Page:Swahili tales.djvu/164

From Wikisource
Jump to navigation Jump to search
This page has been proofread.
144
KISA CHA KIHINDI.

enenda kauze kofia hii kwa Sultani, ndipo utakapopata thamani. Akaenda akauza.

Alipoiona yule Sultani, akajua kazi ile ya kofia ni ya bwana wake. Akasoma na yale mashairi, akayajua maana yake, na maana yake hii:

Ajabu ya Muungu,
Mmoja ametwaliwa na maji,
Mmoja ametwaliwa na papa,
Mngwana nimefungwa,
Mtumwa wangu amepata usultani,
Ajabu ya Muungu.

Akamwuliza yule bedui, umeipata wapi kofia hii? Akamwambia, mke wangu ndiye aliyeifanya. Akampa reale khamsini, akamwambia, mwambie mkewo anifanyie nyingine. Akaenda zake yule bedui.

Akatoa askari, akawaambia, mfuateni nyuma, mkimwona nyumba atakayoingia, mrudi, mje mniambie. Wakamfuata hatta kwake. Akaingia ndani. Wale asikari wakarudi. Wakaenda wakamjibu Sultani. Wakamwambia, tumeiona nyumba yake.

Wakatolewa askari mia, wakaenda kwake. Akawaambia, mkamateni mmfunge na watu wote waliopo kwake 'mwalete, kama mje nao. Wakaenda, wakamkamata, wakamfunga, wakaja naye, na watu wote waliomo nyumbani. Akaulizwa, wee ndiyo kazi yako, kukamata watu ukiwafunga nyumbani mwako, kupata kuwachinja, ukiwalisha watu? Asiweze kukana. Wakaulizwa wale, wakanena ndiyo kazi yake. Akafungwa gerezani.

Akamtwaa yule bwana wake, akawaamrisha watu wakamwoga, akampa nguo, akavaa. Akampa chakula, akala,