karata zake mkononi.

Hatta kulipopambazuka, nokoa wake akija, akamwona bwana wake amelala akitupa macho juu, aona tende hamna. Akamwita, Bwana! Bwana! Akamwitika, naam. Akamwambia, umelala, bwana, na tende ndani ya mtende hamna hatta moja, kama husadiki tupa macho juu utazame.

Alipotupa macho juu yule mtoto, akaanguka. Yule mtwana akisangaa alipomwona bwana wake ameanguka. Akimshika, akimwuliza, bwana, una nini? Akamwambia, nimekufa. Gissi gani, bwana kufa kwako? Kuja kwangu mimi huku shamba, nimemwambia baba yangu kama saa [ 216 ]ya kwanza ikipiga utaiona tende kinwani kwako ukila. Bassi atakapokaa hatta saa kumi haioni tende kinwani kwake akila, ao licha saa ya kumi, hatta miezi mitano, haipati tende kinwani mwake akila.

Bassi utafanyaje bwana? Akamwambia, mimi kwa babangu siendi, nitatoroka. Akamwambia, Bwana, utatoroka nini, afathali wenende, kama kutoroka, utatoroka hatta lini? Akamwambia, nitatoroka hatta baba yangu roho yake hatta iwe rathi. Akamwambia, Bwana, si vema kutoroka mngwana, afathali uende.

Akaenda hatta kwa babaye. Akamkuta hajaamka, akamngoja hatta akaamka. Je! nipe khabari za katika bustani, mwanangu. Akamwambia, sina zayidi ya khabari, khabari nalionao moja, khabari yangu za tende, zimeliwa na ndege. Ndizo khabari nalizo nazo, sina zayidi ya khabari. Utakavyo unitende. Wewe kisu, mimi nyama.

Akamwambia, niondokelee mbele uso wangu, sipendi kukuona. Akaondoka, akaenda zake. Akanena, Ahhh! mimi sikuzaa waana ni marathi. Marathi kuondoa tumboni mwana asiofaa mtu ulimwenguni, atanifaa ahera. Bassi waana hawa waana gani wasioweza kumtia mtu mchanga wa macho, kama ni kuzaa huku sizai tena.

Bassi akakaa kitako hatta mwaka mwingine, ukazaa mtende, na kulla mwaka huzidi kuzaa. Akanena alio mwanamume nitamwona katika bustani, tena nitamwona mkono wake kinwani mwangu akinilisha tende, ndiye nitakapomjua huyu mwanangu. Akawaambia, naye atakayenilisha tende, kijana huyu ntamwoza mke mzuri, [ 218 ]na harrusi miezi minne. Wakamwambia, vema baba, utakula tende mwaka huu.

Wakakaa hatta siku kumi zalipopita tende zimekuwa pevu, akaja akaambiwa, kama tende zimekuwa pevu. Akamwambia, vema, utakapoziona moja moja zinawiva, njoo nambie. Akakaa hatta muda wa siku tano, akaja yule nokoa, akaja kumwambia bwana, tende zinawiva na mapooza yanaanguka. Akakaa muda wa siku tatu, akamwambia, enende.

Akaondoka kijana kwa furaha kwa nguvu, akaenda hatta akawasili katika bustani. Akamwambia, mimi sitalala, nitapanda frasi nizunguke leo usiku kucha humo. Akatwaa bunduki yake, na baruti yake, na marisao yake, na fataki zake. Akapanda juu ya frasi, akizunguka katika bustani. Akazunguka sana hatta yalipokoma saa saba ya usiku, akasikia kaanga analia nyuma ya bustani, akanena sasa kumekuwa saa saba u nussu, nitatoka nimfuate huyu kaanga, anayolia katika bustani. Akitoka akamfuata yule kaanga kule anakolia, naye kaanga yuko mbali; lakini ule usiku anamsikia yuko karibu. Akaenda hatta nuss ya njia, ndege nyuma amekuja mtendeni akila tende, asisaze hatta moja, naye kule hajarudi, naye kule kaanga asimpate, akarudi akija zake.

Hatta alipofika katika bustani akitupa macho juu, tende hamna. Akashuka juu ya frasi, akakaa chini ya mtende, akalia sana. Hatta wakaja watumwa wake. Je! Bwana, unalilia nini? Akawaambia, mimi silii kwa kuogopa baba, nalia kwa kukosa tunu aliotaka kunitunikia baba. [ 220 ]Akamwambia, tunu gani inavyokuliza mno hivi? Akawaambia, baba ameniambia atanioza mke mzuri, atanifanya na harrusi miezi minne, naye ameniambia atajua kama mimi ndiye mwanawe, sasa zote tatu sikupata hatta moja, bassi mimi nina buddi na kulia kwa kuyakosa haya? Bassi tena nitakwenda zangu, nitamjibu.

Hatta alasiri akaenda kwa babaye, amwambia, Baba, masalkheiri! Babaye asimwitikie. Akanyamaa. Akamwambia, zi wapi tende? Akamwambia, tende, baba? tende zimekwisha liwa na ndege. Akamwambia, enende kamwambia mama yako ndani akupe dusamali, uvae, akupe na barakoa, uvae, akupe na kanzu, na suruali uvae, akupe na shela ya kujitanda, akiisha, atafute mume akuoze. Niondokelee mbele ya uso, sipendi kukuona.

Akaondoka mkewe, akamwambia, vijana hawa hawaendei kutazama huu mtende, kwenda kucheza na kulala. Wallakini tufanyeje? Na tungoje hatta safari hii tena uzaapo.

Akakaa Sultani muda miezi mingi kupita. Mtende ukazaa; akaletewa khabari shamba na nokoa wake, Bwana, mtende umezaa. Umezaa kama mwaka jana, ao mwaka huu zayidi? Amwambia, Bwana, kitu kikiwa kidogo, mtu hakitumaini, kama mtu anakitumaini kitu kilicho kidogo ningekwambia bwana, mtende huu ni nyingi kuliko miaka yote, wallakini ni kitu cha kupukutika, lakini na tutazame hatta zitakapopea. Amwambia, vema, ukiziona zinapokwanza kuanguka na mapooza, njoo nambie. Akamwambia, Inshallah, bwana.

[ 222 ]Sultani yule ana paka, ampenda sana, na paka mzuri sana, na yule paka mkuza sana, paka yule mwanzo wake aliyekikamata kuku vidogo vitoto. Akaambiwa Sultani, paka anakamata kuku, akawaambia, paka wangu na kuku wangu, bassi mwacheni.

Tende zile zikawiva shamba, akaletewa khabari na nokoa wake, akamwambia, bwana, tende zinawiva sana, nathani zikikawia hatta kesho zitaharibika kwa sababu zilioiva; na mwaka huu hazikuanguka mapooza mengi, ni kutwa ni nane tissia, kwa ginsi ya mtende kupevuka sana. Bassi nilete mtoto atakuja kuungojea mtende. Sultani akawaambia wale wawili waliobaki, akawaambia, leo enendeni nyote wawili mwaliosalia. Wakamwambia, Ee walla, baba. Wakajifunga, wakaenenda hatta wakifika katika bustani.

Wakawaambia wale watumwa walio shamba. Wakawaambia, tumekuja sisi simba, tumekuja mtazama huyu ndege anayokuja akila tende hizi, bassi leo ajali yake imekwisha, na ajali yake ni katika mkono wetu. Wakawaambia, hapa sisi labuda bunduki isiwake moto. Wakawaambia, vema, bwana. Wakakaa kitako hatta usiku. Wakawaambia, kokeni mabiwi ya moto katika bustani. Wakakoka mabiwi ya moto. Ukawaka moto sana katika bustani mle, itakapoanguka sindano utaiona kwa sababu wanga wa moto. Wakakaa hatta saa ya saba ikipiga, likatanda wingu kuu la mvua, na tufani ikawa nyingi, hatta yalipokoma saa ya nane u nussu ikanya mvua sana, na baridi nyingi, na kiza kikawa kipevu, alipo hapa hamwoni aliyo hapa, labuda wasikilizana sauti, na kumwendea mwenziwe kumpapasa, ndipo atakapomjua [ 224 ]huyu mwenzangu; na mkifanya mzaha mtatiana vidole vya macho, kwa sababu kiza kikuu. Wakakimbia wale wote watumwa, wakaenenda wakaingia katika vibanda vyao, na wale vijana wakaondoka, wakaenda wakalala. Ndege akashuka akila tende akaruka akaenda zake.

