Swahili Tales/Pepo aliyedanganywa na mtoto wa sultani

From Wikisource
Jump to navigation Jump to search
Swahili Tales  (1870)  by Edward Steere
Pepo aliyedanganywa na mtoto wa sultani
English translation: The Spirit Who Was Cheated by the Sultan's Son

[ 380 ]

PEPO ALIYEDANGANYWA NA MTOTO WA SULTANI.


Palikuwa na Sultani akitamani kijana siku nyingi, asipate. Naye ana mali mengi na miji mingi. Akaona—nikifa, itapotea mulki huu pia kwa sababu ya kukosa mtoto.

Akaja sheitani akajifanya kama mtu, akamwambia Sultani, nikikupa dawa, ukipata mtoto, utanipa nini? Akamwambia, nitakupa nussu ya mali yangu. Akamwambia, sitakubali. Akamwambia, nitakupa miji yangu nussu. Akamwambia, sikubali. Akamwambia, wataka nini bass? Akamwambia, ukizaa watoto wawili, nipe mmoja, nawe utwas mmoja. Akamwambia, nimekubali.

Akamletea dawa, akamwambia, mpe mkewo, ale. Akampa, akala, akachukua mimba, akazaa mtoto wa kwanza manamume, na wa pili manamume, na wa tatu tena manamume.

Akaja rafiki yake yule aliompa dawa, akamwambia—haya, tugawanye. Akamwambia, bado, hawajasoma watoto hawa. Akamwambia nipe mimi nikawasomeshe, [ 382 ]akamwambia, chukua. Akaenda nao kwake. Na nyumba kubwa kwake, na killa kitu kimo ndani.

Akawasomesha hatta wakajua elimu pia, wakafanya harufi, akaisha akawapelekea baba yao. Na wale vijana mmoja hodari sana. Akamwambia babao, njoo, tugawanye watoto leo, akamwambia, gawa weye. Akagawanya yee, akatwaa wawili akaweka mbali, akatwaa na mmoja, aka'mweka mbali, akamwambia—Chagua Sultani! Sultani akatwaa wale wawili, na yule akatwaa mmoja, akaenda zake.

Akaenda kwake, akampa funguo zote, akamwambia, killa utakacho fungua. Yule kijana akakaa kitako ndani ya nyumba, na yule babaye kutoka akaenda kutembea mwezi, hatta anaporudi.

Bass, kijana akakaa kitako, hatta siku moja, akachukua ufunguo, akaenda, akafungua chumba kimoja. Akaona thahabu kana maji, akatia kidole ikashika, akaisha kufuta haitoki, akafunga kitambaa. Akaja baba yake, akamwuliza, una nini kidole? Akamwambia, nimejikata. Akakaa hatta siku ya pili, baba yake akatoka, akaenda zake kutembea.

Yule mtoto akachukua funguo zote, akaenda kufungua chumba cha kwanza, akaona mifupa ya mbuzi; akafungua cha pili, akaona mifupa ya kondoo; akafungua cha tatu, akaona ya ngombe, akafungua cha nne, akaona ya punda; akafungua cha tano, akaona ya farasi; akafungua cha sita, akaona vitwa vya watu, akafungua cha saba, akaona farasi mzima.

Akamwambia, ewe binadamu! watoka wapi? Akamwambia, mimi, baba yangu huyu. Akamwambia, kazi yake kula watu, na punda, na farasi, na ngombe, na mbuzi, na killa kitu, na sasa tumesalia mimi nawe.

[ 384 ]Akamwambia, tufanyeje? Akamwambia, njoo unifungue, akamfungua. Akamwambia, sasa fungua chumba cha mali, mimi nitameza killa kitu, na baba yako akija akaenda kuwaita watu kuja kutula, na akija, atakwambia, twendee kuni, useme mimi sijui kazi hiyo, atakwenda yeye pekeyake; akija nazo atateleka sufuria kubwa, atakwambia, chochea moto, mwambia, siwezi, atakwenda mwenyewe kuchochea moto, ataleta samli nyingi, ataitia ndani ya sufuria, hatta ikipata moto atafunga pembea, atakwambia, panda ucheze, mwambia, sijui mimi kucheza mchezo huu, panda wewe mwenyewe nikuangalie kwanza, na mimi nipate kufanyiza kana weye, akipanda yeye kukuonyesha, msukume ndani ya sufuria ya samli ya moto, uje zako mbio, na miye nitakwenda kukungoja chini ya mti huko njiani.

