Swahili Tales/Nyani, na simba, na nyoka

From Wikisource
Jump to navigation Jump to search
Swahili Tales  (1870)  by Edward Steere
Nyani, na simba, na nyoka
English translation: The Ape, the Lion, and the Snake
[ 424 ]

NYANI, NA SIMBA, NA NYOKA.


Hapo kale palikuwa na mji, pana mwanamke, akachukua mimba, mumewe akafa. Alipokufa mume akakaa hatima kuzaa mtoto mume. Na yule mume amali yake kutega mitego, akaguia nyama, akauza vyakula.

Hatima kufa kwake yule mwanamke akauzwa ni mtoto wakwe, mama twafa na njaa. Akamwambia yule mwana, akamwuza mamaye, mama, baba alikuwa kufanya kazi gani, akavumbua chakula? Akamwambia, babayo kevu akatega mitego akavumbua chakula. Bassi nami 'tatega mitego, nipate nyama, tupate uza, tupate chakula.

Akasinda kutwa, akakata matawi ya miti. Siku ya pili, akasinda kutwa, akakata mitego. Siku ya tatu akasinda kutwa, akapakasa ngole. Siku ya nne, akasinda kutwa, akasimika mitego. Siku ya tano, akasinda kutwa kutega mitego. Siku ya sita akaenda kuonja mitego, akanamua nyama, akawachinja, akapeleka nyama mjini, zikaenenda zikauzwa nafaka. Majumba yao yakajaa tele vyakula, wakapata nafasi ya ulimwengu.

Hatima akaenda akaonja mitego, haipati kitu. Siku ya [ 426 ]kwanza alipokwenda mitegoni, ameguiwa nyani. Akataka kuliwaga. Lile nyani likasema, Ewe bin Adamu, usiniwage, njoo ninamue katika mtego, niponya kwa mvua, nije nikuponye kwa jua. Alipokwisha namua nyani, likasema, nakupa wasia wangu bin Adamu si mwema, usimtende mema, ukifanya, kesho atakuja kufanya viovu.

Hatima akaja siku ya pili, katika kuonja mitego, ameguiwa nyoka. Akapiga mbio kuita watu mjini. Akasema nyoka, Rudi, bin Adamu, usiende mbio mjini, usiende kuniitia wakaja niua, nifae katika huu mtego, nami kesho nije nikufale, lakini bin Adamu hafanyii mema mtu.

Siku ya tatu akaenda kuonja mitego, akafika mtegoni, ameguiwa simba ni mtego. Bin Adamu yule mwenyi mtego, akamwona mzee simba akamatwa ni mtego, akapiga mbio kwenda kuita watu kuja 'mua. Simba akamwambia, La; niponya wa mvua, na nije nikuponye ya jua. Illakini alipokwisha namua katika mtego, yule simba akamwambia, Bin Adamu, umenifaa, umenitenda mema, illakini wasia wangu nakusia, Binadamu hafanyi mema. Siku ngine mtu ameguiwa ni mtego, yule mwenyi mtego akamnamua.

Hatima yule kijana kande zikamwishia katika nyumba zote, wakapatiwa ni njaa, yee na mamiye. Akamwambia mamiye, Mama nifanyie mikate saba. Alipokwisha kufanya mikate saba, akashika uta wakwe, akaingia mwituni kuwinda nyama, akapotea, mikate akaila sita, ikaisha, ukasalia mmoja.

Uliposalia ule mmoja, akaenenda hatta mwituni mwitu [ 428 ]mkuu na nyika kuu, akaenenda wakaonana na lile nyani. Yule bin Adamu akaulizwa habari ni nyani. Akamwuliza, Ewe bin Adamu, wenda api? Akamwambia kwamba nimepotea. Akamwambia, bwaga moyo hapa, mimi nikulipe leo yale mema yako uliyotendea juzi, ukanitoa katika mtego, bassi starehe uningoje hapa.

Akaenenda nyani hatta mashambani mwa watu, akaenda akaiba mapapai mabivu, akaiba na ndizi mbivu, akamchukulia yule bin Adamu, akamwambia, twaa vyakula hivi, ndizi na mapapai, akampa yule bin Adamu. Akamwambia, watakani, wataka maji? Akaenda akaiba kibuyu kya maji akampa bin Adamu akanywa, akaisha kunywa, wakaagana. Wakawaambia, kua heri, kua heri ya kuonana. Akaenda zakwe.