Nao hawajaamka, na mvua haijaanuka, na tufani haijaondoka, wakalala wale hatta saa thenashara zikapiga, nao hawana khabari kama kumekucha, na mvua ingalikinya, na giza vilevile, na tufani vilevile imekaza. Wakalala, hatta saa moja ikapiga. Hatta saa ya pili akitolewa mtu mjini kwa baba yao—Chukua mwavuli huu enenda zako hatta shamba, gissi gani watoto hawa? Hatujapata khabari zao, wazima ao hawawezi, tutapata tende, hapana tende, uulize khabari zao, njoo twambie.

Akitoka na mvua yake hatta shamba. Akaenda akifikia kwa nokoa, hawajaamka, amefunga mlango, amelala. Akapiga, hodi! hodi!! hodi!!! Nokoa akamjibu, nani wewe? Akamwambia, mimi Hweduni. Ah! akamwambia, kufanya nini usiku wote na mvua hizi? Akamwambia, ninyi watu wa shamba ati, wajinga ninyi mna saa zenu katika nyumba. Akamwambia, Eh! Hweduni, unatucheka tutapata wapi saa, sisi watu wa shamba? Akamwambia, unazo saa kaisha si moja, si mbili. Akamwambia, hatta kuijua hiyo saa, mimi sijui. Akamwambia; huna majogoo, ndio saa ya shamba ati. Ukisikia jogoo anawika, jue kumekucha, ao ufajiri, bassi si saa yenu hizo?

[ 226 ]Akitoka nje nokoa, wakaamkiana. Je! nipe habari ya mjini. Akamwambia, habari ya mjini njema, nimetumwa kuwatazama watoto, hatta sasa hakupata khabari zao, wazima wamekufa, wagonjwa, tende Sultani atapata alimbuke, ao hapati, bass. Akamwambia, twende nikupeleke waliko watoto. Akaenda, akawakuta wakakaa maongoni wote wawili, wamejikunyata wanatetemeka kwa baridi yalivyowashika.

Wakamwambia, Je! Hweduni! habari za mjini? Akawaambia njema, akina bwana, baba yenu salaam, baada ya salaam amwona kimya hatta sasa, jua limekuwa saa ya nne. Ah! kweli? Akawaambia, kweli saa ya nne, bwana. Wakamwambia, siye tunanena labuda sasa ufajiri? Akawaambia, hakuna bwana, mimi nimeondoka mjini saa ya pili, nalipotumwa huku shamba. Bassi yee, akina bwana, Bwana anauliza, atakula tende mwaka huu, ao hali? Akaondoka yule mmoja, umwambie atakula mwaka huu tende, pana mwaka huu, pana sasa hivi. Ngoja nikukatie, nikupe ukampelekee.

Yule nduguye akamwambia, wewe unasema kwa akili yako, ao una wazimu? Akamwambia, kwa nini? Akamwambia, nakuuliza kama umenena kwa akili yako, nipate kujua kujibu. Akamwambia nanena kwa akili yangu, wala sina wazimu. Akamwambia, wewe una wazimu khálisi, tena wazimu wako wa kutiwa pingu, na mti kati, na mnyoo, ndipo ufanywe dawa upone. Akamwambia, kama wewe huna wazimu, hungenena maneno kama hayo, kwenda kumwambia baba. Akamwambia, kwa nini?

[ 228 ]Hapa killa siku, na killa mwaka, unangojewa mtende, na ndugu zetu wasilale hatta marra moja, na wakapotewa na usingizi. Marra moja akizindukana tende zimeliwa. Bassi sisi walioondoka tokea saa saba mtendeni, tukaja zetu hapa tukalala hatta sasa saa ya 'nne, tende hizi zitungoje sisi? Killa siku watu hulala chini ya mtende, na ndege huja akala tende akaenda zake. Eh! sisi tumelala huku nyumbani, ndege huyu atangojea sisi?

Ah! Labuda báhati yetu kwa mvua ile, na giza lile, na tufani ile, labuda yule ndege hakuja. Akamwambia, bassi mvua zile, na giza lile, na tufani ile haimkatazi ndege kuja kula tende. Bassi, mimi ninakwenda tazama. Enenda wewe ukatazame, mimi siendi pahali, najua tende hakuna. Niende yani kusumbuka burre, nikapate mvua, nipate na baridi, nipate na umande wa burre, nami najua tende hakuna katika mtende, zimeliwa na ndege zote. Lakini yule anaokwenda mpumbavu, ataka kudanganya roho yake, kama hamsadiki, na ngojeni hatta atakaporudi.

Yule akaenda, hatta katika mtende, akaona hamna tende hatta moja, hatta mapooza yalioanguka chini hapana. Akarudi hatta akafika kwa nduguye. Je! tende ziko? Akamwambia, Ee bwana wee, mwenyi kuuona mtende, akiambiwa mtende huu mwaka huu ulizaa, tena jana yalikuwamo tende, hasadiki, gissi ya mtende walipo kuharibika, hatta dalili ya kuambiwa mtende huu umezaa hapana.

Akamwambia, mimi sikukwambia papa hapa, kama hakuna kitu? Sasa nipe shauri, pana shauri sasa? Na twende kwa baba yetu, tukaenda tukamwambia, tende [ 230 ]zimeliwa na ndege, hatukupata hatta moja, nasi tumekuja, wewe kisu, sisi nyama, utakalo lote, ututende? Akamwambia, vema, twende zetu.

Wakaenda hatta kwa baba yao. Wakamkuta, amekaa ukumbi wa ndani. Wakamwamkia, asiitikie. Akaondoka mkewe akamwambia, Bwana, watoto wakikuamkia, waitikie, kwani hasira yako ndio sumu yao ya kuwaua, na furaha yako ndio uzuri wa uso wao; bassi ufanyapo hivyo wewe, uwakasirikia watoto wako wambao uwaweza kuwatenda killa jawabu. Bassi huna haja kuwakasiri, wala kuwafanyia ghathabu, wala usiwafanye uchungu. Bassi, mke wangu, kawakatie kisuto, na kisuto wape na ukaya, kwani vijana hivi vimekuwa waanawake, hawamfai mtu ulimwenguni ali mzima, watamfaa mtu akhera? Lakini miye bassi, sina shughuli nao.

Wakakaa hatta muda wa miezi kupita, mtende ukazaa, ukawacha kuzaa, ukawayawaya. Mwenyi kuziona tende ndogo, nazo changa, mtu akiziona mbali hunena pevu, kwa ginsi ya tende kuwa nene, kwa ginsi ya mtende kusitawi, na tende gissi ya kuwa na nguvu, na killa tawi limejaa sana.

Akaondoka nokoa kwa mguu wake hatta kwa bwana wake, akamkuta bibi yake. Akamwambia, Bibi, bwana yu wapi? Akamwambia, yuko ndani, ngoje. Asipate mda akatoka kule ndani, akamwambia, Je! Nokoa! khabari ya shamba? Akamwambia, Shamba, bwana, kuzuri, shamba kwema, na khabari za shamba bwana, mtende umekithiri kuzaa, tena zimekuwa nene tende, ukiziona hapo zilipo changa, mtu hunena pevu, na akiambiwa hizi [ 232 ]ni changa, hasadiki. Na killa tawi lamwambia mwenziwe, jongea huku, nipishe mimi nikae.

