Swahili Tales/Hekaya ya Mohammadi Mtepetevu

From Wikisource
Jump to navigation Jump to search
Swahili Tales  (1870)  by Edward Steere
Hekaya ya Mohammadi Mtepetevu
English translation: Mohammed the Languid
[ 150 ]

HEKAYA YA MOHAMMADI MTEPETEVU.


Yalikuwa zamani za Kalifa, Amiri al Muhminina, Haruni Rashidi, alikaa kitako katika baraza yake, na mawaziri yake. Akamwona kitwana akiingia. Akamwambia, Bibi salaamu, sitti Zubede, baada ya salaam, amefanyiza taji ya kuvaa, amepungukiwa na johari moja, bassi mtazamie johari moja, ilio kubwa. Akatazama katika makasha yake, akatafuta, asipate ilio kubwa kama atakaye.

Akamwambia, niletee ile taji, niitazame. Akamletea taji, imefanywa kwa johari tupu. Akawaambia mawaziri yake, waliokaa naye. Akawaonyesha na taji, akawaambia nataka johari itakayofaa juu ya taji.

Ikawa kulla mtu kutoka kwenda nyumbani kwake kutafuta johari, atakayo kalifa, killa mtu akatafuta asipate. Walizo nazo ndogo, hazifai juu ya taji. Akaingia mjini kwa matajiri, kutafuta johari ilio kubwa, isipatikano.

Mtu mmoja akanena, akamwambia Kalifa, Johari itakayofaa, hapa katika inchi ya Baghdadi haipatikani: [ 152 ]labuda katika inchi ya Bássara kuna mtu mmoja kijana jina lake Mohammadi mtepetevu, huko itapatikana.

Kalifa akamuita waziri wake Masruri Sayafi. Akamwambia, twaa khati, usafiri wenende Bássara kwa liwali Mohammad Zabidi. Naye ndiye liwali wake, kalifa, alioko inchi ya Bássara.

Akapewa khati Masruri Sayafi, akafuatana na jeshi ilio nyingi, wakasafiri kwa njia barra, wakaenenda hatta il Bássara. Wakaingia katika inchi ya il Bássara, wakafikilia kwa liwali Mohammad Zabidi.

Akatoa khati akampa, akasoma. Alipokwisha soma, akamkaribisha nyumbani, akamfanyizia karamu ilio kubwa, wakaingia wakala chakula. Walipokwisha, akamwambia, Sina amri mimi ya kukaa kwako. Amri yangu niliopewa ya kukupa khati, ukiisha soma, twenende kwa Mohammad mtepetevu. Na sasa toka twenende. Wakatoka wakafuatana, wakaenda kwa Mohammad mtepetevu.

Waziri Masruri Sayafi akatoa khati itokayo kwa Harun Rashidi. Akapokea kwa mikono miwili, akafungua kwa adabu, akaisoma khati itokayo kwa kalifa.

Alipokwisha soma, akamwambia, Karibu nyumbani. Akamwambia, sina amri mimi ya kuingia nyumbani mwako, nimeambiwa nikupe khati, ukiisha soma tufanye safari, twenende. Kwani kalifa ameniambia, usikae, mpe khati uje zenu, mfuatane naye yule. Alipoambiwa vile akanena, sema'a wa ta'a, lakini tafáthali unywe kikombe cha kahawa. Akamwambia, sikuamriwa mimi kunywa kahawa kwako. Akamwambia, huna buddi kunywa kahawa [ 154 ]yangu. Akamnasihi, akakubali kwa nguvu, akaingia ndani ya nyumba, akapanda darini katika sébule yake. Akamkaribisha, akaingia ndani, akakaa kitako.

Alipokaa kitako akaletewa mfuko wa dinari khamsi mia. Akamwambia, tafáthali uingie katika hamami, kwani siku nyingi umetaabika kwa safari mwendo wa barra, huna buddi na kuchoka. Bassi tafáthali uingie katika hamami.

Bassi akaondoka akaingia katika hamami, na maji yake, yalio katika hamami, marashi mawáridi, ndio maji yake yaliomo. Akaingia akaoga. Wakaja na vitwana matowashi, wakaja, wakamsugua kwa vitambaa vya hariri. Alipokwisha, akatoka, akapewa nguo za kukaukia maji, na killa nguo ni nguo hariri na zari. Akakaukia maji. Alipozivua, akaletewa baksha ya nguo nyingine, nguo zayidi ya zile za kukaukia maji. Akavaa, na zile zikakunjwa, zikawekwa na ule mfuko aliopewa kwanza. Akaenda zake sebuleni akakaa kitako.