Alipofika kule mbele, akaenenda, wakakutana na simba. Alipokutana akamwambia simba, watoka wapi, bin Adamu? Yule bin Adamu akamwambia simba, nimepotea. Simba akamwambia, kaa kitako hapa, nikulipe yale mema yako ya juzi ulionifaa, nami nikufale, kaa hapa. Akastarehe bin Adamu, akamsaburi simba. Simba yule akaenda akakamata nyama, akamletea bin Adamu, akasema, umepotea, vyakula hivi la, nije 'lipe yale mema yako ya juzi. Akampa nyama na moto wa kuoka nyama. Akaoka nyama akala. Alipokwisha kula nyama akatawakali, akaenda zakwe bin Adamu.

Alipokwenda zakwe bin Adamu akaenda akatokea shamba, pana mwanamke shaibu la juza, akatokea mtu pale, akamwambia, huko mjini kwetu kuna mtu amehawezi, [ 430 ]kana waweza kufanya dawa, twataka ukafanye dawa. Akasema, mimi sijui kufanya dawa.

Hatta akafika njiani, aona ndoo, pana kisima kando. Asema, nende 'kanywe maji pale kisimani. Akafika kisimani, akaona pandepande ya ndoo. Akasema, nichungulie hiki kisima cha maji, nipate maji ninywe. Hatima akachungulia mle kisimani amwona nyoka mkubwa. Akamwambia, bin Adamu, nisaburi kwanza. Yule nyoka akatoka kisimani, akamwambia, bin Adamu, wenda api? Umenifahamu? Akasema, sikujui. Akamwambia, ni mimi uliyenitoa katika mtego wako, hakuambia, nitoa wa mvua, nami nije nikutoe wa jua, nawe mgeni wendako, illakini lete huwo mkoba wako nikutilie vitu vyende vyakufale nawe huko wendako. Akampa ule mkoba, akamtilia mikufu ya thahabu, na mikufu ya fetha. Akamwambia, chukua ukatumie mkoba tele.

Alipofika katika mji, ule mji aliokwenda, alipofika awali akakutana na mtu yule, aliyeguiwa ni mtego. Akampokea mkoba, akaenda nao hatta nyumbani kwakwe. Alipomwona yule mgeni mkewe, akapika uji, akasema, nampikia mgeni wetu.

Yule mwanamume aliyemtoa katika mtego akaenda hatta kwa Sultani mle katika mji, akamwambia Sultani, yule mgeni anayekuja kule kwangu, msithani kwamba bin Adamu, ndiye nyoka, akaaye kisimani, mkathani kuwa nyoka, wala si nyoka, ni yee huyule ndiye ajigeuaye nyoka. Bassi Sultani, aenende mtu akamtwae na mkoba wakwe, nimeona na mikufu ya thahabu, na mikufu ya fetha.

[ 432 ]Akaenda mtu kumtwaa yule mgeni, akaja naye na mkoba wakwe. Ukafunguliwa ule mkoba na watu tele wakashuhudia vyombo vya mwana wa Sultani, wakashuhudia tena na vyombo vya watoto wa Waziri, na watu mjini. Hatima akafungwa mikono nyuma kwa kamba.

Ile joka likatoka kisimani, likija hatta mjini. Akazunguka mji, akasimama panapo yule bin Adamu. Watu wakataharruki katika mji hatta wakasema na yule bin Adamu, wakamwambia, sema na huyu nyoka, ende zako. Nyoka yule akaja. Watu wakamfungua yule bin Adamu mikono nyuma aliofungwa. Nyoka yule akarudia kisimani kwakwe, akamwambia, Ewe bin Adamu, kadri utakapofanywa maovu, nipigia ukemi, nami 'takutokea marra.

Naye akapata heshima katika inchi. Akaulizwa, kwani wee huyu kuwa mwenyeji wako, akakufanya maovu? Akawaambia, katika nyoka, na simba, na nyani, walinambia kwamba bin Adamu hafanywi mema, ukimtenda mema bin Adamu yee hukutenda maovu, nayo ni kweli wala si uwongo. Yule mema niliomtenda naye anifanya maovu, ule wasia wa nyoka na simba na nyani ni kweli, wala si uwongo.

Sultani akauza maana yakwe, akamweleza yalivyokwenda. Sultani akasema, huyu yastahili kutiwa katika fumba akatoswa baharini, kwani hajui mema, yee amefanywa mema, amelipa maovu.