Akamwambia, nasikitika mimi mtu mwenyi watoto saba, miaka mitano mtende wangu umeliwa na ndege, sikupata kulimbuka hatta kokwa moja, na mwaka huu vilevile, utaliwa na ndege.

Yule mtoto aliokaa jikoni akasikia maneno yale aliyoyanena Sultani Majnuni. Akaondoka yule kijana, akamwambia, baba, mwaka huu utakula tende. Akamwambia, baba yangu, kama mwaka huu sikukulisha tende kwa mkono wangu, na jamii ya matajiri yaliomo katika mji, na jamii ya Wazungu waliomo katika mji, na jamii ya Banyani waliomo, na jamii ya Wahindi waliomo, na maskini waliomo katika mji wetu, kwani haya ni matawi matano yaliomo katika mtende. Akamwambia, bassi, killa tawi ntawapa kabila mojamoja, na kabila ziliomo katika mji ni tano, mna sisi Waarabu, mna na Wazungu, mna na Banyani, mna na Wahindi, mna na jamii za maskini waliomo. Akamwambia, bassi mimi baba ninakwenda mwaka huu, kwenda kuungoja mtende.

Baba yake na mama yake wakacheka sana, wakaona maneno yake yale yote upuuzi. Babaye hakukubali maneno yale, wala mamaye, wanamwona, mwanetu anazumgumza, na tumwache azumgumze hatta shauko yake yamwishe ya kuzumgumza.

Hatta akaletewa khabari Sultani, tende zimewiva. Akatoa khabari Sultani ya kutafuta mtu kwenda kuungojea mtende. Yule mwanawe aliobaki wa saba akasikia, akamwambia, ginsi gani, baba, umetoa khabari ya kutafuta mtu wa kuungojea mtende, nami mwanao mmoja nipo bado nimesalia. Akamwambia, Ah! sita hawakufaa, [ 234 ]utafaa nawe moja? Roho yangu imefanya khofu, sababu ya mtende, nasikia umezaa sana, na tende nzuri, bassi naogopa kukupeleka kuzikosa tende kuzila. Akamwambia, na leo stahamili, nache niende baba, utazame nami bahti yangu, utakula tende, ao utazikosa.

Mkewe akamwambia, Bwana, mwache aende mtoto, tujaribu, huenda tukapata tukala tende, ao tutakosa, bassi mwache aende mtoto. Akamwambia, mke wangu, miye sikatai kwenda mtoto, roho yangu hayamini. Akamwambia, haithuru bwana, mwache aende mtoto. Akamwambia, baba, kesho tukiwa wazima mimi, nawe, na mama, kesho utakula tende baba. Akamwambia, na nduguzo walinena vivi hivi, kama baba utakula tende, nami sili. Akamwambia, haya enenda zako shamba.

Hatta alipofika katika bustani, Akawaambia watumwa wote wa shamba, laleni. Wakamwambia, Ah! bwana tutakuacha pekeyako? Akawaambia, usiku haunili kama ntauogopa. Wakamwambia, bass, bwana, kua heri. Akawaambia, kua herini.

Na yule kijana akaingia ndani akalala, akalala sana hatta saa ya saba ikipiga, akiondoka akija hatta mtendeni. Akakaa kitako akitafuna bisi, na zile bisi ndani zina changarawi; hutafuna zile bisi, akitaka kusinzia, hutafuna ile changarawi, akiamka, ikawa kazi hiyohiyo, hatta yule ndege akija, naye amemwona.

Yule ndege alinena, hapana mtu, kwani yeye alikaa mbali na mtende. Hatta alipotua palipo mtende, yule kijana akaondoka, alipotaka kunyosha mdomo kula tende, amemshika bawa.

Ndege kuondoka kwake panapo mtende aliruka, [ 236 ]akaruka naye kijana, hatta akafikilia naye juu. Akamwambia yule ndege, Ee, binadamu, umenifuata hatta huku nalikofika, ukianguka hapa hatta utakapofika chini, umekufa zamani, bassi uniache nikaende zangu, nawe nikakwache kwenda zako. Yule kijana akamwambia, mimi leo hapa sikwachi, utakapokwenda pote nitakwenda nawe. Akamwambia, mimi tende zako sikula, nami niache nende zangu. Akamwambia, mimi leo sikwachi, mimi hapa leo ni kama kupe na mkia wa ng'ombe. Akamwambia, niache nende zangu kumekucha tena. Akamwambia, mimi leo naliokwambia husikii? mimi hapa sikwachi, labuda uniue. Akamwambia, ndugu yangu sita hawapendezi kwa baba kwa sababu yako wewe, huja akila tende, bassi ntakuachiani leo? Mimi leo baba yangu atakuona, na ndugu zangu sita watakuona, na mama yangu atakuona, na wote watu waliomo katika mji wetu watakuona, mkubwa kwa mdogo, mtumwa kwa mngwana, mke kwa mume, hawa wote watakuona leo, ndio roho ya baba yangu leo itafurahi.

Akamwambia nache, kunakucha, nami tende zako leo sikula, bassi utafathali ukanacha, nami nikaenda zangu, nawe ukaenda zako. Akamwambia, mimi hapa leo siachi, labuda uniue. Akamwambia, bassi wewe hutaki kunacha, nitakurusha nikupeleke mbali sasa.

Akaruka naye sana juu, hatta yule mtoto akiona chini kama nyota. Akamwambia, je! umekuona kwenu? Akamwambia, nakuona kama nyota. Nikikutupa hapa, wewe utasalia? Akamwambia, nastahiba uniachie nife, kama kukuacha leo, sikuachi kabisa, utaporuka hatta ukafika mbingu, nami leo sikwachi.

[ 238 ]Akamwambia, kunakucha, nataka kwenda zangu uniachie, mtoto, tafáthal nitakwenda zangu. Akamwambia, sikuachi kabisa leo, utakapopita ntapita nawe, utakapokaa ntakaa nawe, utakapokufa ntakufa nawe, lakini leo mimi sikwachi.

Akashuka ndege hatta chini, akamwambia, sasa umefika kwenu hapa, nami nipe ruhusa nende zangu. Akamwambia, sikwachi. Akamwambia, tafáthal mtoto uniache. Akamwambia, Ndugu zangu aliopewa ukaya, amepewa, aliopewa kisuto, amepewa, aliovikwa kanzu na barakoa, amevikwa, na yote haya hayangewapata illa kwa sababu yako wewe, kwa kuja kula tende.

Akamwambia, tafáthal, bassi kunakucha sasa bwana, nache, hichi kikomo cha leo, sitakuja tena hapa, wala sitakula tena tende hizi, wala sitapita tena mtaa huu, tafáthali kijana niache nende zangu.

Akamwambia, kama wewe hutaki kuniacha na tupane wahadi mimi nawe. Amwuliza, upi? Akamwambia, mimi nitakupa wahadi, niponye la jua, nikuponye la mvua. Akamwambia, mbona? Sikuamimi. Akamwambia, twaa haya maneno yangu, utakapopita po pote utanipata. Eh! ntakupataje? Akamwambia, ukitwaa hili nyoya, ukitia motoni nikisikia harufi yake, nitakapokuwa pahali gani nitakuja. Akamwambia, bassi nami kunakucha, tafáthali watu wasinione, niache niende zangu. Akamwambia, bassi kua heri, enenda zako. Akamwambia, rafiki yangu, kua heri sana. Amwambia, utakaponiita, [ 240 ]itakapokuwa katika bahari, ntakuja. Akamwambia, vema. Akaruka, akaenda zake.