Alipokaa, akainua macho akatezama sebule, pambo lake, na matandiko yake yaliotandikwa chini. Akaona ajabu kuu, akawaza moyoni mwake, hatta chumba cha kalifa hakikupambwa kama hivi. Akaletewa maji, akanawa, yeye Masruri Sayafi, na liwali, Mohammad Zabidi, na waliopo sebuleni wote. Walipokwisha nawa wakaona vitwana wakaingia na vyakula, wakaja wakaandika, wakala. Walipokwisha kula, akawaza, vyakula vile ni vyakula ambavyo havimo katika ulimwengu.

Akapewa chumba cha kulala, Akaingia chumbani mwake, alichofanyiziwa kulala, wakaja vijakazi, wamevaa [ 156 ]lebasi njema njema, killa mmoja na kinanda, wakaingia wakapiga kinanda, wakaimba, ili kumtumbuiza, na wangine kucheza, na kutoa mashairi ya kumsifu. Akapata usingizi akalala usingizi wa mchana.

Alipoamka watu wamekaa tayari mlangoni, kumngoja kwenda naye katika hamami. Akaenda katika hamami, akavua nguo, zikakunjwa zikawekwa pamoja na zile za kwanza. Akaingia katika hamami, na hali ile ile ya kwanza na ziyada. Bassi alipotoka katika hamami, akapewa nguo za kukaukia maji. Alipokwisha kukaukia maji, akavua na nguo hizi za hariri na zari. Akaletewa nguo nyingine ya kutokea sebuleni, na killa nguo methmini. Akavaa, akatokea nje.

Akitoka, chakula tayari, wakaingia, wakala chakula. Wakaisha wakajizumgumza hatta usiku ukaingia, akatandikiwa chumba kingine. Akaenda kulala. Akitezama chumba chile, pambo lake liliomo, na samani zake, chapita chumba alicholala mchana. Akalala hatta assubui.

Akaamka, wakaja watu wakamtwaa, wakaenda naye katika hamami. Akitoka akapewa nguo nyingine za kukaukia maji, akaisha akaletewa nguo nyingine, akavaa. Na zile alizovaa kwanza zikakunjwa, zikawekwa, na killa anapoletewa nguo, huletewa na mfuko wa dinari khamsi mia.

Akatoka nje akaenda akala chakula. Walipokwisha kula, akamwambia Mohammad mtepetevu, Mimi sina ithini ya kukaa siku mbili, na leo siku ya pili hii, bassi fanya safari twende zetu.

[ 158 ]Akamwambia, ningoje siku ya leo ishi kwani nataka bághala wa kupakia zawadi zangu nitakazo kumpelekea kalifa. Akamwambia, nimekupa ruksa ya leo. Akafanya shughuli zake, mchana kutwa. Siku ile ikawa kustarehe hatta jua likachwa. Akaingia katika hamami waziri yule Masruri Sayafi. Alipotoka akapelekewa kama zile za kwanza akavaa. Na killa nguo anazovua hukunjwa zikatiwa ndani ya kasha na mfuko wa dinari khamsi mia. Na nguo hizo na fetha hizo zake mwenyewe Masruri Sayafi.

Wakakaa hatta assubui wakafanya safari yao. Wakaletwa bághala ároba mia, mabághala hao kupakia haja zake Mohammadi mtepetevu. Wakapakia, akaamrisha kutandikiwa bághala wake wawili, kwa seruji ya thahabu, na lijamu zake za thahabu, na vigwe vyake vya hariri. Mmoja akapanda yule mwenyewe Mohammadi mtepetevu, na mmoja akapanda yule waziri Masruri Sayafi. Na liwali Mohammadi Zabidi, wakaingia katika safari, kusafiri kwenenda kwa Kalifa, inchi ya Baghdadi. Wakasafiri jeshi kuu. Wakaenda njiani.

Jua likichwa wakafanya khema zao, wakalala. Na khema ya Mohammadi mtepetevu, khema yake hariri, na miti yake ya uudi, wakalala, yeye na waziri Masruri Sayafi.

Assubui wakaamka wakatoa vyakula vyao na vinywa vyao, wakala wakinywa. Wakaisha wakatandikwa nyama zao, wakapanda. Ikawa hali hiyo, jua likichwa wakalala, na usiku ukicha wakaenenda. Na katika safari mle, yule waziri Masruri Sayafi akawaza ndani ya moyo wake, akanena, Mimi nitakapofika kwa Kalifa nitamwambia, amuulize sababu yake ya kupatia mali mengi hivi. Nami namfahamu babaye, alikuwa muumishi katika hamami.

[ 160 ]Wakaenda wakafika kwa Khalifa, wakatoa salamu mbele yake Khalifa. Naye Khalifa amekaa, na mawaziri wake pale. Akamkaribisha. Akaanguka chini ya miguu yake Khalifa yule mtepetevu. Akamwambia, nataka msamaha kwako, nna maneno nataka kwambia. Akamwambia, sema. Bassi akainua uso wake, akatazama juu. Akatikiza midomo yake, zikapasuka juu ya nyumba, yakatoka kama majumba, na bustani, na miti ndani ya bustani, na miti ile majani yake ya lulu, na matunda yake ya marijani.

