Swahili Tales/Ao rathi, ao mali

From Wikisource
Jump to navigation Jump to search
Swahili Tales  (1870)  by Edward Steere
Ao rathi, ao mali
English translation: Blessing or Property
[ 392 ]

AO RATHI, AO MALI.


Palikuwa na mtu miime na mkewe, wakaomba kwa Muungu kupata kijana, wakapata wa kwanza manamume, na wa pili manamuke. Na baba yao, kazi yake kuchanja kuni. Wakakaa hatta wanakuwa waana wazima. Baba yao akashikwa na ugonjwa. Akawaita waanawe, akawauliza, wataka rathi, ao wataka mali? Yule manamume akamwambia, nataka mali. Manamuke akamwambia, nataka rathi. Akampa rathi babaye sana. Babaye akafa.

Wakakaa matanga, hatta walipoondoka, mama yao akaugua, naye akawaita waanawe, akawaambia, wataka rathi, ao wataka mali? Mwanamume akamwambia, nataka mali. Na mwanamuke akamwambia, nataka rathi. Akampa rathi mamaye yule. Akafa mama yao.

Wakakaa matanga, hatta alipoondoka ikipata siku ya saba. Akaenda mwanamume, akamwambia nduguye mwanamuke, toa vitu vyote vya baba yangu na mama yangu. Akatoa manamuke, asimsazie kitu. Akachukua vyote.

Watu wakamwambia, huyu nduguyo mwanamuke humwachii walao kitu kidogo? Akanena, sitamwachia, [ 394 ]mimi nalitaka mali, yee akataka rathi. Akamwachia chungu na kinu, hatta chakula kidogo hakumwachia.

Wale jirani zake huja wakaazima kinu, wakatwangia, wakiisha, wakampa mchele kidogo, akapika, akala. Na wangine huja, wakaazima vyungu, wakapikia, wakiisha, wakampa naye chakula kidogo. Killa siku kazi yake ni hii.

Akatafutatafuta nyumbani mwa babaye na mamaye, asipate kitu, ela mbegu ya maboga. Akatwaa, akaenda, akapanda chini ya kisima. Ukaota mboga, ukazaa maboga mengi.

Yule nduguye hana habari, akauliza watu—chakula anapata wapi ndugu yangu? Wakamwambia, kuazima watu kinu, wakatwangia, wakampa naye chakula kidogo, na vyungu vyake kuazima watu, wakapikia, wakampa naye chakula.

Ndugu yake akaondoka, akaenda, akamnyang'anya kinu na vyungu. Amekwisha, akaamka subui akatafuta chakula hapati. Akakaahatta saa a tatu, akanena, nitakwenda kuangalia mboga wangu, umeota. Akaenda, akaona maboga mengi yamezaa. Akashukuru Muungu.

Akachuma maboga, akaenda, akauza, akapata chakula. Ikawa ndio kazi yake killa siku kuchuma, kaenda kuuza. Ikipata siku ya tatu, killa mtu, aliokula maboga yale akaona matamu mno. Killa mtu huchukua nafaka wakamwendea pale pahali pake, wakanunua. Siku nyingi zimepita, akafanya mali.

Mke wa ndugu yake akasikia habari ile, akatuma [ 396 ]mtumwa wake na nafaka kuenda kumnunulia boga. Akamwambia, yamekwisha. Alipojua mtumwa yule wa mke wa nduguye, akamwambia, twaa ile moja, mpelekee, na nafaka yako rudi nayo. Akaenda akalipika, akaona tamu mno. Siku ya pili akampeleka tena mtu. Akamwambia, hapana kabisa leo. Akaenda, akamjibu bibi yake, akakasirika mno.

Hatta mumewe alipokuja, akamwuuza, una nini mke wangu? Akamwambia, nimepeleka mtu kwa ndugu yako na nafaka yangu, kuenda kutaka maboga, hakuniletea, ameniambia, hakuna, na watu wote hununua kwake! Akamwambia mkewe, na tulale hatta kesho nitakwenda kung'oa mboga wake.

Hatta subui kukicha akaenenda kwa nduguye, akamwambia, mke wangu kuleta nafaka ukakataa kumliza boga. Akamwambia, yamekwisha, jana alileta mtu, nikampa burre. Akamwambia, mbona watu unawaliza? Akamwambia, yamekwisha, hakuna tena, hayajazaa. Ndugu yake manamume akamwambia, nitakwenda ukata mboga wako. Akamwambia, huthubutu, labuda ukate mkono wangu kwanza, ndipo mboga uukate. Ndugu yake akakamata mkono wake wa kuume, akamkata, akaenda akaukata na mboga wote pia.

Yule manamke akateleka maji ya moto, akatia mkono wake, akatia na dawa, akafunga kitambaa.

Akamnyang'anya vitu vyote, akamtoa na nyumba.

Akapotea yule nduguye ndani ya mwitu. Nduguye huyu akauza nyumba, akakusanya mali mengi, akakaa akitumia.