Mtoto akirudi katika mtende, akauona mtende, akaziona na tende, akaona na roho yake imefurahi, moyo uliona nafsi yake kama alikuja mtu akamwambia, haya ondoke ende peponi, gissi ya roho yake alivyoiona nzuri, alivyoiona imefurahi, alivyoiona mwili wake na nguvu, anavyojiona macho yake yana nuru. Akacheka kijana sana, akanena hii ni bahati yangu mimi, mkaa jichoni. Walikuja simba sita hapa, killa mtu upanga na ngao, na jamvia kiunoni, na bakora mkononi, na killa kijana amwambia mwenziwe, jongea huku nipishe nami. Kwanza vijana vina nguvu, la pili vijana vizuri, la tatu wajuikana sana katika mji kuliko mimi mkaa jichoni. Lakini hii bahati yangu Muungu amenipa. Kiwekwacho na Muungu, mwana Adamu hawezi kukiondoa, illa yeye aliokiweka.

Akiondoka kijana akamwambia, mtende, kua heri, nami nakwenda lala, alio akikula, sasa hatakula tena, leo hili limekuwa zingizi kumkomesha mzazi. Akaondoka, akaenda akalala.

Hatta usiku ulipopambauka, akija hatta pale mtendeni akajifunuka shuka, akalala. Hatta nokoa wake akaamka. Nikautazame mtende huo leo, kama tutapata haya makombo ya ndege yanaosalia, kwani mtende huu, mtu hauoni tende. Akija nokoa, hatta alipokoma nussu ya njia alipotupa macho kunako mtende kule, akauona mtende umemkalia tamu.

Akirudi mbio hatta nyumbani akipiga goma, wote wajoli wake wakaja, wake kwa waume, hatta watoto [ 242 ]wakachukuliwa. Je! nokoa tupe khabari waliotutia. Akawaambia, naliokutiani? Wakamwambia, twambia nokoa wetu. Akawaambia, bwana hakuzaa mwana, amezaa simba. Akawaambia, katazameni mkaa jikoni, alivyofunua uso wake leo kwa baba yake. Gissi gani, nokoa? Akawaambia, leo siku ya watu kula tende. Kweli, nokoa? Akawaambia, na'am.

Akawaambia, kwanza msiende kumwamsha illa twende tukampukuse, mwenyi kuku na achukue kuku, na mwenyi mbuzi na achukue mbuzi, na mwenyi mchele achukue mchele, na mwenyi mpunga na achukue mpunga, na mwenyi ngano achukue ngano, na mwenyi fetha achukue fetha; lakini mtama, na muhindi msichukue haya.

Watu wakaenda majumbani mwao, wakaja, aliochukua kuku amechukua, aliochukua mbuzi amechukua, aliochukua mchele amechukua, aliochukua mpunga amechukua, aliochukua ngano amechukua, aliochukua fetha amechukua. Wakachukua na ngoma, wakamkuta amelala chini ya mtende.

Wakaenda pale wakamchukua kwa baragumu, kwa zomari, kwa ngoma, na kofi, na vigelegele hatta kwa babaye.

Babaye aliposikia shindo linakuja njiani, na matawi la mtende limechukuliwa ndani ya pakacha, alipoona watumwa wa shamba wanakuja kwa furaha, alipomwona na mtoto amechukuliwa juu kwa juu, Sultani Majnuni alijua, leo nitakula tende. Akamwita, mke wangu! Akamwitika, lebeka, bwana. Akamwambia, bwana wa jiko leo [ 244 ]atatulisha tende. Aliposikia maneno yale, yule mwanamke aliacha kupika akaenda mbio darini. Akamwambia, nini, bwana? Akamwambia, tazama katika dirisha. Alipotazama amwona mwanawe anakuja kwa furaha na wale watumwa, waliokuja kwa furaha.

Babake akaamuru asikari, mfuateni, mkamtwae mtoto. Wakaenda asikari mbio, wakaenda wakamchukua hatta akifika kwa babaye.

Je! khabari mwanangu. Akamwambia, sina khabari, khabari yangu ni kufunua kinwa hakulimbusha tende. Akamwambia, na'am, ndio kuzaa huku nilimbushe mwanangu. Akichuma tende, akamtia baba yake kinwani. Akachuma tende, akamtia mama yake kinwani.

Akamwambia, huku mwanangu ndio kuzaa, si kama wale wapumbavu, si kama wale asherati. Akamwambia, Je! mwanangu walimfanyaje ndege huyu, mwalimngojea wewe na nani, ndege huyu. Akamwambia, ndege huyu nalimngojea mimi peke yangu, nami hamwona tena, wala hatakuja tena maisha yake, na maisha yako, na maisha ya wangine watakaokuja.

Akamwambia, mwanangu, hapana jambo lalionipendeza kwako, kama hili walionilimbusha tende, kwani nimekaa miaka mitano mimi sikupata kulimbuka tende. Nami nna watoto sita, wala si mmoja, wewe naliokwambia mpumbavu ndio walionilimbusha tende. Hawa mimi siwataki.

Akaondoka mamaye akaenda kwa mumewe, akamwambia, si wakatae, mwenyi kukataa mwana hukataa mwana wa haramu, na wewe Sultani Majnuni, ukiwakataa watoto hawa, watu watawaambia waana wa haramu, na mimi [ 246 ]mkeo sina uso kwa watu. Killa nitakapokwenda, katika ukumbi wa watu, sitaweza kuinua uso wangu kutazama watu pia, wake kwa waume, wangwana kwa watumwa, wadogo kwa wakubwa, wataniambia mimi kama nimezaa kwa haramu. Bassi wewe, Bwana, wapenda niambiwe maneno kama hayo na watu? Akamwambia, hasha, sipendi mimi waambiwe maneno mabaya na watu, licha ya haya hatta mangine mabaya, sipendi waambiwe na watu. Napenda mimi nikupe maneno mema na wote watu watakaosikia katika inchi hii ao inchi nyingine, wakiambiwa kama Sultani Majnuni humpa maneno matamu mkewe, hamkasiri mkewe, lile atakalo mkewe ndilo amfanyalo, na watu wangine watakufanya kama yale. Akamwambia, ahsanti, bwana wangu, ndilo jambo nalilotaka kwako, nami nimelipata. Na vijana na vikae kitako.

Bassi yule kijana kitinda mimba, akipendwa sana na babaye, na bibi akimpenda sana, na shangazi lake akimpenda sana na mjumba wake akimpenda sana, kuliko wale nduguze watu sita. Wale watu sita walikipendwa sana na mama yao, kuliko yule kitinda mimba. Yule mke akamwambia mumewe, siachi wingi kwa uchache, siachi waana sita hampenda mmoja.

Bassi wakakaa kitako, hatta yule paka wa Sultani akaenda akakamata ndama wa ng'ombe. Akaenda akaambiwa Sultani yule, paka amekamata ndama wa ng'ombe, akawaambia, paka wangu na ndama wangu. Wakamwambia, vema, bwana.

Wakakaa baada ya siku mbili tatu, akakamata koo la mbuzi. Wakamwambia, Bwana, paka amekamata koo la mbuzi leo. Akamwambia mbuzi wangu na paka wangu.

Wakakaa baada ya siku mbili, akakamata ng'ombe. Akaenda akaambiwa, bwana, paka amekamata ng'ombe. Akawaambia, ng'ombe wangu na paka wangu.

[ 248 ]Akakaa baada ya siku ya pili, akakamata punda. Akaenda akaambiwa, Sultani, paka amekamata punda, akawaambia, punda wangu na paka wangu. Akakaa baada ya siku moja, akakamata frasi. Akaenda akaambiwa Sultani, bwana, paka amekamata frasi. Akawaambia, paka wangu na frasi wangu. Akakaa akajikamatia ngamia. Akaambiwa Sultani, paka leo amekamata ngamia. Akawaambia, wamtakia nini, paka wangu na ngamia wangu, ninyi paka huyu hampendi mwataka ni'mue, killa siku kuniletea maneno maneno tu. Nami si'mui mwacheni ale ngamia, hatta mtu na ale.