Khalifa akastaajabu mno. Akamwuliza, Mali haya umepata wapi wee? Nawe hatukufahamu ela Mohammadi mtepetevu, na baba yako alikuwa muumishi katika hamami. Bassi ilikuwaje hatta ukapata mambo haya weye? Akamjibu, akamwambia, ukiniamuru ntakupa hadithi yangu. Na haya pia sikukuletea kwa kuogopa, lakini nimetazama haya hayafai ela kwako weye mfalme. Bassi kama wataka nikupe hadithi yangu, ntakwambia. Mfalme akampa amri, akamwambia, lete hadithi yako.

Akamwambia, zamani za kwanza nilipokuwa mdogo, na baba yangu alipokufa, nilikuwa mvivu sana, hatta chakula akinilisha mama yangu. Na nijapolala, siwezi kugeuka ubavu wa pili, sharti aje mama anigeuze. Ikawa mama akienda kuomba, akipata kitu akinilisha. Nikakaa hali hiyo miaka khamstashara katika uvivu.

Hatta siku moja akaenda mama, akaenda akaomba, akapata dirhamu tano, akinijia kule nyumbani kwangu nilipolala, akanambia, leo nimekwenda omba, nimepata hizi dirhamu tano, bassi, twaa hizi dirhamu tano umpelekee Sheikh Abalmathfár. Naye Sheikh anasafiri, [ 162 ]anakwenda katika inchi ya Sini. Bassi twaa dirhamu tano hizi umpelekee, labuda huko aendako, atakununulia bithaa, uje upate fayida hapa, kwani Sheikh ni mtu mmoja mtaowa, apenda maskini, bassi ondoka ukampelekee hizi dirhamu tano. Nikamjibu, mamangu, kwenda siwezi, wala usiniambie tena maneno haya. Akaniambia, kana hutaki kwenda, bassi nami nitakutupa, sikupi chakula, wala sikupi maji. Wala ukilala juani, sikuondoi, nitakuacha kufa njaa yako. Akaniapia na kiapo. Nikaona tena utakufa mimi.

Nikamwambia kama huna buddi, nisogezee vyatu vyangu. Akanisogezea, nikamwambia, nivike miguuni, akanivika. Nikamwambia, nipe na kanzu yangu, akaniletea. Nikamwambia, nivike. Akanipa na nguo ya kujitanda. Nikamwambia nipe na gongo langu mkongojo, nipate kujigongojea. Akanisogezea. Nikamwambia, niondoe bassi, nisimame, akaniondoa. Nikamwambia, kaa kwa nyuma ukanisukuma, nipate kwenenda. Bassi ikawa hali hiyo, akinisukuma, hiinua mguu moja, hatta tukafika pwani. Tukamtafuta Sheikh Abalmathfár. Yu katika kupakia.

Aliponiona akastaajabu, akaniambia, Vilikuwaje leo, hatta ukafika pwani huku? Nikampa dirhamu zangu tano zile, nikamwambia, amana yangu hii, nichukulie huko wendako, uninunulie bithaa, ndilo jambo nililokujia pwani. Akazipokea Sheikh Abalmathfár.

[ 164 ]Nami nikajirudia nyumbani kwangu, ikawa hali yangu ile ile, kulala na kulishwa, na kunyweshwa maji.

Sheikh akasafiri yule, akaenda zake katika inchi ya Sini. Wakafanya biashara zao hatta wakaisha. Wakasafiri, wakaenda mwendo wa siku mbili, dirhamu zangu zile akazisahao, asininunulie kitu. Akazikumbuka baada ya siku mbili. Akawaambia matajiri wenziwe, kama hatuna buddi na kurudi, amana ya Mohammadi mtepetevu nimeisahao. Wakamjibu matajiri wenziwe, wakamwambia, utarudi kwa sababu ya dirhamu tano, naswi tumepakia mali mengi ndani ya merikebu? Akawaambia kana hamtaki kurudi mkamfanyizie killa mtu kitu maalum. Wakakubali wale matajiri.

Bassi wakaja safiria wakaenda hatta wakawasili katika kisiwa. Na kisiwa kile kimekwitwa, kisiwa cha Sunudi, ndio jina lake. Wakashuka pale, ili kwenda kupumzika kwa taabu ya bahari ile. Wakatembea mjini mle.

Yule Sheikh niliyempa amana yangu, akapita mahali dukani, akaona kima wamefungwa, pana na mmoja mdogo wao amenyonyoka manyoya pia, na wale wenziwe humpiga. Bassi Sheikh alipomwona, akamwonea huruma, akamtaka kwa mwenyewe, akamnunulia kwa dirhamu zangu tano. Naye Sheikh nia yake kuniletea kuchezea, kwani amenijua ni mtu sina kazi.

