Page:Swahili tales.djvu/366

From Wikisource
Jump to navigation Jump to search
This page has been proofread.
346
HASSIBU KARIM AD DINI.

Naye nabii Sulimani anangojewa na Majini. Wakakaribia wale wawili, wakasikia mtu anasema. Na nabii Sulimani amelala na mkono ameuweka kifuani, na pete kidoleni. Yule mtu akamwambia, akamwita Bolukia, unakwenda wapi weye? Akamwambia, nimefuatana na Alfán, anakwenda twaa pete ile. Akamwambia, rudi weye, huyu atakufa.

Alfán akamwambia Bolukia, ningoje hapa weye. Akaenda yee, akikaribia kutaka kushika pete, akapigiwa ukelele, akarushwa hapa hatta kule. Akarudi, asikubali, akaenda marra ya pili akataka kuishika pete, akapuziwa, akateketea kamma jifu.

Na yule Bolukia anaona pia, akasikia mtu akimwambia, rudi, enda zako, huyu thalimu amekwisha kufa.

Akarudi Bolukia, akaja zake hatta njiani akaona bahari, akapaka dawa yake miguuni, akavuka, akaenda kisiwa kingine, hatta akaisha akapaka dawa tena akavuka. Ikawa ndio kazi yake siku nyingi sana, na miezi mingi, na miaka mingi inakwisha naye njiani.

Akaenda hatta siku moja akamtokea mtu, akamwona amekaa kitako, akampa salaam, naye akamjibu. Akamwuliza, weye nani? Akamwambia, mimi, jina langu, Jani Shah, weye nani? Akamwambia, mimi Bolukia, akamwuliza, wafanya nini hapa?

Pana makaburi mawili, na yule mtu amekaa katikati ya makaburi, hulia sana, kiisha akacheka, akashukuru Muungu. Akamwuliza, nipe kisa chako wewe. Akamwambia, kisa changu kikubwa, lakini nipe chako weye kwanza, umetoka wapi, unakwenda wapi?