Akakaa hatta siku ya pili, akakamata mtoto wa mtu. Akaenda akaambiwa Sultani paka amekamata mtoto wa mtu. Akawaambia paka wangu na mtoto wangu. Akakaa siku ya pili akakamata mtu mzima, akaenda akaambiwa, amekamata mtu paka, bwana. Akawaambia, paka wangu na mtu wangu.

Akahama mjini yule paka, akakaa kama katika Mnazimoja katika magugu. Bassi akipita mtu hwenda maji, humla, akiona ng'ombe akipita kwenda kuchungwa, akamkamata akala. Akiona mbuzi akamata, akila. Kitu akionacho cho chote kinachopita katika njia ile, akamata akila.

Watu wakaenda wakamwambia Sultani, Gissi gani Bwana, wewe ndio Sultani wetu, wewe ndio bwana wetu, wewe ndio ngao yetu, umemwacha yule paka bwana, amekwenda kaa Mnazimoja, akipita mtu humla, akipita ng'ombe humla, akipita punda humla akipita mbuzi humla, cho chote kitu kinachopita katika njia ya Mnazimoja hukamata akila, na usiku hushukia katika mji, aonacho [ 250 ]cho chote katika mji hukamata akala. Bassi, bwana, tufanyeje mambo haya?

Akawaambia, nathani ninyi roho zenu, paka huyu hampendi, wataka ni'mue, nami sita'mua paka wangu na hivyo anavyokula vyangu.

Bassi watu wakasangaa, hapana mtu anaothubutu ku'mua, na watu wamekwisha kuliwa na paka. Akakaa njia ya Mnazimoja, tena watu wasipite njia ile; paka akahama njia nyingine, akikamata vilevile.

Wakaenda wakamwambia Sultani, paka anahasiri watu. Akawaambia maneno yenu mimi siyataki, maneno yenu kwangu madogo, wala sisikii maneno haya, wala paka si'mui.

Watu wakahama njia ile wasipate. Akahama njia nyingine akafanya kama yale. Akaambiwa Sultani, amezidi paka, bwana, amekuwa mkali kabisa, hakipiti kitu mbele yake, amekidaka. Akawaambia, paka wangu na hicho anachotwaa changu. Wakahama watu, wasipite njia ile.

Akaona yule Sultani maneno yamekuwa mengi ya watu, aka'mweka mtu mwangoni. Killa mtu atakayekuja hapa kwa mashtaka ya paka, mwambia, bwana hapatikani. Akamwambia, Ee walla, bwana.

Bassi usiku paka huja mjini, akikamata killa apatacho, na ufajiri hurudi akaenda zake kiungani. Hatta mle viungani hamna watu; waliokimbia, wamekimbia, na waliokamatwa, wamekamatwa. Akajongea mbali ndogo mashamba yule paka, akikamata huko watu na nyama, na [ 252 ]usiku huja mjini, akakamata akipatacho na ufajiri akaenda shamba. Na killa watu wakimwendea kumpa khabari Sultani, kwa maneno ya paka, hawampati.

Akazidi kujongea mbele shamba yule paka, hukamata akipatacho, akipata kuku, akipata mbwa, akipata mbuzi, akipata ng'ombe, akipata mtu, cho chote kimpitiacho mbele yake hukamata, na asipokiona kitu cha kukamata hufanya juhudi ukitafuta, na usiku wa mjini, na ufajiri akaenda shamba. Kazi ikawa ileile, ya kukamata paka na Sultani hapatikani.

Hatta siku hiyo Sultani akanena, mimi leo natazama shamba, tendeni tukatazama, watoto. Akafuatana Sultani na watoto wale sita. Wakaenda hatta katika njia pana magugu, wale watoto sita huko nyuma, baba yao yu mbele. Yule paka akatoka katika mwitu, akiwaua watoto watatu. Watu wakaruka, paka! paka! paka! paka! Wakamwambia asikari, Je! Bwana tumtafute tu'mue. Akawaambia, tafuteni m'mue. Wakamwambia, Ee walla, bwana.

Akawaambia, huyu hakuwa paka tena, huyu jina lake nunda, aliokuja kunikamatia hatta waanangu. Wakamwambia, Bwana yule paka hatachagua, huyu mwana wa bwana, nimwache, ao huyu mke wa bwana nimwache, ao huyu jamaa yake bwana, nimwache; neno hili hakuna kwake la paka huyu kuchagua. Twakuchelea bwana hatta wewe kukula. Akawaambia, kweli hatta mimi atanila. Hatukwambia bwana, kama paka huyu anakwisha watu, ukanena, paka wangu na watu wangu? Akawaambia, kweli nimenena.

Wale asikari walipokwenda kumpiga yule paka, wangine [ 254 ]wakauawa, wangine wakakimbia. Yule Sultani akarudi na watoto wale, akaja akazika.

Yule mtoto wa saba, alio nyumbani, alipoona khabari zile za nduguzo walipouawa na paka, akamwambia mama, nami nitakwenda, paka aniue kama alivyoua ndugu zangu. Akamwambia, wee utakwendaje mtoto peke yako? Akamwambia, mimi nitakwenda kwa uchungu wa ndugu zangu, siku moja mtu kuondokewa na watu watatu katika dunia, bassi mtu huyu asifanye uchungu? Bassi mimi ntapotea, nikamtafuta yule paka aliowaua ndugu zangu. Akamwambia, vema mwanangu, lakini mimi sipendi uenende. Akamwambia, hawa wamekufa na wende ukafe, juu ya donda si donda? Akamwambia, sina buddi mama ntakwenda kwa jambo hili, wala baba simwambii.

Yule paka tena amekimbia mbali sana. Akafanyizwa mikate na mama yake, akapewa na watu wa kumchukulia vyakula. Akapewa na mkuki mkuu mkali kama wembe, na upanga wake. Akamwambia, mama buriani. Akatoka, akaenda zake.

Hatta alipokoma viungani akaona jibwa kubwa, akampiga, akamfunga, anamkokota. Akaja anakwimba.

Mamá wee, niulága
Nundá mla wátu.

Hatta akafika hatta karibu na mji. Mama yuko juu, akamwona, akamsikia anakwimba,

Mamá wee, niulága
Nundá mla wátu. (Marra 'nne.)

Akamjibu mamake, akamwambia,

Mwanángu, si yéye
Nundá mla watu.

[ 256 ]Na yule mtoto amekaza kule kwimba,

Mamá wee, niulága
Nundá mla watu. (Marra tano.)

Na mamaye akamjibu,

Mwanángu, si yéye
Nundá mla watu. (Marra mbili.)

Akamwacha yule jibwa.

Akamwambia, Ee! siye nunda, yule nunda mkubwa, uwache mwanangu, ukakaa kitako. Akamwambia, mama si jambo la kupatikana mimi la kukaa kitako. Akatoka akaenda zake mwituni.

Akaenda mbali kuliko siku ile, na watumwa wake waliomchukulia chakula. Akaenda akamwona fungo, aka'mua, akamfunga akamkokota, akija naye, hatta alipokoma nussu ya njia akaimba,

Mamá wee, niulága
Nundá mla watu. (Marra sita.)

Mwanángu, si yéye
Nundá mla watu. (Marra tatu.)

Akamtupa.

Akamwambia, mwanangu huachi ukakaa kitako? Utataabika sana, tazama siku hizi mbili umekuwa mweusi. Akamwambia, mama sina buddi na kwenda twaa kisasi cha ndugu zangu. Akamwambia, enenda.