Wakasafiri wakaja zao hatta kisiwa cha pili. Kisiwa kile kinakwitwa kisiwa cha Sodani, kwani wenyewe na watu wenzi wao hula nyama za waana Adamu. Walipoona merikebu imefika pale, wakaipandia wakaenda wakawafunga watu waliomo pia wote, wangine wakachinja, wakala [ 166 ]nyama zao. Akasalia Sheikh Abalmathfár na jamaa zake watu wawili, na nuss ya baharia. Wakafungwa, ili kuchinjwa assubui.

Hatta ilipofika usiku akaondoka yule kima, akafungua yeye kwanza, akaisha akafungua Sheikh Abalmathfár, akaisha akafungua na wale jamaa waliosalia, hatta akawaisha pia yote. Sheikh alipoona wamefunguliwa, wakakimbia wakaenda zao merikebuni kwao wakaiona bado mzima, haijavunjika, wakatweka, wakakimbia. Wakaenda katika bahari kule katika kuja zao.

Na watu katika merikebu mle huzamia lulu. Alipoona kima yule watu wanazimia lulu, naye akajitosa pamoja nao. Sheikh akasema, nimekwisha potea kwa bakhti ya yule maskini ya Muungu. Hatta zamani waliporejea watu, naye akarejea nao. Amechukua na lulu, na lulu zake njema kuliko za watu. Akamtupia bwana wake miguuni pake.

Bassi akawaambia jamaa wale, kama sisi hatungepona ela kwa sababu ya kima huyu, bassi killa mtu na atoe dinari thenashara mia, tumpelekee bwana wake, killa mtu dia ya roho yake. Wakatoa, akazikusanya Sheikh Abalmathfár, akatanganya na lulu zile alizopata kima. Na fayida ya dirhamu tano zangu akatia ndani ya makasha akafunga, akaandika alama ya Mohammadi mtepetevu.

Bassi wakasafiri hatta wakafika inchi ya Bássara, wakapiga mizinga, wakashuka.

Mama yangu akasikia kama Sheikh Abalmathfár amekuja, akaja akaniambia, toka wenende ukamtazame Sheikh Abalmathfár, ukampe mkono wa salama. Nikamwambia, siwezi kwenda, njoo niondoe. Akaniondoa, [ 168 ]akanivika viatu vyangu na nguo zangu. Bassi nikamwambia, nipe fimbo yangu, akanipa fimbo yangu. Nikamwambia, kaa nyuma ukanisukume. Akakaa nyuma akanisukuma, nikainua mguu moja, akanisukuma, nikainua mguu moja, hatta tukafika.

Nikaonana naye nikampa mkono. Akaniuliza hali, akaisha akaniambia, amana yako itakuwasilia nyumbani. Tulipokwisha onana, tukatoka, na mama yangu akanisukuma, hatta nikafika nyumbani kwetu. Nikafika, nikarejea mahali pangu, nikalala.

Kitambo kidogo nikaona mtu akaingia, akaja akinipa kima. Yule akaniambia, Salaam Sheikh Abalmathfár. Nikapokea kima yule, nikamwacha, akatokea yule mtu alioleta kima.

Nikamwita mama yangu, akaja, nikamwonyesha, nikamwambia, kitu kikubwa alichoniletea Sheikh Abalmathfár, hapa petu kima wanakuzwa kumi kwa dirhamu, na dirhamu tano ameniletea kima moja.

Sijadiriki kwisha kusema maneno haya na mama yangu, nikamsikia mtu, akibisha—Hodi! Nikamwambia? karibu. Akaingia na funguo, akanipa funguo zile. Naona na mahamali nyuma yake, wakaingia wanachukua makasha makubwa mno ajabu. Akaniambia, hizi funguo za makasha haya. Nikamwuliza, makasha haya ya nini kuniletea mimi? Akaniambia, hii ndio amana yako uliompa kwenda kukununulia bithaa.

Nikamwambia, hana haja Sheikh Abalmathfár ya kunithihaki, mimi maskini ya Muungu. Mimi kijana mbele zake, na yeye mtu mzima mbele yangu. Hana haja [ 170 ]ya kunithihaki. Ni kitu gani nilichompa hatta kuniletea makasha haya? Mimi nalimpa dirliamu tano, na thamani ya dirhamu tano ni huyu kima alioniletea. Bassi, hana haja ya kunifanya thihaka, mimi maskini ya Muungu.

Na yule aliopeleka amana ile, makasha, akaniambia, hakuthihaki, walaye, si mtu wa kukufanyizia thihaka. Na yee mwenyewe atakuja sasa hivi.

Tusijaisha kusema maneno yale, marra nasikia—hodi! Nikimtazama, ni Sheikh Abalmathfár nikaondoka mwenyewe nikakaa kitako, nikamkaribisha.

