Swahili Tales/Mwalimu Goso

From Wikisource
Jump to navigation Jump to search
Swahili Tales  (1870)  by Edward Steere
Mwalimu Goso
English translation: Goso the Teacher
[ 286 ]

MWALIMU GOSO.


Palikuwa na mwalimu akisomesha watoto, tini ya 'mbuyu, jina lake huyu mwalimu yuwaita Goso. Hatta siku moja akaja paa, akakwea juu ya ule 'mbuyu, akaangusha buyu, likampiga yule mwalimu, akafa. Wale waanafunzi wakamtwaa mwalimu wao, wakaenenda, wakamzika.

Walipokwisha mzika, wakanena, Na twenende, tukamtafuta huyu aliyeangusha buyu, likampiga mwalimu wetu Goso, nasi tukimpata, tu'mue.

Kisha wakanena, Aliyeangusha buyu ni kusi, ilivuma ikaangusha buyu, likampiga mwalimu wetu, na twenende tukaitafute kusi, tuipige.

Wakaitwaa kusi wakaipiga. Ile kusi ikanena, mimi kusi, mwanipiga, nimefanya nini? Wakamwambia, Wewe kusi ndiwe uliyeangusha buyu, likampiga mwalimu wetu Goso, si mtende. Ile kusi ikanena, kwamba mimi ni bora, ningalizuiwa ni kiyambaza?

Wakaenenda wakatwaa kiyambaza, wakakipiga. Kile kiyambaza kikanena, mimi mwanipiga, nimefanya nini? Wakamwambia, Wewe kiyambaza mzuia kusi, na kusi [ 288 ]ikaangusha buyu, likampiga mwalimu wetu Goso, si mtende. Kiyambaza kikanena, kwamba mimi ni bora, ningalizuliwa ni panya?

Wakaenenda wakanitwaa panya, wakampiga. Yule panya akanena, mwanipiga, nimefanya nini? Wakamwambia, wewe panya mzua kiyambaza, na kiyambaza mzuia kusi, na kusi ikaangusha buyu, likampiga mwalimu wetu Goso, si mtende. Yule panya akanena, kwamba mimi ni bora, ningaliliwa ni paka?

Wakaenenda wakamtafuta paka, wakamtwaa, wakampiga. Yule paka akanena, mimi mwanipiga, nimefanya nini? Wakamwambia, wewe paka mla panya, na panya mzua kiyambaza, na kiyambaza mzuia kusi, na kusi ikaangusha buyu, likampiga mwalimu wetu Goso, si mtende. Yule paka akanena, kwamba mimi ni bora, ningalifungwa ni kamba?

Wakaenenda, wakaitwaa kamba, wakaipiga. Ile kamba ikanena, mimi kamba mwanipiga, nimefanya nini? Wakamwambia, wewe kamba mfunga paka, na paka mla panya, na panya mzua kiyambaza, na kiyambaza mzuia kusi, na kusi ikaangusha buyu, likampiga mwalimu wetu Goso, si mtende. Ile kamba ikanena, kwamba mimi bora, ningalikatwa ni kisu?

Wakaenenda, wakatwaa kisu, wakakipiga. Kile kisu kikanena, mimi mwanipiga, nimefanya nini? Wakamwambia, wewe kisu mkata kamba, na kamba mfunga paka, na paka mla panya, na panya mzua kiyambaza, na kiyambaza mzuia kusi, na kusi ikaangusha buyu, likampiga [ 290 ]mwalimu wetu Goso, si mtende. Kile kisu kikanena, kwamba mimi ni bora, ningaliliwa ni moto?

Wakaenenda wakautwaa moto, wakaupiga. Ule moto ukanena, mimi mwanipiga, nimefanya nini? Wakamwambia, Wewe moto mla kisu, na kisu mkata kamba, na kamba mfunga paka, na paka mla panya, na panya mzua kiyambaza, na kiyambaza mzuia kusi, na kusi ikaangusha buyu, likampiga mwalimu wetu Goso, si mtende. Ule moto ukanena, kwamba mimi ni bora, ningalizimwa na maji?

Wakaenenda wakayatwaa maji, wakayapiga. Yale maji yakanena, mimi mwanipiga, nimefanya nini? Wakamwambia, Wewe maji mzima moto, na moto mla kisu, na kisu mkata kamba, na kamba mfunga paka, na paka mla panya, na panya mzua kiyambaza, na kiyambaza mzuia kusi, na kusi ikaangusha buyu, likampiga mwalimu wetu Goso, si mtende. Yale maji yakanena, mimi kwamba ni bora, ningalinwiwa ni ng'ombe?

Wakaenenda, wakamtwaa ng'ombe, wakampiga. Yule ng'ombe akanena, Mimi mwanipiga, nimefanya nini? Wakamwambia, Wewe ng'ombe, mnwa maji, na maji mzima moto, na moto mla kisu, na kisu mkata kamba, na kamba mfumga paka, na paka mla panya, na panya mzua kiyambaza, na kiyambaza mzuia kusi, na kusi ikaangusha buyu, likampiga mwalimu wetu Goso, si mtende. Yule ng'ombe akanena, kwamba mimi ng'ombe ni bora, ningaligandamwa ni kupe?

Wakaenenda wakamtwaa kupe, wakampiga. Yule kupe akanena, Mimi mwanipiga, nimefanya nini? [ 292 ]Wakamwambia, Wewe kupe mgandama ng'ombe, na ng'ombe mnwa maji, na maji mzima moto, na moto mla kisu, na kisu mkata kamba, na kamba mfunga paka, na paka mla panya, na panya mzua kiyambaza, na kiyambaza mzuia kusi, na kusi ikaangusha buyu, likampiga mwalimu wetu Goso, si mtende. Yule kupe akanena, kwamba mimi ni bora ningaliliwa ni paa?

Wakaenenda wakamtafuta paa, walipomwona wakamtwaa wakampiga. Yule paa akanena, mimi paa, mwanipiga, nimefanya nini? Wakamwambia, Wewe paa, mla kupe, na kupe mgandama ng'ombe, na ng'ombe mnwa maji, na maji mzima moto, na moto mla kisu, na kisu mkata kamba, na kamba mfunga paka, na paka mla panya, na panya mzua kiyambaza, na kiyambaza mzuia kusi, na kusi ikaangusha buyu, likampiga mwalimu wetu Goso, si mtende.

Yule paa asinene neno, akanyamaza. Wakanena, Huyu ndiye aliyeangusha buyu likampiga mwalimu wetu Goso, naswi na tuta'mua. Wakamtwaa yule paa, nao waka'mua.