Akaenda katika mwitu mbali zayidi kuliko juzi. Akaenda, akamwona ngawa, aka'mua, akamfunga, [ 258 ]akamkokota. Alipokuja hatta alipokoma nussu ya njia, akaimba,

Mamá wee, niulaga
Nundá mla watu. (Marra saba.)

Mwanángu, si yeye
Nundá mla watu. (Marra nne.)

Akamtupa.

Akamwambia, utapata wapi nunda huyu naye mbali, nawe humjui alipo, utataabika sana mtoto, uso wako umebadilika kwa siku tatu hizi, utafathali ukakaa kitako. Akamwambia, sina buddi, mama, ya kuenenda. Akamwambia, mama maneno matatu nitapata moja kwa Muungu. Akamwambia, la kwanza mwanangu? Akamwambia, la kwanza ntakufa. Akamwambia, lapili, mwanangu? Ao ntampata nunda, ni'mue. Akamwambia, la tatu mwanangu? Ao ntamkosa nunda nirudi. Bassi matatu haya mama, sitakosa moja kwa Muungu. Akamwambia, mimi mwanangu napenda umpate huyu nunda uje nawe, na roho yangu nimwone, iwe safi. Akamwambia, bassi mama kua heri, naenda zangu.

Akaenda mbali kuliko siku ile, akaenda akamkuta punda milia, aka'mua, akamfunga akamkokota, akaja zake hatta nussu ya njia, akaimba,

Mama wee, niulaga
Nunda mla watu. (Marra nane.)

Mwanangu, si yeye
Nunda mla watu. (Marra tano.)

Akamwacha.

Akamwambia utafathali mwanangu, ukae kitako, roho yangu imefanya khofu, mwanangu. Akamwambia, una [ 260 ]khofu ya nini mama? Akamwambia, kama khofu yako mama ya kufa, nitakaa hatta lini, sina buddi ntakufa. Akamwambia, naenda zangu. Akamwambia, kua heri.

Akaenda akaingia katika msitu na nyika, akaenda, akamkamata twiga. Aka'mua, akafurahi sana roho yake, akanena, huyu ndio khalisi nunda. Akamfunga, akamkokota, hatta akija akikoma nuss ya njia, akaimba,

Mama wee, niulaga
Nunda mla watu. (Marra kenda.)

Mwanangu, si yeye
Nunda mla watu. (Marra tano.)

Akatwaa akamwacha.

Akamwambia, mwanangu, taabu unazo kupata peke yako, nawe unao nduguzo watu watatu hapa, hapana mmoja anaonena, naswi tumfuate yule mdogo wetu, kwenda naye mwituni, tukamtafute huyu nunda. Hapana. Wote wamekaa kitako na shughuli zao, unasumbuka peke yako, mwanangu. Akamwambia, tumbo waliotoka wewe ndio waliotoka wale, na baba yenu ndiye mmoja Sultani Majnuni. Si kwamba mna baba wawili, ukasumbuka peke yako, lakini baba yenu ndiye huyu mmoja. Akamwambia, mama killa mtu ana roho yake, tungezaliwa tumbo moja, na killa mtu ana roho yake. Akamwambia, bassi mwanangu usiende, hizi siku walizokwenda bass. Akamwambia, mama ndilo jambo lisio buddi, sina buddi ntakwenda. Mamaye akalia sana, na babaye akalia sana, sababu wamefanya khofu, kwa mwanetu atakufa, na huyu ndio mwana bora tulionaye. Lakini tutafanyaje? Hakubali kukaa.

Akaenda msitu na nyika, hatta akaenda akamkuta faru, [ 262 ]amelala katika mti mkuu, akawaambia watumwa wake, leo tumemwona nunda yule. Yu wapi, bwana? Yule chini ya mti. Ee, tufanyeje, bwana? Akawaambia, sasa na tule kabisa, tupate kwenda kumpiga, tumempata vema, akituua, bassi. Wakamwambia, haya, bwana, wakatoa mabumunda, wakala hatta wakashiba. Akawaambia, na killa mtu na ashike bunduki mbili, moja iwe chini, moja iwe mkononi mwake. Wakamwambia, Ee walla, bwana. Akawaambia, na tupige marra moja hizi zote. Wakamwambia, Ee walla, bwana. Wakaenda polepole ndani ya miiba ile, hatta wakaingia katika mwitu pale, wakamtokea kwa mgongoni wakamjongelea hatta akawa karibu yao, wakampiga, risasi zika'mingia sana. Akatoka mbio yule faru pale alipopigwa, akaenda, akaangukia mbali kidogo. Wakamfuata, hatta wakamwona ameanguka amekufa. Wakamfunga, wakamkokota muda wa siku mbili njiani, hatta walipofika nuss ya njia wakaimba,

Mama wee, niulaga
Nunda mla watu. (Marra kumi.)

Mwanangu, si yeye
Nunda mla watu. (Marra saba.)

Wakaja watu wengi kumtazama yule faru, wakamsikitikia sana yule kijana.

Babaye na mamaye wakalia sana. Wakamwambia, baba ukae kitako. Akawaambia, baba yangu, naliokwambia halirudi nyuma, kama kufa mimi hivyo ninavyokwenda killa siku, nami nimekwisha kufa, lakini sijui, bassi niacheni, mimi.

Babaye akamwambia, ntakupa mali uyatakayo, ntakupa na enzi yangu, uwe wewe Sultani, mimi nishuke, nikae [ 264 ]mtu kwako wa kunipa chakula na nguo tu. Nawe usiende mwituni, mwanangu. Akawaambia, kua heri, baba, naenda, haya yako siyasikii.

Akaenda msitu na nyika, akaenda akamkuta ndovu amelala athuuri katika kichaka. Akawaambia watumwa wake, leo tumemwona nunda. Wakamwambia, vema, bwana, yu wapi? Akawaambia, yule katika kichaka, mtazameni sana. Wakamwambia, bassi bwana, hatumjongelei pale alipo? Akawaambia, tukimjongelea uso wake, kama anatazama huku tunakokuja sisi, hatatujia? Na akitujia atatuua sote. Lakini sasa na tufanye shauri tumtoe mtu mmoja akamtazame uso wake umelekea wapi, uje atwambie. Wakamwambia, vema, shauri jema bwana, na sisi bunduki ziwe tayari.

Akatoka mtwana wake mmoja, jina lake Kiroboto, akitambaa kwa magoti katika mwitu, hatta akakaribia alipo. Akamwona amelala, na uso umelekea upande mwingine.

Akirudi kwa magoti vilevile, hatta akafika alipo bwana wake. Je! tupe khabari. Akamwambia, habari njema, bwana. Akamwambia, yeye ndiye nunda? Akamwambia, miye, bwana, simjui, lakini huyu ndiye nunda bwana hana shaka; mpana, kitwa kikubwa, mashikio yake, nimeyaona bwana mkubwa sana. Akamwambia, ndiye bwana nunda.

Haya, na tule bassi, tupate kumwendea, wakatoa mabumunda, wakatoa na ladu, wakatoa na mkate wa kumimina, wakala; wakala sana, hatta wakashiba.

[ 266 ]Akawaambia, akina baba! Akawaambia, siku ya leo labuda ndio riziki yetu ya mwisho, bassi leo watu hutakana buriani, atakaopona atapona, na atakaokufa atakufa, lakini atakaopona kama mimi nimekufa, na akamwambie mama na baba asifanye msiba. Wakamwambia, haya bwana twende zetu tutapona inshallah.

Wakaenda zao kwa magoti, hatta wakifika pale kichakani, alipo. Wakamwambia, tupe shauri, bwana. Akawaambia, hapana shauri illa na tumpige tu marra moja. Wakampiga marra moja. Ndovu akawafukuza, killa akatupa bunduki yake aliokuwa nayo, hatta nguo waliovaa wakaziona nzito, wakazitupa kwa sababu ya kwenda mbio, killa mtu akapata mti akapanda. Ndovu akaenda zake akaanguka upande mwingine.