Akakaa kitako akanieleza khabari yake, toka mwanzo hatta mwisho iliowapata tangu kusafiri kwao. Akaniambia, na haya makasha ndiyo fayida yako, na viliomo ndani; na huyu kima, ndio ras il mali yako. Akanitaka rathi sana, akaniambia, mimi si mtu wa kukufanyizia thihaka wewe. Tukaagana, akatoka akaenda zake.

Tukafungua kasha, tukatazama tukaona mali mengi. Mama yangu akaniambia, walikuwa mvivu, hukuona kitu na sasa Mwenyi ezi Muungu amekupa kheri. Bassi ondoka ukatafute nyumba ilio njema, ukae. Bassi nikaondoka nikaenda nikatafuta nyumba, nikanunua nyumba ilio njema, nikanunua na pambo la nyumba, nikanunua na watumwa wa nyumba, vijakazi, na wazalia, na Habashi, nikatia katika nyumba yangu. Na killa kilichoihtajia nyumba, nikanunua nikatia. Nikanunua na bithaa, nikafanya duka.

Na mimi mwenyewe hukaa dukani, na nyani wangu hukaa nami pamoja. Hatta assubui nyani akaondoka, akaenda, harudi illa jioni, na anapokuja huchukua mfuko [ 172 ]katika kinwa chake, akaja hatta nilipo, akaniwekea mbele yangu, nikaushika mfuko ule nikaufungua, nikatazama ndani mna thahabu, nikazimimina thahabu ile mashkhas, nikahasibu khamsi mia, nikazitoa nikaziweka, nikakaa hatta subui. Zamani nilipokula akaja hula sote, nikakaa hali hiyo, hutoka assubui, hukarudi akatoa mfuko mashkhas. Hatta siku nyingi zikapita.

Hatta siku hiyo usiku, nimelala katika órafa yangu, yule nyani akanijilia, akampa salamu, nikamwitikia. Lakini moyo wangu nimefazaika, nikafanya khofu sana, kwa sababu kuona nyani kusema. Akaniambia, Mohammadi, usifanye khofu, mimi, Mwenyi ezi Muungu amenijalia kuwa nyani, lakini si nyani mimi, mimi ni Jini il Maradi. Mwenyi ezi Muungu amenijalia kuwa iftahi yako, kukutoa katika umaskini, nawe usifanye khofu. Nna maneno nataka kukwambia. Wewe walikuwa mtu mmoja fukara, huna mbele huna nyuma. Mwenyi ezi Muungu amefanya mimi kunigeuza kuwa nyani kwa ndio sababu yako, ya kupatia mali. Na sasa ulionayo hayajawa mali, kwani huna mke. Bassi nimekupatia manamke, nataka nikuoze, na ukipata mke huyu, utastarehe nafsi yako, na mali utapata zayidi.

Nikamwuliza, ni yupi mke huyo? Akaniambia, kesho assubui fanya uzuri, uvae nguo borabora, na bághala yako utandike matandiko ya thahabu, ufuatane na vitwana walio wema miongoni mwa watumwa wako, uenende hatta soko il aláf. Wenende hatta baraza ya fullani, utamwona Sherifu amevaa nguo za kitaowa. Bassi mkaribia huyu, mpe salamu, mweleza khabari yako ya kutaka mke, ya [ 174 ]kuja kuposa binti yake. Atakwambia, huna ásili wala fásili. Mwambia, ásili ni dinari elfu, na fásili dinari elfu. Bassi ukamwambie na kulla utakalo, na ukiisha mpa ásili na fásili, atakubali, lakini atakuihtajia mali mengi. Atakachotaka cho chote mpe, wala usione choyo, na ukiisha oa, mali yako hayo utakayoyatoa utajilipa na zayidi. Tukaagana nikalala.

Hatta kulipokucha nikafanya kama alioniambia. Nikafanya uzuri mimi, na watumwa wangu, na bághala yangu, nikapanda, nikaenenda hatta katika soko ile, nikaenda nikamwona Sherifu, nikampa salaam, akaniitikia. Nikamwambia, jongolea, nikamweleza khabari yangu, akanijibu maneno kama yale aliyonena nyani. Akanambia, huna ásili wala huna fásili. Nikampa dinari elfain, elfu za ásili, na elfu za fásili. Akakubali, akanipa shuruti zake.

Akaniambia, dinari elfu mahari, na dinari elfu nguo, na dinari elfu kilemba changu. Nikampa dinari khamsi elafu, nikatoa na dinari elfu, nikawapa waliohuthuria, nikaoa. Nilipokwisha oa nikaenda nikamwambia nyani kama nimekwisha kuoa.

Akaniambia ulimwengu wako utakufanikia, bassi katake saa ya kuingilia nyumbani, nina khabari nataka kuja kukupa. Nikaenda nikataka saa ya kuingilia nyumbani, nikaisha nikamwambia, nimepata.

