Page:Swahili tales.djvu/296

From Wikisource
Jump to navigation Jump to search
This page has been proofread.
276
SULTANI MAJINUNI.

mwambia, vema, twende zetu bwana. Wakaenda hatta wakafika chini.

Akawaambia, killa mwenyi nguo mbili, na avue nguo moja. Wakamwambia, kwa nini, bwana? Akawaambia, huku tu katika mwitu, na mwitu hauna udogo, huenda tukanaswa na miiba, ao huenda tunapopenya katika miiba, ao kama tunafukuzwa, nguo yetu ya pili itatufanya uthia, hutaweza kwenda mbio. Afathali hizi nguo moja moja, na hiyo moja tena shuti tuipige uwinda. Wakamwambia, vema, bwana. Wakapiga uwinda wote. Akawaambia, haya twendeni. Wakaenda kwa magoti hatta wakamwona yule nunda pale penyi kichaka, akalala.

Yule bwana akanena, ndiye nunda huyu. Na wale watumwa wakamwambia, ndiye, bwana. Akawaambia, sasa jua linakuchwa, tumpige, tumwache? Wakamwambia, bwana, tumpige, tujue kumpata, ao tujue tumemkosa. Akawaambia, vema, akawaambia, shikeni bunduki zenu tayari. Akawaambia, bunduki zenu nikiziamru marra moja zilie. Wakamwambia, inshallah, bwana.

Wakatambaa kwa magoti, hatta wakamkaribia alipo. Wakamwona waziwazi. Akawaambia, haya sasa na tumpige. Yule bwana, alipopiga bunduki yake, nazo za watumwa wote zikalia. Yule nunda asiinuke, bunduki zile zalimtosha. Wale wakakimbia, wakapanda juu ya mlima.

Jua limekuwa magharibi, hatta wakafika juu ya mlima, wakakaa kitako. Wakatoa mikate, na mabumunda, na ladu, na mkate wa kusonga. Wakala, wakala sana, wakashiba, wakanywa maji, wakakaa kitako.