[ 398 ]Yule akapotea na mwitu, hatta siku ya saba akatokea mji mgine. Akapanda juu yamti mkubwa, akila matunda ya mti, usiku hulala mle mtini. Hatta siku ya pili, akatokea kijana cha mfalme anapiga ndege, yee na watu wake. Hatta saa ya sita amechoka, asema, nitakwenda pale mtini, nikapumzike, na ninyi pigeni ndege. Akakaa chini ya mti, yee na mtumwa wake.

Yule kijana manamke akalia hatta machozi yakamwangukia mtoto wa mfalme chini. Akamwambia mtumwa wake, angalia nje, hakuna mvua? Akamwambia, hakuna, bwana. Akamwambia, bassi, panda mtini uangalie ndege gani alionitia mavi. Akapanda mtumwa wake, akamwona manamke mzuri mno analia, asimwambie neno, akashuka. Akamwambia bwana wake, kuna kijana manamke mzuri mno, sikuthubutu kumwambia neno. Bwana wake akamwuliza, kwa nini? Akamwambia, nimemkuta, analia, labuda wende wewe. Akapanda bwana wake, akaenda, akamwona, akamwambia, una nini, bibi yangu, weye mtu, ao pepo? Akamwambia, mimi mtu. Akamwambia, unalilia nini? Akamwambia, nakumbuka ulimwengu, mimi ni mtu kana wewe.

Akamwambia, shuka, twende zetu kwetu. Akamwambia, kwenu wapi? Akamwambia, kwa baba yangu na mama yangu, mimi ni kijana cha mfalme. Akamwambia, umekuja fanya nini huku? Akamwambia, nimekuja kupiga ndege, mwezi hatta mwezi ndio kazi yetu, nimekuja na wenzangu wengi. Akamwambia, mimi sitaki kuonekana na mtu. Yule manamke, amemwambia kijana cha mfalme. Akamwambia, hatuonekani na mtu. Akashuka chini.

Akamtuma mtumwa wake—enenda mjini upesi, [ 400 ]ukaniletee machela. Akaenda mtumwa wake marra hiyo akarejea na machela na watu wanne, wakamchukua. Akamtia manamke, akamwambia mtumwa wake, piga bunduki, wapate kuja jamaa yote. Akapiga bunduki, wakaja watu wenzi wake, wakamwambia, una nini, kijana cha mfalme? Akamwambia, una baridi, nataka kwenda zangu mjini. Wakachukua nyama iliopata, wakaenda zao. Na kijana cha mfalme ameingia ndani ya machera, yeye na yule kijana manamke. Na wale wenziwe hawana habari.

Wakaenda hatta mjini kwao, wakafikia nyumbani kwake. Akamwambia mtu—enenda kamwambia mama na baba, nna homa leo, nataka uji upesi, waniletee. Wakafathaika mamaye na babaye, akapikiwa uji, akapelekewa.

Na babaye akaenda na mawiziri yake wakaenda kumtezama. Hatta usiku mamaye akaenda na watu wake kumtezama.

Hatta siku ya pili akatokea nje, akaenda, akamwambia mamaye na babaye, nimeokota kijana manamke nataka mnioze, walakini hana mkono moja. Wakamwambia, wa nini? Akawaambia, nataka vivyo hivyo. Na yule Sultani ampenda sana mwanawe mmoja tu, akafanya harusi, wakamwoza.

Watu wakapata habari mjini, mtoto wa Sultani ameoa kijana manamke, hana mkono moja.

Wakakaa kitako hatta mkewe akachukua mimba, akazaa mtoto manamume, wakafurahi mno wazee wake.

Yule kijana cha Sultani akasafiri, akaenda kutembea katika miji ya baba yake.

Huko nyuma akatokea yule ndugu yake manamume, hana kitu cha kutumia, anakwenda akiomba. Hatta siku moja, akasikia watu wanazumgumza—kijana cha mfalme [ 402 ]ameoa manamke, hana mkono moja. Yule nduguye manamume akauliza, amempata wapi kijana huyu mtoto wa mfalme? Wakamwambia, amemwokota mwituni. Akamjua kuwa nduguye.

Akaenda hatta kwa mfalme. Akaenda akamwambia, mtoto wako ameoa manamke hana mkono moja, ametolewa huyu katika mji wao kwa sababu mchawi, killa mume anayemwoa humwua.

Na mfalme akaenda akamwambia mkewe, wakanena, kufanya shauri gani? Nao wanampenda sana mtoto wao mmoja tu, wakasema, kumtoa mji yule. Nduguye mwanamume akawaambia, mwueni, kwani huko kwao amekatwa mkono, na hapa mwueni. "Wakamwambia, hatuwezi kumwua, tutamtoa mji. Wakaenda, wakamtoa mji, yeye na mwanawe. Akashukuru Muungu.

Akatoka, amechukua kitunga, akaenda zake, hatta mwituni, hajui anapokwenda, wala anakotoka. Akakaa kitako, akamwonyesha manawe, akitupa macho, akaona, nyoka anakuja mbio hatta karibu yake, akanena, leo nimekufa.

Nyoka akamwambia, mwana Adamu, funua kitunga chako niingie, uniponye wa jua nitakuponya wa mvua. Akafunua akaingia, akafunika. Akitezama, akaona nyoka mgine anakuja mbio, akamwambia, hakupita mwenzangu? Akamwambia, huyu anakwenda. Akapita mbio.