Bassi akaniambia, usiku utakayoingia nyumbani ukipita mlango wa kwanza, tezama katika behewa, utaona mlango upande wa shoto, pana na pete katika mlango ule, katika [ 176 ]pete mno ufunguo, fungua uingie ndani, utaona sanduku kubwa limejaa katika ghala, juu ya sanduku pana sufuria, na juu ya sufuria pana tassa, na ndani ya tassa mna maji, na mkono wa kushoto wako pana jogoo mwekundu, na mkono wa kulia wako pana kisu kimeandikwa talássim. Bassi twaa kisu kile, unchinje jogoo juu ya sanduku, ukaisha kumchinja utoe maji yale ndani ya tassa ile, uoshee kisu. Bassi ukaisha fanya amri hiyo, utaona sanduku itafunguka, na ndani ya sanduku utaona khazina, na khazina hiyo mwenyewe haijui Sherifu, nawe ukiisha ipata utastarehe. Kwani mimi Mwenyi ezi Muungu amenifanya nyani kuja kuwa iftahi yako. Nawe utastarehe nafsi yako, nami ntakwenda zangu. Lakini sharti ufanyize kama kayo, na usipofanyiza, hutaona mema illa utaona mabaya tu.

Nikamwambia, nitafanya kama haya uliyoniambia.

Nikaenda nikaingia nyumbani kama aliyoniagiza kufanya, nikafanya. Katika kufungua mlango kule nikamsikia yule kijana binti ya Sherifu, mke wangu, niliyo'moa, akanena; Amekwisha nichukua Jini. Hatta nilipokwisha ingia nilipotoka, nikaenda chumbani kwa mke wangu, hako. Jini amekwisha mchukua. Bassi nikawa hali yangu kama mtu mwenyi wazimo.

Khabari akaipata babaye Sherifu, marra akaja nyumbani, akija kwa kulia na kujipiga makonde, na kupasua nguo. Hatta akifika pale, akaniambia, haya ndio aliyoyataka, kwani mimi Jini nalimwona zamani kutaka kuniibia mwanangu, nikamfunga kwa haya matalassimu, uliokuja kuyafungua. Nayo yale ni madawa yaliomfunga hatta geuka nyani. Na wewe umekuja umemfungua, kunipotezea mwanangu. Bassi na sasa ni kheiri uniondokee [ 178 ]machoni pangu, kwani mwanangu nimempenda, namwonea uchungu, bassi nisitake kukuthuru.

Aliponiambia vile, nikaona ndiyo yalio. Nikaondoka nikaenda nyumbani kwangu, nikakaa kitako nikawaza, nikatafakari, nikaona nyumba hainiweki, nikatoka kwenda mtafuta mke wangu. Nikaenda wala sijui niende api. Nikalemea njia, nikafuata msitu.

Nikaona nyoka wawili mweupe na mweusi. Na mweusi yule akaja na kinwa wazi anamfukuza yule mweupe. Nikaondoka mimi, nikampiga nyoka mweusi, nikamwua. Yule mweupe akatoka akaenda zake. Akaenda nikamwona akirejea na nyoka watatu weupe kana yeye. Wakamshika yule nyoka mweusi, wakamkatakata vypande vidogo vidogo, wakaisha wakavitupa. Wakaniambia, jamala yako haipotei.

Wakaniuliza, weye siye Mohammadi mtepetevu? Nikawaambia, mimi ndiye mtepetevu? Wakaniambia tena, jamala yako haipotei, nawe twalijua liliokutoa kwenu. Sababu ni mwanamke binti Sherifu, naye mwanamke huyu zamani Maridi yule akitaka kumwiba. Naye yule si nyani, ni Jini, na yale yaliokwambia yakuwa kuna khazina, si khazina, vile na vifungo alivyofungwa yeye, akageuzwa kwa nyani na Sherifu. Na sasa, wakaniambia, inshallah utampata mkeo.

Akaenda akarudi na mtu mmoja mkubwa mno ajabu. Akamwuliza, fullani wamjua? Na fullani huyu ndiye Maridi yule aliokuwa nyani. Akamwambia, namjua, na sasa amegeuka amekuwa hali yake ya kwanza na manamke amempata amemchukua aliyekuwa akimngojea. Na sasa amekwenda yuko mji wa Nuhás. Ameona ulimwengu wote hau'mweki.

[ 180 ]Bassi wamemwambia, mchukua bwana wako huyu, wende naye hatta mji wa Nuhás, aliko mkewe. Akamwambia, nasikia. Bassi wakamwambia, inama, akainama, wakanitwaa wakanipandisha juu yake. Akaniambia, huyu ni Maridi, bassi hapo ulipo juu yake usithukuru ismu ya Mwenyi ezi Muungu, kwani ukithukuru ismu ya Mwenyi ezi Muungu atayeyuka huyu, kwani huyu ni Maridi. Nikawaambia, sitathukuru.

