Swahili Tales/Kisa cha mwewe na kunguru

From Wikisource
Jump to navigation Jump to search
134776Swahili TalesKisa cha mwewe na kunguru1870Edward Steere
[ 364 ]

KISA CHA MWEWE NA KUNGURU.


Aliondoka Sultani ya kunguru, akampelekea waraka Sultani ya mwewe, akamwambia, nataka uwe asikari yangu. Akamwambia sikubali. Akamwambia, kama hukubali tutapigana, mimi nawe. Akamwambia, na tupigane, ukinishinda nitakufuata, nikikushinda weye utanifuata.

Wakapigana, kunguru wakashindwa. Akaondoka mzee mmoja, akawaambia—tukimbie. Wakakimbia katika mji wao, wakaenenda mji mgine. Mwewe walipokuja wasimwone mtu, wakakaa katika mji wa kunguru.

Hatta siku nyingi kunguru wakafanya shauri. Akaondoka mzee, akasema, ninyonyoeni manyoya mkanitupe mjini mwa mwewe. Wakamnyonyoa, wakaenda, wakamtupa.

Walipopita mwewe, wakamwona, wakamwambia, wafanya nini huku mjini kwetu? Akawaambia, wenzangu wamenipiga wamenitoa mji kwa sababu nimewaambia, mfuateni mwewe.

Wale wakamchukua, wakaenda naye kwa Sultani yao, wakamwambia, huyu kunguru tumemwokota, naye mwulize, atasema maneno yake.

[ 366 ]Sultani akamwuliza, akamwambia, wenzangu wamenipiga, wamenitoa mji kwa sababu naliwaambia kweli, mfuateni mwewe, ndio Sultani, wakanipiga. Sultani ya mwewe akamwambia, kaa kitako hapa.

Akakaa kitako siku nyingi. Hatta siku moja wakaenda kanisani, nayee wakamchukua, wakasali pamoja, hatta walipotoka, wakamwuliza, sisi na ninyi, nani anaabudu sana Muungu? Akawaambia, ninyi.

Akakaa kitako wakampenda sana. Hatta siku kuu yao ikikaribia, akatoka usiku, akaenda, akawaambia wenziwe, kesho watakwenda kanisani wote, njooni nje ya mlango wa kanisa, mutie moto. Wale wakatoka, wakaenda kutafuta kuni na wangine wakachukua moto.

Hatta assubui wakaenda zao kanisani, asisalie mtu katika mji, ela yule mzee kunguru. Wakamwambia, kwa nini huenendi kanisani leo? Akawaambia, tumbo linaniuma sana. Wakamwambia, bass. Akaenda, akawaita wenziwe. Akawaambia, wamekwisha kuingia kanisani wote.

Wakaenda wale, wakatia kuni katika mlango wa kanisa, na wangine wakatia moto. Moto ukawaka. Wakaona moshi waingia ndani ya kanisa, wakakimbia madirishani na wangine wakafa wengi sana na Sultani pia akafa. Kunguru wakatwaa mji.

Wale waliobaki mwewe wakawakimbia kunguru hatta leo.