Farasi akakimbia, akamwacha mtoto pekeyake. Hatta alipokuja baba yake, akamwambia, kesho twendee kuni. Akamwambia, mimi sijui kazi hiyo. Akamwambia, bass, kaa kitako. Akaenda mwenyewe pekeyake, akaleta kuni nyingi. Naye amekwisha waambia watu, kesho nna karamu, njooni. Akaja akatoa sufuria akateleka, akamwambia, tia kuni, akamwambia, sijui mimi. Akamwambia, kaleta samli, akamwambia, siwezi kuichukua, sina nguvu. Akaenda mwenyewe, akaichukua, akaitia ndani ya sufuria, akatia moto. Akamwambia, chochea, akamwambia, sijui kuchochea moto.

Akamwambia, umewona mchezo wa kwetu? Akamwambia, sijauona bado. Na samli imepata moto sana. Akafunga pembea, akamwambia, panda hapa, nikuonyeshe. [ 386 ]Akamwambia, panda mwenyewe kwanza, ucheze, nami nikiona baba, nipate kucheza. Akapanda, akacheza. Akashika, akamsukuma ndani ya sufuria, akatokota pamoja na samli, akafa.

Akakimbia mtoto, akaenda hatta chini ya mti akaona farasi akaja mbio. Farasi akaja, akamkamata, aka'mweka juu ya maungo yake, akamwambia, twende zetu sasa. Wakaenda zao.

Wale wenziwe kule wakaja, wakamtafuta, hawamwoni. Na njaa inawauma sana, wakaangalia ndani ya sufuria wakaona chakula kimekwisha, wakasema, katule chakula hiki, wakaepua wakapakua, wakala. Hatta walipokwisha, wakamtafuta, hawamwoni. Wakaingia ndani ya nyumba, wakatoa vyakula pia na michele pia, wakaja wakapika, wakala, siku ya pili tena, wakaona hajaja, wakaenda zao kwao.

Huyu mtoto, yee na farasi wakaenda hatta mbali miji mingine, wakakaa mwisho wa mji. Akamwambia, hapa tukae, wakakaa, wakala chakula. Akamwambia, hapa, tujenge nyumba, wakajenga nyumba kubwa na killa kitu ndani, wakatia punda na farasi na ng'ombe na mbuzi na watumwa, wakakaa.

Hatta siku yule Sultani akasikia, akaenda, akapeleka watu, wakaenda kutezama kweli habari iko nyumba kubwa, watu waambia, kweli Sultani, ni nyumba kubwa.

Sultani akampelekea watu wake kuangalia nani huyu. Akawaambia, mimi mtu kama watu. Wakamwambia, watoka wapi? Akawaambia, natoka mjini kwetu, [ 388 ]nimekuja kutembea. Wakaenda wakamwambia mfalme, amekuja kutembea mgeni. Akawaambia, enendo mtu kesho amwambie, Sultani atakuja kukutezama. Akaenda mtu, akamwambia. Akamwambia, marahaba na aje.

Akaamrisha kufanya vyakula vingi. Hatta assubui mfalme akaenda, na watu wake, akafika nyumbani. Akamkaribisha, akapita ndani, akaona Sultani nyumba kubwa na watumwa wengi ndani. Akakaa kitako, wakazumgumza. Akamwuliza, kwa nini huji mjini kutembea? Akamwambia, mimi mgeni, sharti nipate watu wanitwae, wanipeleke mjini. Akamwambia, twende zetu, tukatembee.

Mfalme akampenda sana, wakakaa siku nyingi pale. Mfalme akamwuliza, utake mke kuoa? Akamwambia, nataka. Akamwambia, nitakuoza mwanangu. Akafanya harusi kubwa Sultani akamwoza.

Akakaa na mkewe, akazaa mtoto mmoja, wakakaa hatta hatima, yee na mkewe na mtoto wake mmoja, na frasi yake, akampenda kama roho yake.