Akaniambia, jizuia sana juu yangu. Nikajizuia sána. Alipokwisha nizuia, akaruka, akaenda juu, nami nili hali ya kuwa juu yake. Akapaa hatta tangu ulimwengu nilipokuwa, inchi nikiona hatta nisione tena, nikaliona hewa tu. Hatta tukaenda, tukasikia tusbiih za Malaika katika mbingu, naye alina na ghathabu ya kupaa.

Bassi katika kupaa kule, nikamwona mtu kijana, sura njema sana, amepiga na kilemba cha shali akhthár, amechukua na kimwondo cha moto. Akaniita kwa jina langu, Mohammadi mtepetevu! Aliponiita, nikamwitikia. Akaniambia, thukuru ismu ya Mwenyi ezi Muungu, ao usipothukuru nitakupiga kimwondo. Nikathukuru.

Kadiri ya kuthukuru, jini aliniacha, nalitoka juu ya maongo yake. Marra kijana aliponiacha, akampiga kile kimwondo alichochukua mkononi, akayeyuka kama rissás.

Bassi nikawa kujijia zangu hatta nikafika chini. Nikaanguka katika habari. Kuangukani kwangu nikaona chombo cha wavuvi. Waliponiona, wakaja wakaniokota, wakanipakia katika chombo chao. Wakanitolea samaki, wakaniokea, nikala. Nilipokwisha kula nikaona sijambo punde. Ikawa kusema nami, na ile lugha yao hatusikizani. [ 182 ]Wakanichukua, wakaenda nami hatta kwa mfalme wao. Yule mfalme wao ajua kusema Kiarabu na inchi yenyewe katika inchi za Kihindi.

Bassi yule mfalme akasema nami kwa lugha ya Kiarabu, akaniuliza khabari zangu, nitokako, nilivyokwenda, hatta nikaokotwa katika bahari. Bassi nikampa khabari zangu zilionipata. Yule mfalme akamwita waziri wakwe, akanitwaa mimi, akampa waziri wakwe, akamwambia, u'mweke kwako, ukamtenda vema hatta arudi hali. Bassi nikaenenda nikamfuata. Akaenenda akanipa nyumba njema, malalo mema, makula mema, kwa killa jambo la wema akanitenda.

Nikakaa siku nilizokaa kwake. Na katika nyumba ile naliokaa ina bustani, nikakaa siku hiyo nikafungua dirisha ile iliolekea bustani, nikatezama, ikanipendeza mno bustani ile. Nikaona mto wa maji ndani yake, nikapenda kwenda kuoga katika mto ule. Nikashuka, nikaenda nikaingia ndani ya maji, nikaoga. Bassi nikaufuata mto ule, ukanitoa mji.

Nikitahamaka, sikujua nitokako, wala nendako, nikawa kama mtu wa kupigwa na bumbuazi. Bassi marra ile, nikamwona mtu amepanda frasi, akanijongelea hatta nilipo. Akaniita kwa jina langu. Akaniambia, jamala yako haipotei. Akaniuliza, wanijua mimi? Nikamwambia, sikujui. Akaniambia, yule nyoka mweupe ndimi nduguye. Na sasa nimekuja kulikhatimisha jambo letu. Akaniita, akaniambia, njoo, tupande frasi, tukapanda wawili frasi, tukaenenda.

Akaniambia, sasa tumekaribia mji wa Nuhás. Nami sijui nitokako, wala sijui nendako. Sijui mbele, sijui nyuma, nimekuwa mtu tu. Tukaenda, tukafika pahali pana [ 184 ]jabali, na chini yake mto unapita. Bassi tukashuka pale juu ya jabali. Niliposhuka nikamtafuta, nisipomwona tena.

Bassi nikarejea hali yangu ileile ya kwanza, nikakaa kitambo kidogo hivi. Nikamsikia mtu, akanipa salaam, nikamwitikia. Akaniuliza, wanijua mimi? Nikamwambia, sikujui. Akaniambia, mimi ni nduguye nyoka mweupe, naswi watu watatu, kulla mmoja amekutendea awezalo, bassi na mimi nimekuja kukutendea niwezalo. Akaniambia, tumekaribia sasa mji wa Nuhás, tumefika, ni ile unayoiona pale.

Nikamwambia, nimeiona, nitaiingiaje kule? Akatoa upanga akanipa, akaniambia, chukua huu upanga. Na upanga ule umeandikiwa talassimu, wote. Nikaushika upanga. Nikamwuliza, njia i wapi ya kuingilia ndani? Nayo ule mji wa Nuhás, mtu mmoja hawezi kufungua mlango, wala wawili, wala watatu, na mlango wake umefungwa, nitapitia wapi mimi? Akaniambia, fuata mto wa maji, na mto huu unaingia ndani ya mji wa Nuhás.