Yule nyoka, aliomo kitungani, akamwambia, nifunua. Akamfunua, akashukuru Muungu, akamwambia yule mwana Adamu, unakwenda wapi weye? Akamwambia, sijui ninapokwenda, ninapotea katika mwitu. Akamwambia nyoka, fuata mimi, twende kwetu. [ 404 ]Wakafuatana hatta njiani wakaona ziwa kubwa. Nyoka akamwambia, mwana Adamii, tukae tupumzike, jua kali, enenda kaoge ziwani na mtoto. Akamchukua kijana chake, akaenda kumwosha, akatumbukia, akampotea ziwani. Akamwuliza, una nini, mwana Adamu, huko? Akamwambia, mtoto wangu amepotea ndani ya maji. Akamwambia, mtafute sana. Akamtafuta saa mzima, asimwone. Akamwambia, tia mkono wa pili. Akamwambia, weye nyoka unanifanyia mzaha. Akamwuliza, kwa nini? Akamwambia, nimetia huu mzima, sikumwona, huu mbovu utafaa nini? Nyoka akamwambia, tia tu weye yote miwili. Akatia mwana Adamu, akaenda akamwona mwanawe, akamshika, akimtoa mkono wake mzima. Akamwambia, umemwona? Akamwambia, nimemwona na mkono wangu nimepata mzima. Akafurahi sana.

Akamwambia nyoka, sasa twende zetu kwa wazee wangu, nikakulipe fathali huko. Akamwambia, hii yatosha, kupata mkono wangu. Akamwambia, bado, twende wazee wangu. Wakaenda hatta walipofika, wakafurahi sana, wakampenda yule kijana manamke. Akakaa kitako, akila, na kulala, siku nyingi.

Yule mumewe akarudi kutembea. Wale wazee wake wakafanyiza makaburi mawili, moja la mkewe, na moja la mtoto wake. Na yule ndugu yako manamume amekua mtu mkubwa kwa mfalme.

Akaja mumewe kijana cha mfalme. Akauliza, mke wangu yu wapi? Wakamwambia, amekufa. Na mtoto wangu yu wapi? Wakamjibu, amekufa. Akauliza, makaburi yao yako wapi? Wakampeleka kuenda kuyaona. [ 406 ]Alipoona akalia sana. Akafanya matanga. Akashukuru Muungu.

Siku nyingi zimepita. Yule kijana mwanamke mwituni akamwambia rafiki yake nyoka, nataka kwenda zangu kwetu. Akamwambia, kamwage mama yangu na baba yangu, watakapokupa rukusa kwenda zako, wakikupa zawadi, usikubali ela pete ya baba na kijamanda cha mama.

Akaenda akawaaga, wakampa mali mengi, akakataa akawaambia, mimi mtu mmoja nitachukuaje mali haya? Wakamwambia, wataka nini? Akamwambia, weye, baba, nataka pete yako, na weye, mama, nataka kijamanda chako. Wakasikitika mno, wakamwuliza, aliokwambia nani habari hii? Akawaambia, mimi mwenyewe najua. Wakamwambia, hakuna, ni huyo nduguyo, aliokwambia.

Akatwaa pete, akampa, akamwambia, pete hii nakupa, ukitaka chakula, ukitaka nguo, ukitaka nyumba ya kulala, yambie pete, itakutolea, kwa rathi ya Muungu na mimi babayo. Na mamaye akampa kijamanda, akamwambia vile vile. Wakampa na rathi.

Akatoka, akaenda zake, hatta kule mjini kwa mumewe asifike nyumbani kwa mumewe. Akifika kiungani, akayambia pete, nataka utoe nyumba kubwa. Ikatoa nyumba, na pambo la nyumba, na watumwa. Akakaa kitako, yee na mwanawe. Na mwanawe amekuwa kijana mkubwa.

Mfalme akapata habari, kuwa nyumba kubwa kiungani, akatuma watu kuenda kutezama, wakamjibu, kweli. Akaondoka Sultani na mawaziri yake na kijana chake.

[ 408 ]Wakaenda, wakikaribia, akatezama durabini yule manamke, akamwona mumewe, na baba ya mumewe, na watu wengi, na yule nduguye yumo. Akawaambia watu, fanyeni vyakula upesi. Wakafanyiza, wakaandika meza. Wakafika, wakakaribishwa, wakaingia ndani, wakamwuliza habari. Akamwambia, njema. Akawaambia, kaleni chakula, natoka mbali mimi, mkiisha chakula, niwape habari yangu,

Wakala chakula, hatta walipokwisha, akawaambia, toka mwanzo alipozawa, yeye na nduguye manamume, hatta yakaisha yote, kama yalipokuwa. Yule kijana cha mfalme akaenda kumkamata mkewe, wakalizana sana, na waliopo wote wakalia, wakajua kuwa nduguye manamume si mwema.

Mfalme akamwuliza, tumfanyieje nduguyo mwanamume? Akamwambia, mtoeni mji tu. Akakaa na mumewe hatta hatima kwa furaha.