Page:Swahili tales.djvu/284

From Wikisource
Jump to navigation Jump to search
This page has been proofread.
264
SULTANI MAJINUNI.

mtu kwako wa kunipa chakula na nguo tu. Nawe usiende mwituni, mwanangu. Akawaambia, kua heri, baba, naenda, haya yako siyasikii.

Akaenda msitu na nyika, akaenda akamkuta ndovu amelala athuuri katika kichaka. Akawaambia watumwa wake, leo tumemwona nunda. Wakamwambia, vema, bwana, yu wapi? Akawaambia, yule katika kichaka, mtazameni sana. Wakamwambia, bassi bwana, hatumjongelei pale alipo? Akawaambia, tukimjongelea uso wake, kama anatazama huku tunakokuja sisi, hatatujia? Na akitujia atatuua sote. Lakini sasa na tufanye shauri tumtoe mtu mmoja akamtazame uso wake umelekea wapi, uje atwambie. Wakamwambia, vema, shauri jema bwana, na sisi bunduki ziwe tayari.

Akatoka mtwana wake mmoja, jina lake Kiroboto, akitambaa kwa magoti katika mwitu, hatta akakaribia alipo. Akamwona amelala, na uso umelekea upande mwingine.

Akirudi kwa magoti vilevile, hatta akafika alipo bwana wake. Je! tupe khabari. Akamwambia, habari njema, bwana. Akamwambia, yeye ndiye nunda? Akamwambia, miye, bwana, simjui, lakini huyu ndiye nunda bwana hana shaka; mpana, kitwa kikubwa, mashikio yake, nimeyaona bwana mkubwa sana. Akamwambia, ndiye bwana nunda.

Haya, na tule bassi, tupate kumwendea, wakatoa mabumunda, wakatoa na ladu, wakatoa na mkate wa kumimina, wakala; wakala sana, hatta wakashiba.