Nikafuata mto ule na upanga wangu mimechukua mkononi. Nikafuata mto, hatta nikaingia ndani ya mji. Nikiingia, nimeona mambo ya miujiza, kulla laoni ya vitu nikaviona, nivijuavyo nisiovijua. Nikaenenda na upanga wangu mkononi, haingia katika mji, hatembea katika mji. Nami haona nao, lakini wao hawanioni, kwa sababu ya upanga wangu ilioandikiwa na talássim.

Nikazunguka hatta nikamwona manamke, mke wangu. Nilipomwona, marra nikamtambua, naye akanitambua, nikamjongelea, tukaonana tukaulizana khabari. [ 186 ]Nikamwuliza, aliyekuleta huku nani? Akaniambia, alionileta huku ni yule nyani. Ulipokwisha kufanyiza amali ile, naliona mtu akanichukua, bassi hatukukaa mahali illa huku. Na killa mahali atakapo kukaa, hapakumweka, illa huku, kwani huku mwana Adamu hana tamaa ya kufika huku. Bassi sasa amekuja aniweke huku. Naye amekwenda tembea, bassi huku haji isipokuwa kwa siku zake. Na sasa usifanye khofu wewe, maadám ya kufika huku wewe tukaonana mimi nawe, na kwetu tutakwenda.

Bassi akanieleza khabari zake. Akaniambia, amri zote za Majini ya katika mji huu wa Nuhás, amri zake, zina yeye. Naye ana amali hufanyiza za kuwafunga Majini. Nawe sasa enenda. Akaniagiza. Utaona mtaimbo, una na pete, pana na chetezo, pana na buhuri. Utwae buhuri, utie ndani ya chetezo, ufukize mtaimbo, usome na azma zake, utwae pete hii, ugonge na mtaimbo ile pete, iliomo na mtaimbo. Bassi watakutokea Majini, kulla namna, kulla mmoja kwa fazaa ya nafsi yake. Na watakapokuja, watakuambia, sisi tu watumwa wako, na amri amri yako, tuamru utakalo, tutafanyizia. Bassi wakiisha kuja, amri ni ya wewe, lile utakalo kumtenda nathari yako tena.

Na maneno haya mke wangu amenieleza. Nikaondoka, nikaenda upesi palipo mtaimbo, nikatenda kama alivyoniambia. Nalipokwisha kwa kugonga mtaimbo ule, marra naona waana wanitokea, wangine jicho moja, wangine mkono moja, wangine mguu moja, kwa kulla namna wakanitokea. Wakaniambia, neno gani utakalo, sisi watumwa wako, na amri ni wako. Nena utakalo. Nikawaambia mimi, yuko wapi Maridi aliokuja na mke huku, ndiye aliogeuzwa nyani? Wakaniambia, hako amekwenda [ 188 ]tembea, lakini mwezi wa pili ametoka kuenda kutembea, na huu ndio wakti wake wa kuja. Nikawaambia, upesi mfungeni, mleteni. Marra ile nikamwona ameletwa mbele yangu, naye mikono nyuma. Nikamwuliza, wewe ndiye uliomchukua binti yule? Akaniambia, ni mimi. Bassi nikamwambia, kama Sherifu aliokugeuza nyani akakutupia ulimwenguni, mimi nitakutia ndani ya chupa la shaba nitakutupa baharini.

Bassi nikamtwaa yule, nikamtia ndani ya chupa la shaba. Nikamchukua kwa binti yule, tukamtupa baharini. Bassi nikawaamrisha Majini, killa kitu cha tunu, cha hedaya, kuvichukua. Na mimi na mke wangu tumekaa juu ya ulili, na mtaimbo, na chetezo, na buhuri yake, na kulla kinipendezacho. Nikawaamrisha Majini kutuchukua.

Wakatuchukua Majini hatta tukafika mji wa Bássara, wakanitia ndani ya nyumba yangu. Nikamwita mkwe wangu, Sherifu, assubui, akaja na mama yangu na jamaa zangu, na nipendao. Wakaja, tukaonana kwa furaha, kwa kusema, na kwa kucheka. Ikafanya harrusi vingine tena, tukafanya harrusi kubwa na furaha, na babaye binti yule akafuraha mno. Bass, tukakaa kitako kwa furaha, kwa kusema na kucheka.

Na haya, usinene mimi kukufanyizia kwa sababu ya kuogopa, lakini nimeona vitu hivi havinisulihi mimi, bassi nimeona ni kheri nikupe wewe, wewe Kalifa mtu mkubwa, na mimi mtu mdogo.

Kalifa akamwambia, ahsanta, nawe kaa kitako papa hapo, usiende tena Bássara. Wakatolewa watu kwenda Bássara, kwenda kuhamisha vyombo vyake. Wakaja navyo inchi ya Baghdadi, akakaa kitako raha mustarehe.