Wale wakakaa juu ya mti killa mtu tokea saa ya tissia hatta saa ya thenashara ussubui, hawana kula, hawana nguo, wamekaa kama siku walipozaliwa katika matumbo ya mama yao.

Yule kijana juu ya mti akalia sana. Akanena, mimi kama sijui kufa, ni huku leo kufa. Na killa mtu hamwoni mwenziwe. Yule kijana ataka kushuka juu ya mti aogopa, asema, labuda nunda yuko chini atanila, na wale watumwa wake vilevile, waogopa kushuka, wasema labuda nunda yuko chini atatula. Nao katika mwitu ulio mkuu, si pahali peupe.

Yule Kiroboto amemwona yule nyama alipoanguka, lakini aogopa kushuka peke yake, hunena, labuda pale alipoanguka, anena, yule mzima bado hajafa; hatta alipomwona mbwa anakuja kumnuka, akajua kama kweli amekufa.

[ 268 ]Akashuka juu ya mti kwa nguvu, akapiga kikorombwe, akajibiwa kikorombwe, akapiga tena kikorombwe marra ya pili, akatega shikio lake—hivi—upande, apate kusikia atakapojibiwa kikorombwe kule, aenende. Akajibiwa kikorombwe marra mbili, akaenda hatta akawakuta wajoli wake wawili juu ya mti. Akawaambia, haya shukeni nunda amekufa. Wakashuka wale mbio, akija zao katta wakimkuta bwana wao, akawaambia, Je! Shindano! Akamwambia, tumefuatana bwana na Kiroboto, nunda amekwisha kufa, bwana, ushuke. Akashuka, akifika chini pale wakikutana wote. Killa mtu akatafuta nguo yake, akavaa. Wakatafuta bunduki zao, wakatafuta yale majamanda, yaliotiwa mabumunda, wakaja, watoto wamekonda kwa siku ile moja.

Wakakaa kitako kule wakala vyakula vyao, wakanywa na maji, wakaenda hatta kule alikoanguka nunda. Kijana alipomwona, akanena, ndiye nunda, ndiye, ndiye! Ah! kweli, bwana, ndiye.

Wakamkokota siku tatu njiani. Hatta wakatoka katika mwitu; roho yake ina furaha, ndiye nunda, akaimba,

Mama wee, ndi yeye
Nunda mla watu. (Marra kumi na moja.)

Mwanangu, si yeye
Nunda mla watu. (Marra nane.)

Ah!——uthia huu, mwanangu, uliokupata! Na watu wa mjini wanataajabu udogo wako, na akili zako kwa kuwa nyingi. Na babaye akamwambia, hapa walipokuwa bass. Usende tena mbele. Akamwambia, baba, mimi sina buddi kwenenda, labuda Mwenyi ezi Muungu [ 270 ]ameniandikia mauti yangu kuwa huku hatika mwitu. Akamwambia, mwanangu, lile nalilokwambia nifuate. Akamwambia, Ee walla, bwana wangu, mambo yote nitakufuata, bwana wangu, lakini hili moja nami nipe hisa. Akamwambia, enenda, lakini safari hii ukirudi hutakwenda tena. Akamwambia, nami, baba, nikiwa mzima hatta nikirudi, roho yangu imenihubiri siendi tena. Akamwambia vema, mwanangu.

Akaenda zake msitu na nyika, hatta akapita mwitu mkubwa, akiona kilima kikuu sana, na kule juu ya kilima, kuna kilele kikuu sana. Akaona njia inakwenda hatta imeshuka chini ya kilima. Akawaambia, Je! watumwa wangu, shauri yenu. Wakamwambia, kama ipi, bwana? Akawaambia, shauri ya kwanza, sasa hapa tuliopo sisi, nataka tupande mlima mkuu hatta tufike juu ya kilele, tutazame gissi yake mji, tuna nafasi kupata kwenda mbele. Wakamwambia, Bwana, mbona sisi hatuwezi kupanda katika mlima. Akawaambia, kama nyie mwaogopa, jua limekuchwa, na tulale hapa hatta kesho. Wakamwambia, vema, bwana.

Wakatwaa mabumunda pale, wakatwaa na mkate wa kusonga, wakala, wakatwaa na ladu, wakala, wakashiba, wakanywa maji, wakalala; wakapata usingizi mwema sana. Killa mtu hakufahamu hatta ussubui jua linachomoa, wakaamshana, haya, ondokeni kumekucha. Tufanye shauri kungali na mapema bado.

Wakamwambia, haya, bwana, tumeamka, tupe shauri yako. Akawaambia, shauri ya kwanza, na pike wali, tule. Akawaambia, twaa, mpekeche moto mpike wali, tule upesi. Wakapika wali pale, wakaisha, wakamwambia, Bwana, wali umekwisha. Akawaambia, kama umekwisha, pakueni.

[ 272 ]Akawaambia, leo roho yangu naiona itapata mambo matatu katika ulimwengu kwa siku ya leo. Wakamwuliza, la kwanza, bwana? Akawaambia, la kwanza, leo naona roho yangu, ntakufa. La pili, bwana? Nathani leo nitampiga nunda. La tatu, bwana? Akanena, nathani ntaonana na mama yangu, ntaonana na baba yangu ntaonana na mjumba wangu, ntaonana na shangazi langu, ntaonana na ndugu zangu, ntaonana na wote rafiki zangu. Wakamwambia, heri, bwana.

Wakakaa kitako pale, wakapakua wali, wakala, wakala sana, wakashiba. Wakaondoka. Akawaambia, na tupande sasa juu ya mlima. Wakamwambia, Ee walla, bwana. Akatangulia na watumwa wake, Shindano na Kiroboto. Wakapanda, wakaenda hatta walipotupa macho nuss ya mlima, wakaona chini mbali sana, wakaona na juu mbali. Akawaambia, msiogope na twende. Wamwambia, na twende hatta tufike juu ya mlima, tusipande juu ya kilele.

Wakaenda hatta walipofika juu ya mlima macho yao yaona mbali. Akawaambia, na tupumzike hapa juu. Hapa nafasi tele. Bassi wa leo tulale kuku huku hatta kesho, tufanye shauri. Wakamwambia, vema, bwana.

Akaondoka yule mtumwa wake mmoja, akazungukazunguka juu ya mlima. Alipotupa macho chini, aona nyama mkubwa, lakini kule chini kiza kwa miti hamwoni vema. Akamwita, Bwana! Bwana! Akamwitika, naam. Akamwambia, njoo tazame, bwana. Akaenda hatta akifika pale aliposimama Shindano, akamwambia, tupe macho [ 274 ]chini sana. Yule mtoto akitazama, roho yake ikamhubiri kuwa ndiye nunda.

Akishuka yule kijana yeye na bunduki yake mkononi, na mkuki wake, hatta akipata nussu ya mlima, akatazama huyu, hapana buddi ndiye nunda. Mama yangu alinambia masikio yake madogo, na huyu yake madogo; alinambia, nunda mpana si mrefu, na huyu mpana si mrefu; alinambia ana mawaa mawili kama ngawa, na huyu ana mawaa mawili kama ngawa. Alinambia mkia wake mnene, na huyu mkia wake mnene; zile sifa zote zake alizoniambia mama yangu, hizi zote ndizo. Akarudi hatta kwa watumwa wake.

Alipofika kwa watumwa wake, akawaambia, na tule sana leo. Wakamwambia, haya bwana, tule. Wakala sana, wakala mikate, na mabumunda, na mkate wa kumimina, na ladu, wakashiba. Wakanywa maji. Akawaambia, mmekwisha? Wakamwambia, bwana, tumekwisha sisi, twakungoja wewe tu. Akawaambia, nami tayari.

