Swahili Tales/Kisa cha punda wa dobi (parallel)

From Wikisource
Jump to navigation Jump to search
Swahili Tales  (1870)  by Edward Steere
Kisa cha punda wa dobi (Swahili and English in parallel)
Swahili text; English translation

[ 2 ]

KISA CHA PUNDA WA DOBI.

[ 2 ] Aliondokea kima akafanya urafiki na papa. Pana mti mkubwa, jina lake mkuyu, umeota katika kilindi, matawi yake nussu yako mjini, na nussu yako baharini. Yule kima kulla siku kwenda akila kuyu, na yule rafiki yake papa huwapo chini ya mti. Humwambia, utupie nami rafiki yangu vyakula; humtupia siku nyingi na miezi mingi.

Hatta siku hiyo papa akamwambia kima, fáthili zako nyingi, nataka twende kwetu nikakulipe fathili. Kima akamjibu, ntakwendaje, nasi hatuingii majini, nyama wa barra. Akamwambia, ntakuchukua, tone la maji lisikupate. Akamwambia, twende.

Wakaenda zao hatta nussu ya njia. Papa akamwambia, rafiki yangu weye, ntakwambia kweli. Akamwambia, niambie. Akamwambia, huko kwetu tunakokwenda, Sultani wetu hawezi sana, na dawa tumeambiwa ni moyo wa kima. Kima akamjibu, hukufanya vema usiniambie kulekule. Papa akamwuliza, ginsi gani?

Akafikiri kima akaona, nimekwisha kufa; sasa ntanena uwongo, labuda utanifaa.

[ 2 ]Papa akamwuliza, umenyamaza huneni? Akamwambia, sina la kunena, kwani usiniambie kulekule, nikapata [ 4 ]kuchukua moyo wangu. Papa akamwuliza, hapa, kunao moyo wako?

Huna khabari yetu? Sisi tukitembea mioyo yetu huacha mitini tukatembea viwiliwili tu, wallakini hutanisadiki, utaniambia nimeogopa, sasa twende zetu hatta huko kwenu, ukanichinje kama utauona moyo wangu.

Papa akasadiki, akamwambia kima, turudi sasa, ukatwae moyo wako. Kima akamwambia, sikubali, ela twende kwenu. Akamwambia, turudi kwanza ukatwae moyo wako, tupate kuenenda.

Kima akawaza—ni heri kumfuata hatta mtini, akili nnayo mwenyewe nikiisha fika. Wakaenda wakarudi hatta mtini, akapanda juu yule kima akamwambia, ningoje hapa, papa, naenda twaa moyo wangu, tupate kwenda zetu.

Akapanda mtini akakaa kitako kimya. Papa akamwita. Akanyamaza. Akamwita tena. Akamwambia, twende zetu. Kima akamjibu, twende wapi? Akamwambia, twende kwetu. Akamwambia, una wazimo? Papa akamwuliza, ginsi gani? Kima akamwambia, umenifanya punda wa dobi? Papa akamwuliza kima, ginsi gani punda wa dobi? Akamwambia, Ndiye hana moyo, wala hana mashikio. Papa akamwuliza, ginsi gani kisa cha punda wa dobi? Nambie, rafiki yangu, nipate kujua maana.

[ 4 ]Akamwambia, Dobi alikuwa na punda wake, akimpenda sana mwenyewe. Akakimbia punda akaingia mwituni siku nyingi, hatta akamsahao mwenyewe dobi. Akanenepa sana kule mwituni.

Akapita sungura, akamwona yule punda, mate [ 6 ]yakamtoka, akanena, nyama imenona hii. Akaenda akamwambia simba. Na simba atoka ugonjwani, amekonda sana. Sungura akamwambia, ntakuleta nyama kesho, tuje tule. Akamwambia, vema.

Sungura akaondoka, akaenda mwituni, akamwona punda, na yule punda mke. Akamwambia, nimetumwa kuja kukuposa. Na nani? akamwuliza. Akamwambia, na simba. Akakubali, akafurahi sana punda. Akamwambia, Twende zetu, bass.

Wakaenda zao, hatta wakafika kwa simba. Akawakaribisha simba. Wakakaa kitako. Sungura akamkonyeza simba, akamwambia, nyama yako hiyo imekwisha kuja, nami naondoka. Akamwambia punda, nnakwenda chooni mimi, zumgumzeni hapo na mumeo.

Simba akamrukia, wakapigana, akapigwa sana simba kwa mateke, naye akampiga makucha mengi. Akaangusha simba akakimbia punda, akaenda zake mwituni. Akaja sungura, akamwambia, Je! simba, umempata? Akamwambia, sikumpata, amenipiga kwa mateke amekwenda zake, na mimi nimemtia madonda mengi, sababu sina nguvu. Sungura akamwambia simba, tulia we.

[ 6 ]Wakakaa siku nyingi, hatta punda akapona madonda yale, na simba akapata nguvu sana. Akaenda sungura kwa simba, akamwambia, waonaje sasa, nikuletee nyama yako? Akamwambia, kaniletea ntaikata vipande viwili.

Akaenda sungura mwituni. Punda akamkaribisha sungura, akamwuliza khabari. Akamwambia, na mchumba wako anakwita. Punda akamwambia, siku ile umenipeleka, amenipiga sana kwa makucha, naogopa sasa. [ 8 ]Akamwambia, hapana neno yalio ndio mazumgumzo ya simba. Akamwambia, twende zetu, bass.

Wakaenda hatta wakafika. Simba alipomwona tu, akamrukia akamkata vipande viwili.

Hatta sungura alipokuja, akamwambia, chukua nyama hiyo ukaoke, wallakini sitaki kitu mimi, ela moyo na mashikio ya punda. Sungura akamwambia, marahaba. Akaenda akaoka nyama mahala mbali, simba hamwoni. Akatwaa moyo ule na mashikio akala yeye sungura, hatta akashiba. Na nyama ngine akaziweka.

Akaja simba, akamwambia, niletee moyo na mashikio. Akamwambia, yako wapi? Simba akamwuliza, kwa nini? Akamwambia, huyu punda wa dobi, huna khabari? Akamwambia, ginsi gani kutoa kuwa na moyo na mashikio? Akamwambia, wewe simba mtu mzima hayakuelei? Kama ana moyo huyu na mashikio, angalikuja tena hapa? Kwani marra ya kwanza amekuja akaona atakuuawa, akakimbia, marra ya pili amekuja tena, bassi kama ana moyo angalikuja? Simba akamwambia, kweli maneno yako.

[ 8 ]Bassi kima akamwambia papa, nawe wataka unifanye mimi punda wa dobi, shika njia wende zako kwenu, mimi hunipati tena, na urafiki wetu umekwisha. Kua heri.