Swahili Tales/Kititi, na fisi, na simba

From Wikisource
Jump to navigation Jump to search
Swahili Tales  (1870)  by Edward Steere
Kititi, na fisi, na simba
English translation: The Hare, the Hyæna, and the Lion
[ 326 ]

KITITI, NA FISI, NA SIMBA.


Hapo kale aliondoka simba, na kititi, na fisi, wakafanya mashauri kuenenda mashamba kulima. Wakaenenda hatta mashamba, wakalima wakapanda vyakula, baadaye wakarejea katika maskani yao wakakaa.

Hatta ilipowadia wakati wa kuiva vyakula, wakanena, Na twendeni shamba, tukaangalie vyakula vyetu. Na hilo shamba lao lilikuwa mbali sana. Yule kititi akawaambia wenziwe, zamani tutakapokwenenda shamba tusisite katika ndia, atakayesita na aliwe. Wale wenziwe wakakubali maneno hayo.

Bassi wakaenenda hatta walipofika ndiani, yule kititi akasita. Wale wenziwe wakanena, Kititi amesita na aliwe. Yule kititi akasema, Je! kwamba nawaza. Wale wenziwe wakamwuliza, Wawaza nini? Akasema, Nawaza yale mawe mawili, moja kubwa na moja dogo, lile dogo halendi juu, wala lile kubwa halendi tini. Wale wenziwe wakanena, Ni kweli maneno haya.

Wakaenenda tena, walipofika mbele, kititi akasita tena. Wale wenziwe wakasema, Kititi amesita, na aliwe. Yule kititi akanena, Je! kwamba nawaza. Wale wenziwe [ 328 ]wakamwuliza, Wawaza nini. Akasema, Nawaza vile watu wakivaa nguo mpya, zile nguo kukuu kuenenda wapi? Wale wenziwe wakanena, Ni kweli maneno haya.

Wakaenenda tena, walipofika mbele fisi naye akasita. Wale wenziwe wakanena, Fisi amesita, na aliwe. Yule fisi akasema, Je! kwamba nawaza. Wale wenziwe wakamwuliza, Wawaza nini? Akasema, Siwazi hatta kitu. Wale wenziwe wakamtwaa fisi wakamla.

Akasalia simba na kititi, wakaenenda tena. Walipofika mbele wakaona mahali pana paango. Yule kititi akasita. Simba akasema, Kititi amesita, na aliwe. Yule kititi akasema, Je! kwamba nawaza. Simba akamwuliza, Wawaza nini? Akanena, Nawaza ile paango, hapo zamani za kale, wazee wetu walikuwa wakiingia kwa huku wakitokea kwa huku, nami nitakwenenda jaribu niingie kwa huku, nitokee kwa huku. Akaenenda akiingia kwa huku, akitokea kwa huku marra nyingi.

Akamwambia simba, Mzee simba, nawe enende ukajaribu uingie kwa huku utokee kwa huku. Yule simba akaenenda akaingia katika paango, akasakama asiweze kuenenda mbele wala kurudi nyuma. Yule kititi akaenenda maungoni mwa simba akamla nyama. Alipokwisha mla, yule simba akamwambia, Ndugu, unile upando wa mbeleni. Yule kititi akanena, Siwezi kuja kukula upande wa mbeleni, mato yaona haya.

Yule kititi akaenda zake, akamwata simba papale, na shamba lao akatwaa yeye.