Akawaambia lakini leo, akina baba, tusichukue vyombo vyetu kama safari ya kwanza. Vyombo vyetu na vyakula vyetu, na maji yetu, tuweke papa hapa, twende zetu kupigana kule. Kama tumeshinda, tupate kuja kula kulala, kesho twende kwetu, ao tukishindwa, tukimbilie hapa, tupate chakula chetu, tupate kwenda zetu upesi.

Na jua limekuwa alasiri. Akawaambia, haya shukeni, twende zetu. Wakishuka, hatta walipokoma nuss ya mlima, wale watumwa wawili wakafanya woga. Akawaambia, twendeni msiogope, ulimwenguni ni mawili, ni kuwa mzima na kufa. Bassi mwaogopa nini ninyi? [ 276 ]Wakamwambia, vema, twende zetu bwana. Wakaenda hatta wakafika chini.

Akawaambia, killa mwenyi nguo mbili, na avue nguo moja. Wakamwambia, kwa nini, bwana? Akawaambia, huku tu katika mwitu, na mwitu hauna udogo, huenda tukanaswa na miiba, ao huenda tunapopenya katika miiba, ao kama tunafukuzwa, nguo yetu ya pili itatufanya uthia, hutaweza kwenda mbio. Afathali hizi nguo moja moja, na hiyo moja tena shuti tuipige uwinda. Wakamwambia, vema, bwana. Wakapiga uwinda wote. Akawaambia, haya twendeni. Wakaenda kwa magoti hatta wakamwona yule nunda pale penyi kichaka, akalala.

Yule bwana akanena, ndiye nunda huyu. Na wale watumwa wakamwambia, ndiye, bwana. Akawaambia, sasa jua linakuchwa, tumpige, tumwache? Wakamwambia, bwana, tumpige, tujue kumpata, ao tujue tumemkosa. Akawaambia, vema, akawaambia, shikeni bunduki zenu tayari. Akawaambia, bunduki zenu nikiziamru marra moja zilie. Wakamwambia, inshallah, bwana.

Wakatambaa kwa magoti, hatta wakamkaribia alipo. Wakamwona waziwazi. Akawaambia, haya sasa na tumpige. Yule bwana, alipopiga bunduki yake, nazo za watumwa wote zikalia. Yule nunda asiinuke, bunduki zile zalimtosha. Wale wakakimbia, wakapanda juu ya mlima.

Jua limekuwa magharibi, hatta wakafika juu ya mlima, wakakaa kitako. Wakatoa mikate, na mabumunda, na ladu, na mkate wa kusonga. Wakala, wakala sana, wakashiba, wakanywa maji, wakakaa kitako. [ 278 ]Wakaulizana, Je! nyama yule tumempata? Killa mtu akanena, tumempata, bwana. Bassi natulale, hatta ussubui tutazame.

Wakalala hatta ussubui, wakapika wali, wakala, wakanywa maji. Wakaenda, wakazunguka kule nyuma ya mlima. Wakamkuta yule nunda amekufa. Wakashuka hatta wakafika chini, wakamtazama amekufa. Yule mtoto akafurahi sana, na wale watumwa wake wakafurahi. Akawaambia, naona njaa, pikeni tena, tule. Wakatoa mchele, wakapika wali. Wakapika wali mwingi, wakala wali hatta mwingine wakamwaga.

Akawaambia mfungeni, haya, tumkokote. Wakamkokota siku ya kwanza, msitu na nyika, siku ya pili, msitu na nyika, siku ya tatu, msitu na nyika, siku ya nne, nyama tena ananuka. Wale watumwa wake wakamwambia, yule ananuka na tumwache. Akawaambia, huyu tutamkokota hatta utakaposalia mfupa mmoja, tukaende nao kwetu. Hatta alipokoma nuss ya njia, akaimba mtoto,

Mama wee, niulaga
Nunda mla watu. (Marra kumi na mbili.)

Akaenda hatta alipokaribia karibu na mji,

Mwanangu, si yeye
Nunda mla watu. (Marra tano.)

Mama, mama, mama,
Nilawa kumakoikoi, nimbe.
Mama, mama, mama,
Nilawa kumakoikoi, nimbe.
Kumakoikoi, nimbe,
Mama wee, niulaga
Nunda mla watu. (Marra nyingi.)

Mwanangu, ndiyeye
Nunda mla watu. (Marra nyingi hwa kujibiana.)

[ 280 ]Watu wote wa mjini wakakimbizana kuenenda, wakamkuta yule kijana, anakwimba,

Mama ni lawa kumakoikoi,
Nimbe we mama.
Nilawa kumakoikoi, nimbe we.
Mama wee, niulaga
Nunda mla watu.

Mwanangu, ndi yeye
Nunda mla watu.

Babaye aliposikia mwanawe amekuja, ame'mua nunda, akamwona hakuna mtoto bora katika mwango wake zayidi ya yule. Watu wote walio katika mji, wangwana kwa watumwa, wake kwa waume, wadogo kwa wakubwa, wakaenda kumpukusa. Akapata mali sana, akapendeza sana katika mji, babaye akampenda sana.

Siku ya tatu kuja baba yake akashuka katika enzi, akampa mwanawe. Akamwambia, mimi na mamayo, tupe chakula chetu na nguo, hatutaki illa zayidi, kwani tumekuonea, ndiye kijana mwenyi akili, taabu iliokupata, na mashaka yote, jua lako, mvua yako, kiza chako katika mwitu, watu wakakwambia utakufa, wallakini umerudi mwanangu, bassi mimi pukusa zangu mimi na mamayo, tumekupa hii inchi yako, ndio pukusa zako, mwanangu. Nawe sinene nakukomaza niwie rathi, mwanangu.

Akaamria yule nunda, akachukuliwa, akaenda akatiwa shimoni, akafukiwa sana. Akajenga nyumba juu ya shimo la nunda. Aka'mweka asikari, akamwambia, Killa atakaopita hapa katika njia hii, atoe ada, aweke, na asipotoa [ 282 ]u'mue. Bass killa apitaye pale akatoa ada, na yule kijana akakaa na mamaye sana, akakaa na babaye sana.

Baba akapatikana na farathi, akafa, yule mamaye akafanya hathari, nisije nikafa kabla sijamwoza mwanangu. Akamtafutia mwanamke mwanawe, kwa juhudi, mke jamaa yake, mzuri, kijana. Akaoa, akaingia nyumbani, akakaa sana na mkewe, akakaa sana na watu katika mji, na watu wakampenda.

Mamaye akapatikana na farathi, akafa. Akakaa msiba wa mamaye, hatta akatoka, walipokwisha toka msiba, akawaita wale nduguze watatu waanaume; akawaambia, ndugu zangu, nipeni shauri, baba amekufa, na mama amekufa, na hii enzi baba amenipa mimi kabla hajafa.

Wakamwambia baba yetu amekupa enzi, baba yetu kukupa kwako tama, hairudi. Wakamwambia, bassi sasa ndugu yetu wewe, sisi nduguzo tupatie chakula na nguo za kuvaa, hatutaki kitu zayidi, nasi tuko chini yako, lilo utwambialo ndilo tutakalotenda.

Akawaambia, ndugu yangu mkubwa kuwa ndio waziri, na wewe wa kati uwe ndio akida, na wewe wa mwisho ndio karani wangu.

Wakakaa kitako, yeye na nduguze, kwa mashauri mema. Killa mtu akamwoza mke, wakakaa na wake wao, wakakaa na mji wao. Killa mtu akazaa na watoto wao, wakapatana mashauri kama watu wapatanavyo.

Hii ndio hadithi alioifanya Chuma, kumfanyizia Sultani Majnuni, na huu ndio mwisho wa hadithi. Ikiwa njema, njema yetu wote, na ikiwa mbaya, mbaya yangu mimi pekeyangu, nalioifanya.